CHANZO:- MWANANCHI
Dar es Salaam. Ni wazi kuwa mchango wa pombe kwenye kukuza uchumi wa nchi ni mkubwa, hasa kwenye nyanja ya kodi na ajira. Mpaka sasa mchango huo upo hatarini kupotea kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa bidhaa hiyo.
Ripoti ya ‘Tanzania in figures 2021’ inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha uzalishaji wa bia nchini umeshuka kutoka lita milioni 386 mwaka 2020, hadi lita milioni 380, ikiwa ni sawa na anguko la asilimia 1.5.
Kwa upande wa pombe aina ya konyagi nayo uzalishaji wake umeporomoka kutoka lita milioni 33 mwaka 2020, hadi lita milioni 22 mwaka 2021, sawa na kushuka kwa asilimia 33.
Hata hivyo, takwimu zinaonyesha mwenendo wa uzalishaji bia ulianza kushuka tangu mwaka 2019 ambapo lita milioni 391 zilizalishwa ikilinganishwa na lita milioni 413 za mwaka 2018 sawa na anguko la asilimia 5.3.
Akizungumzia sababu za kushuka kwa uzalishaji wa bia nchini, Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Messiya Mwangoka alisema upungufu wa malighafi za kutengenezea bia, ikiwamo ngano na shayiri ndiyo chanzo cha anguko hilo.
“Sababu kubwa inayopunguza uzalishaji wa bia ni ukame uliopunguza upatikanaji wa ngano na shayiri na vita ya Ukraine na Russia imeongeza shida, tofauti na awali, hivyo lazima uzalishaji wa bia utapungua zaidi,” aliongeza.
Akilizungumzia hilo, Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Timothy Lyanga alisema kama malighafi ndiyo kigezo cha kupungua kwa uzalishaji, watu wa ndani wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo.
Dk Lyanga alisema suala hilo litawezekana kwa kufufua mashamba yaliyopo maeneo mbalimbali, yazalishe zaidi ili kuhakikisha viwanda vinaendeshwa kupitia bidhaa za ndani.
“Hili pia litapunguza utegemezi wa malighafi kutoka nje ambazo wakati mwingine huuzwa kwa bei kubwa na kufanya gharama za uzalishaji kuongezeka,” alisema.
Mbali na kushuka uzalishaji pombe, pia uzalishaji ngano inayotumika kwa kiwango kikubwa kuzalishia kinywaji hicho umeshuka kwa asilimia 9.4 kwa mwaka 2020 hadi 2021. Mwaka 2020 zilizalishwa tani 77.2 za ngano hapa nchini, kabla ya kushuka hadi tani 70 mwaka 2021, huku 2018 uzalishaji ulikuwa tani 57 na tani 63 mwaka 2019.
Wakati uzalishaji pombe ukishuka, upande wa pombe haramu aina ya gongo na pombe kali zisizo na vibali kesi zake zimeongezeka kwa asilimia 30.8 mwaka 2021 ikilinganishwa na 2020.
Ripoti hiyo imeonyesha kuwa kesi za pombe haramu mwaka 2021 zilizorekodiwa na Jeshi la Polisi ni 6,022, huku zikiongezeka kutoka kesi 4,602 mwaka 2020.
Kwa upande wa Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema: “Serikali itashirikiana na Tume ya Ushindani (FCC) katika msako dhidi ya wafanyabiashara wa pombe haramu, ili kuweka usawa katika soko.
Akizungumzia ongezeko la uzalishaji pombe haramu, mchambuzi wa kujitegemea wa uchumi, Dk Rose Samson alisema: “Inasikitisha kuongezeka kesi za pombe haramu, muhimu kujua nini sababu, kama ni mikakati iliyosukwa kwa ajili ya kukandamiza uzalishaji au ni kwa ajili ya watu kupata fedha za haraka.
“Nashauri kubadili mbinu ya kukabiliana na pombe haramu kwa sababu idadi kubwa ya watu nchini ni vijana ambao hali yao ya kifedha haiwaruhusu kununua pombe halali, wanaangukia kwenye pombe haramu”.
Gazeti la Mwananchi liliwahi kumkariri Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Mesiya Mwangoka akisema: “Tanzania Distilleries Limited (TDL), kampuni tanzu ya TBL, inapoteza wastani wa Sh19.5 bilioni kila mwaka kutokana na uwepo wa pombe haramu”.
Naye Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL), John Wanyancha alisema watu wengi wanatumia pombe haramu kutokaa na bei yake kuwa ndogo.
Watumiaji wa pombe kali za bei rahisi na haramu wanena
“Bia moja Sh1,500 hadi Sh4,000 huko, unaingiza shilingi ngapi kwa siku hadi utumie Sh10,000 kunywa bia za kukutosha na maendeleo mengine utafanya saa ngapi. Lakini hizi pombe nyingine kuna za Sh700, Sh1,000, Sh500 kulingana na aina ya pombe unayohitaji, hii inakuwa ni rahisi kuliko bia,” alisema Peter Jimhan.
Naye Joackim Kigua alisema zamani walikuwa wanakunywa bia kwa sababu bei yake ilikuwa afadhali, “Unaweza ukawa huna hela kabisa lakini unapata chako cha buku (kipimo cha Sh1,000) ikakupa usingizi kidogo kuliko kutokunywa kabisa,” anasema.
Kampuni ya TBL pekee mwaka 2021 ilitoa Sh472 bilioni kwa Serikali kama gawio, ikiwa ni ongezeko la asilimia mbili ikilinganishwa na Sh463 iliyoitoa mwaka 2020.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.