“Uhai wa wanyamapori ni jambo
linalotuhusu sisi sote katika Afrika, viumbe hai wa porini wakiwa katika
mapori waishimo sio muhimu tu kwa ajili ya kuajabiwa na kuvutia lakini
pia ni sehemu ya maliasili yetu na mustakabali wa maisha yetu baadaye”
Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere alisema hayo wakati akitoa tamko la Arusha kuhusu Uhifadhi wa
wanyamapori kipindi Tanganyika inapata Uhuru mwaka 1961.
Alisema kukubali dhamana ya
wanyamapori, watanzania wanawajibu wa kufanya kila liwezekanalo
kuhakikisha wajukuu na watoto wa kitanzania wanaweza kufurahia urithi
mkubwa wa thamani hiyo adhimu ya wanyamapori.
Juhudi za uhifadhi na kulinda
rasilimali, malikale na kuendeleza shughuli za ufugaji nyuki pamoja na
kukuza Sekta ya Utalii ikiwa ni jukumu la Wizara ya Maliasili na Utalii
zilikuwepo hata kabla ya ukoloni ambapo jamii nchini zilitenga mapori
kwa ajili ya kuabudia na kutambika.
Kuingia kwa wakoloni nchini
kuliambatana na kutunga Sheria za uhifadhi wa rasilimali za maliasili na
malikale ambapo ni Sheria ya kuhifadhi Majengo ya kihistoria ya mwaka
1937, Sheria ya Makumbusho ya mwaka 1941, Sheria ya Usimamizi wa Misitu
ya mwaka 1957, Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro ya mwaka 1959, Sheria ya
Hifadhi za Taifa ya mwaka 1959 na Sheria ya kuhifadhi wanyama ya mwaka
1959.
Chini ya uongozi wa Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Nyerere, kuanzia mwaka 1961 Wizara ya Maliasili na Utalii
imekuwa na Sera na Sheria tofauti kulingana na mabadiliko yaliyokuwa
yakitokea duniani katika nyanja za kiuchumi, kiteknolojia, kiasiasa na
kijamii.
Juhudi za Baba wa Taifa katika
kuhakikisha Sekta ya utalii mwaka 1961 ilikuwa na idara moja ambapo
ilianza kuwa na Sera ya uhifadhi wa maliasili, malikale na kuendeleza
utalii nchini.
Mabadiliko na matukio makuu ya
Wizara ya Maliasili na Utalii mara baada ya uhuru mwaka 1961 yalipelekea
jitihada za makusudi za kuwezesha wazawa kielimu ili kuweza kuchukua
nafasi za utendaji na uongozi ambazo awali zilishikiliwa na wageni.
Aidha, mwaka 1967 kufuatia
kupitishwa Azimio la Arusha mali binafsi zilitaifisha na kuundwa kwa
mashirika na taasisi za umma ambapo Wizara iliunda mashirika ya umma
ikiwemo Shirika la Wanyamapori, Shirika la Viwanda vya mbao, Shirika la
Utalii Tanzania, Shirika la kuhudumia wasafiri na Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro kwa lengo la kukuza na kuimarisha sekta ya utalii nchini.
Katika mabadiliko hayo ndani ya
Wizara, juhudi za Mwalimu Nyerere zilipelekea Serikali kujitoa katika
kuendesha shughuli za kibiashara na kujikita katika kusimamia Sera na
uwezeshaji.
Kadhalika katika suala la ulinzi
wa rasilimali za maliasili za taifa, Serikali ilirithi mfumo wa kikoloni
na kuendelea kuwa mlinzi na mwendelezaji mkuu wa rasilimali za
maliasili, malikale na utalii.
Miaka 1991 Serikali ilifanyika
mabadiliko ya kisera yaliyokuwa na mwelekeo wa uhifadhi na uendelezaji
wa rasilimali kwa kuhimiza ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi na
uendelezaji wa rasilimali za maliasili, malikale na utalii.
Ushirikishwaji huu wa jamii katika
shughuli za maliasili na utalii ulipelekea Wizara kuanzisha vitengo
mbalimbali ikiwemo kitengo cha Ugani katika idara na taasisi zake ikiwa
na lengo la kuimarisha na kukuza sekta ya utalii nchini.
Katika suala la ajira katika
wizara wakati nchi inapata uhuru, jinsia haikupewa kipaumbele katika
sekta za maliasili hususani wanyamapori, misitu, malikale na nyuki. Kazi
hizo zilikuwa maalumu kwa wanaume ambapo juhudi za Mwalimu Nyerere
zilipekea mabadiliko ya kimtazamo uliosababisha kupatikana kwa ajira
ikihusisha jinsia zote mbili, ambapo kwa mara ya kwanza sekta ya utalii
iliajiri mwanamke mwaka 1970.
Katika sekta ya nyuki wanawake
wawili waliokuwa na astashahada ya ufugaji wa nyuki waliajiriwa mwaka
1975, sekta ya misitu iliajiri mwanamke wa kwanza mwenye shahada mwaka
1976, katika sekta ya wanyamapori mwanamke aliajiriwa mwaka 1967 na
katika sekta ya mambo ya kale mwanamke aliajiriwa mwaka 1978 kwa ngazi
ya cheti na 1981 kwa ngazi ya shahada.
Katika kuongeza tija na kufanya
maamuzi kwa kutumia taarifa zilizofanyiwa utafiti, wizara ilianzisha
vyuo vya ulinzi, uhifadhi na uendelezaji wa maliasili, malikale na
utalii ambapo chuo cha viwanda vya misitu kilianzishwa mwaka 1975, chuo
cha ufugaji nyuki Tabora mwaka 1978 pamoja na vyuo vya elimu ya
wafanyakazi Rongai na Sao Hill vilivyoanzishwa mwaka 1979 kwa lengo la
kutoa elimu ya awali ya uoteshaji miche na kuhudumia misitu.
Katika kukuza na kuimarisha sekta
ya utalii nchini Mwalimu Nyerere aliweza kutekeleza majukumu ya wizara
kulingana na mabadiliko ambayo yamekuwa yakitokea nchini na duniani
katika nyanja ya kiuchumi, kisiasa kiteknolojia na kijamii.
Juhudi hizo zilipelekea wizara
kuongeza vituo vya malikale na kutangaza maeneo tofauti kama urithi wa
Taifa, mashamba ya miti yaliongezeka, misitu ya asili pamoja na hifadhi
za Taifa kuongezeka.
Mbali na juhudi hizo za Mwalimu
zilisaidia kukuza na kuimarisha sekta ya utalii mara baada ya uhuru
zilipelekea ongezeko la mikusanyo ya malikale ambapo wakati wa uhuru
wizara ilihifadhi jumla ya mikusanyo ya 10,151 ya fani za Akiolojia,
mila, historia, bayolojia na nyaraka mbalimbali.
Aidha, baada ya uhuru kutokana na
tafiti zilizofanywa na watafiti wazawa na wageni kutoka nje ya nchi hadi
juni, 2011 wizara imefanikiwa kuhifadhi nchini urithi wa malikale
unaohamasisha wenye jumla ya mikusanyo 337,361.
Katika suala la ongezeko la idadi
ya watalii wanaongia nchini ndani ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere
idadi ya watalii iliongezeka kutoka watalii 9,847 mwaka 1960 hadi
watalii 103,361 mwaka 1986.
Tukiwa tunaadhimisha miaka 18 bila
Mwalimu Nyerere kumekuwa na mafaniko makubwa katika sekta ya utalii
ambapo mpaka kufikia mwaka 2016 idadi ya watalii waliotembelea nchini
Tanzania ilifika 1,284,279
Ukuaji huo wa sekta ya utalii
unatokana na misingi imara iliyowekwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere
kuendelezwa na kusimamiwa kwa manufaa ya sasa na baadaye.
GSENGO BLOG
INATOA AKSANTE KWA
: Beatrice Lyimo,
MAELEZO-DOdoma
KWA HABARI HII.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.