ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, March 1, 2018

SIKILIZA KISA HIKI CHA MTANGAZAJI WA JEMBE FM WAKATI WA KUADHIMISHA SIKU YA KUPINGA VITENDO VYA UBAGUZI NA UNYANYAPAA DUNIANI 2018


#Binadamu hutofautiana kwa Mawazo na Mtazamo na sio Magonjwa, Maradhi, Jinsi, Ulemavu wala Rangi, sikiliza kisa hiki anachosimulia Johari Ngassa wa Jembe Fm alipofanya mahojiano na KAZI NA NGOMA wakati @jembefm ikiungana na Dunia kupinga unyanyapaaji wa binadamu katika hali yoyote ile. 

Kwa kauli thabiti twasema "Tusiwanyanyapae Tuwapende na Kuwajali, Upendo na Heshima ndio #Utu wetu #Ndichotulichofunzwa #Paza sauti tukatae Unyapaaji katika siku hii ambapo Dunia nzima tunaadhimisha #worlddiscriminatinday"

MADA: UNYANYAPAA NA UBAGUZI
                                           (Stigma & Discrimination)
IMETAYARISHWA NA: SHEIKH ZAHOR SALEH OMAR
KATIBU MKUU ZANZIBAR CHILDREN’S FUND ALIPOKUWA AKITOA MADA YA UNYANYAPAA NA UBAGUZI KATIKA SEMINA YA MAIMAMU NA WALIMU WA MADRASA. MWAKA 2005 KATIKA UKUMBI WA ZCF CHAKE CHAKE PEMBA.
VIPENGELE:
Maana ya Unyanyapaa na Ubaguzi
Sababu za Kuwepo Unyanyapaa na Ubaguzi
Mtazamo wa Kiislamu Kuhusu Unyanyapaa na Ubaguzi
UNYANYAPAA NI NINI?
Unyanyapaa au fedheha (stigma) ni hali inayomfanya mtu ajihisi ana kasoro au aibu.
Hali hii ina athari zake kwa wahusika watakavyojihisi au kubugudhiwa na wengine.
UBAGUZI ni athari mbaya zitokanazo na unyanyapaa na kupelekea mtu kudhulumiwa, kujihisi mpungufu, mhalifu na aliyetengwa na jamii.
Kuwepo kwa unyanyapaa na ubaguzi kunaharibu au kudhoofisha juhudi zinazofanywa katika hatua nyengine pia za kupingana na UKIMWI, kama vile taaluma na njia za kujikinga, kutoa huduma kwa waathirika, matibabu au hatua za kupunguza athari za mripuko wa maradhi. Matokeo yake ni kuongezeka kwa balaa litakalowaelemea watu fulani peke yao tu iwe ni familia au kundi.
Kwa vile hali hii ya unyanyapaa na ubaguzi inaonekana kukita kwa kiwango kikubwa katika jamii zetu, basi hatuna budi sote kwa pamoja kuungana kuitokomeza tabia hii.
Ili kupata angalau hisia za muathirika wa unyanyapaa na ubaguzi, hebu na tuangalie mifano hii ifuatayo:
MAHALA PA KAZI:
Mfanyakazi aliyeambukizwa na UKIMWI anaweza kukoseshwa haki zake kwa kusimamishwa kazi, kutopandishwa cheo, au kuzuiliwa nafasi za mafunzo, pamoja na kutengwa na wafanyakazi wenzake.
HUDUMA ZA AFYA:
Aliyeathirika na UKIMWI inawezekana akatengwa au kubugudhiwa kwa matusi na watoa huduma za matibabu, pia huweza kudharauliwa wakati ambapo msaada wa huduma hiyo muhimu unahitajika zaidi kwa hali yake.
DURU ZA KIDINI:
Mgonjwa mwenye UKIMWI anatazamwa na wengi kwa mtazamo wao wa kidini kama mhalifu, kwa hivyo anakosa kushirikishwa katika shughuli za kijamii kadri anavyostahiki.
KATIKA MASHULE:
Watoto walioathirika kwa UKIMWI, nao hali ya kuwa si wenye hatia kwa namna yoyote ile, hawatasilimika na kushambuliwa kwa matusi, kero na kudharauliwa.
KATIKA FAMILIA:
Suala hili likiendelea kuwepo katika familia basi athari zake huwa ni mbaya zaidi hususan kuhusiana na kinga na kutoa huduma.
Pasipochukuliwa hadhari ndani ya familia ndipo sawa ya gonjwa hili na mafuta yanapomwagiwa mafuta na mripuko wake kuongezeka.
JINSIA:
Matatizo ya wanawake mara nyingine hutofautiana na yale ya wanaume. Wanawake mfano wa vizuka wanakuwa ni wahanga wa unyanyapaa na ubaguzi.
Hii ni hali ya kuwanyanyasa kijinsia pasina kuwepo sababu. Unyanyapaa unaweza kusababisha pia wanawake wasichukue hatua za kujikinga na maambukizi kutoka kwa waume wao.

SABABU ZA KUWEPO KWA UNYANYAPAA NA UBAGUZI
Ziko sababu kadhaa zinazofanya hali hii iwepo na iendelee kuwepo. Baadhi yake na siyo zote ni hizi zifuatazo:
1. Kutofahamu kabisa au kikamilifu kuhusiana na UKIMWI na athari zake.
2. Kuwepo aina fulani ya hofu au wasiwasi juu ya kujitambulisha au kuwatambulisha walioambukizwa na UKIMWI.
3. Matamshi yanayowakabili waathirika ya kuwalaani na kuwasimanga badala ya kuwaliwaza na kuwasaidia.
4. Kuhusishwa kiholela baina ya UKIMWI na masuala ya ngono.
5. Itikadi za kidini ambazo zimekosa upeo sahihi wa kufahamu juu ya suala la UKIMWI.
MTAZAMO WA KIISLAMU JUU YA UNYANYAPAA
Japokuwa inakubalika Kiislamu kusema kuwa UKIMWI ni adhabu itokanayo na kuenea kwa uasharati kama ilivyo sababu mojawapo kuu ya kuenea kwa maradhi haya, lakini kuna wajibu wa kuchukua hatua za makusudi za kupunguza athari zake kwa vile waathirika ni jamii yote kwa ujumla – aliyemo na asiyekuwemo.
Waumini wa dini ya Kiislamu wamelazimika kushiriki kampeni dhidi ya UKIMWI katika nyanya zake tofauti, zikiwemo taaluma za kujikinga, kutoa huduma, kufanya mbiu shawishi (advocacy), kupunguza arthari, n.k.
Kufanya kampeni dhidi ya unyanyapapaa ni mojawapo ya mbinu za mpango huo wa kuzuwia maambukizi ya UKIMWI na kupunguza athari zake.
Shughuli hii kama ni wajibu wa kila Muislamu kwa kiwango cha nafasi au wadhifa wake aliyonao, umetokana na misingi ya Kiislamu ifuatayo:
I. Kauli ya Allah (S.W.) katika Qur’an, anasema:
Na uogopeni (jikingeni na) mtihani au balaa ambalo halitowapata kwa maangamizo wale tu waliodhulumu (kwa kulisababisha) peke yao.
{وَاتَّـقُواْ فِـتْنَــةً لاَّ تُصِيـبَنَّ الَّذِيـنَ ظَلَمُواْ مِنــكُمْ خَاصَّةً } الأنفال25
Tujue kuwa wale waumini wema haitoshi kuwa wao wamejizuwia nafsi zao na matendo ya kuambukiza magonjwa. Matokeo ya kunyamazia na kubakia wachamungu ndani ya nafasi zetu tu ni kuangamia sote kwa pamoja wakiwemo watoto wadogo na wengine wasio na makosa.
II. Mwenendo wa Mitume (A.S.):
Mitume wote, na ndio ambao tumeagizwa kufuata mifumo ya maisha yao,walikuja kulingania mataifa yao katika maisha ya ndoa za halali na uaminifu kama ni sehemu ya ibada na njia muwafaka ya kujitosheleza haja za kijinsia baina ya mwanamke na mwanamme. Njia nyengine zote ni kinyume na maumbile na huwa ni uadui wa kuvamia nje ya mipaka iliyoruhusiwa:
Basi atakayetaka kupita kinyume na hilo (ndoa) hao ndio wanaofanya uadui. 23:7
{فَمَنِ ابْتَغَى وَرَاءَ ذَلِكَ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْعَادُونَ } المؤمنون7
Kondomu sio ufumbuzi wala ukewenza siyo tatizo kwenye UKIMWI.
III. Kauli ya Allah (S.W), anasema:
Haitobeba nafsi mzigo (wa hatia) ya mwengine. 35:18
{وَلا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَى } فاطر18
Si halali wala ubinaadamu kwa waathirika wa UKIMWI kubaguliwa kijamii au katika kupatiwa huduma.
Watoto yatima waliofiliwa na wazazi wao kwa UKIMWI, au huyo aliyepatwa na maradhi akiwa muasharati, hao ni mfano wa wenye haki kamili ya kusaidiwa sawa na misiba mingine inayowafika hata wachamungu.
IV. Hadithi na Kanuni ya Kifiqhi:
Haifai kujidhuru wala kumdhuru mwengine
لا َ ضــَرَرَ و َلا َضـــِرَارَ
Ni kosa kwa mtu yeyote aliyewajibika kuifuata sheria iwapo atafanya tendo la kumletea madhara yeye binafsi au kumdhuru mwengine.
Kwa msingi huu, inatosha kufahamu kuwa miongoni mwa njia kuu za kuambukiza UKIMWI kama uasharati, ulevi, na kutumia madawa ya kulevya, yote yameharamishwa na sheria ya Kiislamu na zaidi ya hukmu hiyo yakawa ni njia ya kuleta madhara ya maradhi.
Kwa hivyo basi hata kama jambo hukmu yake kiasli ni halali hubadilika kuwa haramu kama linamletea mtu madhara.
Na mwenye maradhi pia amelazimika kujizuwia, au azuwiliwe kwa njia zote za hikma, asimwambukize mwengine kwa makusudi.
Kwa mfano wa hadhari za kuchukuwa kwa mmojawapo wa watu wa karibu aliyepata maradhi ni kama mume na mke, mama anayenyonyesha, wawili wanaotarajia kufunga ndoa, anayetoa damu kumchangia mgonjwa, n.k. yeyote kati hayo mmojawapo akipata maradhi ajizuwie au azuwiliwe asimmwambukize mwengine.
V. MSINGI WA SHERIA:
Mtuhumiwa hatiwi hatiani mpaka lithibiti kosa lake
الْمُتَّهَمُ بَرِيءٌ حَتَّى تَثْبُتَ إِدَانَـــتُهُ
Mgonjwa asibaguliwe kwa Unyanyapapaa wa UKIMWI eti kwa dhana tu ya kuwa ameupata kwa uhasharati. Kutamka kauli hiyo ni kosa linalompasa msemaji achapwe bakora thamanini ikiwa atashindwa kuleta mashahidi wanne wenye akili timamu na waadilifu kuwa wameshuhudia waziwazi kitendo cha mtuhumiwa kufanya zinaa bila ya kuwepo shubha. Au kwa njia nyengine akiri mwenyewe mtuhumiwa ili kuthibitisha tuhma hiyo.
Hata baada ya kuthibiti maasi hayo, muhusika atastahiki adhabu muwafaka kama ilivyotajwa katika sheria lakini hatonyimwa haki zake nyengine za kutobaguliwa na kuhudumiwa ipasavyo.
VI. MSINGI WA SHERIA:
Dharura huzingatiwa kwa mujibu wa uzito wake.
الضَرُوْرَاتُ تـُـــقَدَّرُ بـــِقَدَرِهــَا
Haina maana ya kuondoa unyanyapapaa ni kupita akitangaziwa kila mwenye UKIMWI mabarazani na kwenye vyombo vya habari, bali huko ndiko kumnyanyapaa kwenyewe.
Cha msingi ni kumdhibiti baada ya kuthibitika kikweli kusibiwa kwake na ugonjwa asiweze kuwaambukiza wengine, badala ya kunyamaziwa kimya mgonjwa akaingiliana na wengine kwa njia zinazojulikana za kuambukiza bila ya yeye mgonjwa kubaguliwa au kubugudhiwa.
Kinachotakiwa ni njia za busara, upole na utaratibu za kuzinusuru pande zote mbili – mgonjwa asiache asinyanyaswe na mzima asiambukizwe.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.