AFYA NA UZAZI WA MPANGO,KANDA YA ZIWA WABADILIKA
Na. Mashaka Bartazar.
Mwanza.
Dira ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 ni kuwa na jamii yenye afya bora na ustawi, ili kuweza jamii kuhangia maendeleo ya nchi na mtu mmoja mmoja.
Bila kuwa na jamii yenye afya bora ni vigumu kwa taifa lolote kupiga hatua za maendeleo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi,kisiasa na kijamii.Ukizingatia kuwa ili taifa liendeelee linahitaji watu,ardhi ,siasa safi na uongozi bora.
Hivyo ungana na Baltazar Mashaka, katika makala hii inayohusiana na afya ya uzazi wa mpango, hasa katika kuzuia vifo vya akina mama wajawazito na watoto wa umri chini ya miaka mitano na kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Ni katika mkutadha huo Serikali katika sera yake ya mwaka 2007 inasema kuwa kuwa upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendea kazi ni muhimu katika utoaji huduma za afya kwa jamii.
Takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinaonyesha kuwa wanawake wajawazito 454 wanakufa kila mwaka kati ya akinamama 100,000 wanaojifungua.
Idadi hiyo ni kubwa mno, inapaswa kupungua kwa serikali kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya afya ya uzazi wa mpango na kupunguza vifo hivyo ambavyo si vya lazima.
Lakini pia kwa kuzingatia athari za kukosekana kwa afya ya uzazi wa mpango ipo haja kwa halmashauri kutenga fedha kwa ajili uzazi wa mpango.Asilimia 76 ya bajeti ya Serikali katika sekta ya afya kwa mwaka inategemea wafadhili,wakati yenyewe ikichangia kiasi kdogo cha asilimia 24.
“Ni hatari kwa maisha ya akina mama wajawazito wanaopoteza maisha kila mwaka kutokana matatizo ya uzazi.Wabunge na madiwani wafikirie maisha ya wanawake na watoto,watenge na kupitisha bajeti zinazokidhi mahitaji ili kunusuru maisha yao,”anasema Dkt. Makunja wa Hospitali ya Teule ya Bunda
Wakati sera ya serikali ikieleza hayo, bado kuna changamoto kubwa kwa upande wa afya ya uzazi na uzazi wa mpango katika jamii.Wananchi wengi bado hawana elimu ya kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika maeneo hayo mawili kutokana na mila na desturi.
Mila na desturi kwa baadhi ya makabila huchukua nafasi kubwa,kwamba mwanaume hana nafasi ya kushiriki uzazi wa mpango ama kumsindikiza mkewe kliniki ya uzazi wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua.
*
Hali hiyo imeanza kupungua katika baadhi ya mikoa hasa Mwanza,ambapo wanaume sasa wanaongozana na wenzi wao kwenda vituo vya afya kupima na kupata elimu ya uzazi wa mpango.
Wajawazito waliombukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU) pamoja na wenzi wao wanaoambatana kwenda vituo vya afya na zahanati kupima afya wanapata elimu ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT), jambo ambalo linaonyesha kuwapo kwa mwamko kwa wanaume kushiriki afya ya uzazi.
Nilimeshuhudia mara kadhaa, baadhi ya wanaume wakiwa wamebeba watoto kuwapeleka kwenye vituo vya afya na zanahati kupima uzito ama kupata tiba.Kadhalika kuwasindikiza wenzi wao wakati wa ujauzito jambo ambalo hapo zamani ilikuwa nadra kwa mwanaume kufanya hivyo.
Wataalamu wa afya ya uzazi na uzazi wa mpango wanashauri baba kushiriki kikamilifu afya ya uzazi ,kupima afya,kumsindikiza mama kwenda kliniki, na kupanga taratibu za mama kuhudhuria kliniki muda wote wa ujauzito hadi kujifungua.
Ushiriki wa wanaume katika suala la afya ya uzazi kama nilivyotangulia kusema mwanzo,umeongezeka kwa asilimia 24 mwaka 2011 kutoka asilimia 20 mwaka 2009.
Takwimu hizo zilitolewa na Mganga Mkuu wa hospitali ya mkoa wa Mwanza, Dkt.Valentino Bhangi,wakati akitoa ufafanuzi wa hali hiyo kwa mwandishi wa makala hii.
Mbali na hilo Dkt Bhangi anasema kuwa,vifo kwa akianamama wajawazito vinavyotokana na uzazi wakati wanajifungua,mkoani hapa vimepungua kutoka vifo 200 na kufikia vifo 160 mwaka jana.
Jitihada bado zinafanyika ili vifo vya aina hiyo vipungue zaidi ya hapo,ambapo takwimu za taifa zinaonesha kuwa akinamama wajawazito 100000 kati yao 454 hupoteza maisha kila mwaka wakati wa kujifungua.
Lakini pia lipo tatizo la ukosefu wa vifaa tiba na vitendea kazi katika vituo vya afya na zahanati nyingi hasa za maeneo ya vijijini,mfano kifaa cha kumsaidia kupumua mtoto mchanga anayezaliwa akiwa amechoka.
Ukiachilia mbali hilo kuna suala la kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.Upo uwezekano mkubwa kwa mama mjamzito mwenye VVU kumwambukiza mwanaye wakati wa kujifungua.
Ili kudhibiti hali hiyo upo utaratibu wa kupima afya na kupata ushauri na tiba kwa wanaoibainika kuwa na VVU,tangu wakati wa mimba hadi kujifungua .
Wanawake wajawazito 122,000 hupata maambukizi ya VVU kila mwaka na kusababisha watoto 48,800 kuambukizwa virusi hivyo kutoka kwa mama wakati wa kuzaliwa ama kunyonyeshwa na mama zao.
Mratibu wa mradi wa Tuunganishe Mikono Pamoja (JPI) Agapiti Manday anasema, serikali kwa kushirikiana na watu wa Marekani imeweka mkakati kamambe wa kuhakikisha baba au mama anashiriki kikamilifu kuhusu afya ya uzazi.
Mradi huo ambao unaendeshwa na taasisi ya Afya ya Aga Khan, ni kuhakikisha baba,mama wanashirikiana katika kupata huduma ya tiba kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) baada ya kupima afya zao na kubainika kuwa na VVU ili kuwakinga watoto wasipate maambukizi hayo.
Huduma hizo za PMTCT ni pamoja na kupata shauri na upimaji wa VVU, ushauri kuhusu lishe ya mtoto anayezaliwa na mama mwenye maambukizi ya VVU,matumizi sahihi ya dawa na huduma bora na salama wakati wa kujifungua na ufuatiliaji wa mama na mtoto baada ya kujifungua.
Mama mjamzito mwenye VVU anaweza kuzuia kabisa maambukizi hayo kwenda kwa mtoto endapo atahudhuriia kliniki ili apate ushauri wa namna ya kumkinga mtoto aliyetumboni,kupata ushauri wa jinsi gani amshirikishe mwenzi wake umuhimu wa kupima VVU ili kujitambua kama hajapima.
Kama hajapima atashauriwa kuhusu mambo mengine muhimu yanayohusu afya ya uzazi ,atapatata unasihi kutoka kwa wataalam kuhusu unyoneshaji wa mtoto atakayezaliwa na mama mwenye VVU.Mama atapewa dawa katika muda muafaka kabla na baada ya mtoto kuzaliwa ili kuzuia asiambukizwe.
Kwa mujibu wa Dkt Bhangi kati ya wanawake asilimia 25 hadi 45 wenye VVU waliopata ujauzito wanaweza kuwaambukiza watoto wao ambao hawajazaliwa bado.Kinachotakiwa kwao ni kupata ushauri wa kitaalam na dawa kupunguza hatari ya kuwaambukiza watoto wao wakiwa tumboni au wakati wa kuzaliwa.
Sera ya serikali ya mwaka 2006 inasistiza umuhimu wa kupunguza maambukizi ya VVU ya mama mjamzito kwenda kwa mtoto,hivyo ni wajibu wa serikali,baba,mama na jamii yote kusimama pamoja kupiga vita maambukizi mapya ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Ni kutokana na kadhia hiyo, Mkakati wa kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto (PMCT) umeweza kusambaza asilimia 70 ya dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs) kwa akina wajawazito wanaoishi na virusi hivyo, sawa na asilimia 92 ya wanawake wenye VVU.
Binadamu anapokumbwa ama kuambukizwa VVU, husababisha mwili kuathiriwa hivyo kuwa rahisi kushambuliwa kwa chembechembe nyeupe (kinga) za damu ambazo hupigana na maadui wanaoushambulia mwili.
Chembechembe hizo nyeupe zinaposhambuliwa na kukosa nguvu ndiyo chanzo cha kushambuliwa na maradhi mbalimbali nyemelezi na kuufanya mwili uhitaji virutubisho ikiwa ni pamoja na kuboresha lishe ya kusaidia kuimarisha kinga ya mwili na kupunguza makali ya Ukimwi.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.