MAAMBUKIZI YA VVU
TOKA KWA MAMA MJAMZITO
KWENDA KWA MTOTO YANAWEZA KUEPUKWA
Edwin Soko
Mwanza
Tafiti zinaonyesha
kwamba kuna uwezekano mkubwa wa
mama mjamzito kumwambukiza mwanae Virusi Vya Ukimwi (VVU), endapo mama
atakuwa anaishi na Virusi Vya
ukimwi kama hakutakuwa na mipango mathubuti
ya kimkinga mtoto aliye tumboni kupitia mpango wa kuzuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi toka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto(PMTCT).
Baba ana nafasi ya kumpenda mkewe akiwa mjamzito |
Mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza,
bwana Valentino Bangi, alisema kuwa, virusi vya ukimwi vinaweza
kusambazwa kutoka kwa mama mjamzito aliyeambukizwa, hadi kwa mtoto tumboni kwa
njia kuu tatu. Njia ya kwanza wakati mtoto yungali tumboni mwa mama, ambapo
virusi vinaweza kusambaa kutoka kwa mama hadi kwenye nyumba ya uzazi.
Pili ni wakati wa kujifungua, ambapo mtoto anaweza
kuingiwa na majimaji ya ukeni au majimaji mengine kutoka kwa mama. Tatu ni wakati wa kunyonyesha, ambapo virusi vinaweza
kuambukizwa kupitia maziwa anayonyonya mtoto.
Kwa mujibu wa
UNICEF, uwezekano wa kumwambukiza mtoto wakati wa kujifungua ni mkubwa zaidi kama mama
ana ujazo mkubwa wa virusi mwilini mwake na kinga yake tayari ni dhaifu.
Kabla
ya mwanamke aliyeambukizwa kupewa usaidizi wowote wa kimatibabu kwanza
atafanyiwa uchunguzi wa damu kuona kima cha virusi ndani ya mwili na hali yake
ya kinga kwa ujumla. Kama kinga yake itakuwa thabiti na idadi ya virusi ni
ndogo mwilini, huenda hatahitaji dawa mpaka kipindi cha mwisho mwisho cha uja
uzito yaani baada ya wiki ya 24.
Lakini kama
ujazo wa virusi ni mkubwa na kinga mwili ni dhaifu, huenda italazimu kutumia
madawa maalumu ya kupunguza makali ya
ukimwi, mapema ili kupunguza uwezekano wa kumwambukiza mtoto.
Tanzania ni
moja kati ya nchi
zilizo mstari wa mbele kutekeleza
mkakati wa kuzuia maambukizi ya
Virusi Vya Ukimwi
toka kwa mama mjamzito
kwenda kwa mtoto(PMTCT) kupitia huduma zitolewazo na mkakati huo. Hali hiyo imepelekea kushuka kwa maambukizi toka
kwa mama kwenda kwa mtoto sanjali na vifo vya
kina mama wajawazito
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid
alibainisha kwenye maadhimisho ya
siku ya
utepe mweupe yaliyofanyika duniani kote na kitaifa
kufanyika mkoani Mwanza machi
15 mwaka huu kuwa, vifo
vya kinamama vinavyotokana na uzazi
vimeshuka kutoka 200 kwa mwaka 2006 hadi
kufikia vifo 160 kwa mwaka 2012. Hali
hiyo imsababishwa na
kuongezeka kwa huduma ya PMTCT.
Nchini Tanzania kwa mujibu wa kituo cha kuzuia
maambukizi toka kwa mama mjamzito
kwenda kwa mtoto, kiliainisha takwimu
zinaonyesha kuwa, wanawake wajawazito wanaopata huduma ya PMTCT imeongezeka
toka 34% kwa mwaka 2007 hadi 80%
kwa mwaka 2012. Nchini Kenya kwa mujibu wa UNICEF pia idadi imeongezeka toka 56%
kwa mwaka 2008 hadi 74% kwa mwaka 2008. Nchini Uganda
ungezeko ni 27% kwa mwaka 2007 hadi 50% kwa mwaka 2011, kwa mujibu wa ripoti ya
wizara ya afya ya Uganda.
Dira ya maendeleo
ya Taifa 2025 kipengele cha tatu
cha ustawi wa jamii kinasisitiza
kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na lengo
la tano la malengo ya
millenia linasisitiza kuimarisha huduma za kinamama wajawazito,
lengo hilo zikitekelezwa vyema ni wazi kwamba hatari ya kumwambukiza mtoto
virusi vya ukimwi inaweza kupunguzwa hadi kufikia kati ya asilimia, moja na
asilimia mbili tu kama hatua zifuatazo zitazingatiwa. Kupata matibabu ya
kupambana na virusi vya
ukimwi, kuzaa kwa njia ya upasuaji na kutonyonyesha kama
mama atabainika kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Sera ya Taifa
ya kuthibiti ukimwi (2001) katika
lengo lake la kwanza inasisitiza juu ya
kuzuia na kuenea kwa ukimwi, hivyo basi
ni wajibu baba na jamii nzima kuzuia
maambukizi toka kwa mama kwenda
kwa mtoto ili kuwaokoa watoto wasiambukizwe virusi hivyo.
Sera ya afya ya Taifa ya mwaka 2007 moja ya lengo lake kati ya
malengo tisa ni kupunguza maradhi kwa wakina mama wajawazito na watoto na
kuongeza umri wa kuishi. Huenda
lengo hili likawa linatia matumaini kupitia takwimu, kwani Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa,
UNICEF linabainisha kwamba, maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama
kwenda kwa mtoto yamepungua kwa 24% katika nchi ishirini na mbili na nyingi kati
ya hizi ni zile ambazo ziko Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Mkakati wa Pili wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI
(2008-2012) umehusisha mchakato wa Ushirikiano wa wadau mbalimbali, kama
mashirika asasi na watu
binafsi katika kupunguza maambukizi
ya Virusi vya
ukimwi.
Shughuli
nyingi za kuzuia maambukizi toka
kwa mama kwenda kwa
mtoto (PMTCT) nchini Tanzania zimekuwa vikiungwa mkono na mfuko wa dharura wa Rais wa Marekani wa
kupunguza maambukizi ya Virusi
Vya Ukimwi( U.S President’s
Emegence Plan for AIDS Relief ) kupitia
shirika la Engender health ambalo
umekuwa ukitoa elimu kuhusiana na
afya ya uzazi wa mpango, kutoa mafunzo kwa wadau juu
ya afya ya uzazi wa mpango na uzazi salama.
Mkakati huo unatukumbusha wajibu wa baba, mama na
jamii nzima kushirikiana na kutumia huduma ya kuzuia maambukizi ya Virusi Vya
Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) ili kuwakinga watoto wasipate
maambukizi hayo. Huduma za PMTCT ni pamoja na ushauri na upimaji wa Virusi Vya
Ukimwi. Pia ushauri kuhusu ulishaji wa
mtoto aliyezaliwa na mama aliyeambukizwa Virusi Vya Ukimwi, matumizi sahihi ya
dawa (ARV) za kuzuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi; huduma bora na salama
wakati wa kujifungua na ufuatiliaji wa mama na mtoto baada ya kujifungua.
Katika kujali
hilo Tanzania tarehe 1 Desemba 2012 mheshimiwa Rais Jakaya
Mrisho Kikwete alizindua mpango wa kupunguza maambukizi ya VVU toka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa mwaka 2012 – 2015. Mpango huo una lengo la
kupunguza maambukizi mapya kwa
watoto na kumfanya mama kuendelea kuishi salama.
Kuhakikisha programu ya kuzuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi
toka kwa mama kwenda kwa mtoto
(PMTCT) inafanikiwa ni lazima hatua
zote muhimu zifuatwe, kama kuhudhuria kliniki, kupatikana kwa vipimo, kukubali kupima,kupata majibu, kupatikana kwa
dawa, kukubali dawa, kumeza dawa, dawa kwa mtoto na lishe salama
Hatua mbalimbali za kufuatwa ili kukamilisha programu ya PMTCT) |
Makala haya yameandaliwa kwa msaada mkubwa wa sera ya Afya ya Taifa (2007),Sera ya Taifa ya kuthibiti ukimwi(2001), Dira ya maendeleo ya Taifa (2005), Mkakati wa pili wa kuthibiti UKIMWI(2008-2012), Mkakati wa PMCT wa Kenya, Malengo ya Millenia 2015, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, Tume ya kuthibiti UKIMWI Tanzania. Mkakati wa kutathimini hali ya PMTCT Tanzania . Mpango wa Uganda wa kupunguza maambukizi mapya miongoni mwa watoto ifikapo mwaka 2015 na kuwaweka mama zao salama.
Kwa
maoni na ushauri juu ya makala hii wasiliana na mwandishi
kupitia Simu No.0754
551 306
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.