ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, June 12, 2013

SERIKALI KUENDELEA KUDHIBITI MAJOKOFU NA VIYOYOZI VILIVYOTUMIKA NA VINAVYOTUMIA KEMIKALI ZISIZO RAFIKI WA TABAKA LA OZONI

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Eng. Evarist Ndikilo akifungua warsha ya mafunzo ya usimamizi wa sheria ya mazingira (kanuni za kudhibiti kemikali zinazoharibu tabaka la ozoni) na udhibiti wa biashara haramu ya kemikali na bidhaa zinazoharibu tabaka la Ozoni, uzunguzi uliofanyika leo Lakairo Hotel Mwanza.
Uelewa mdogo wa baadhi ya wafanyabiashara kuhusu madhara kwa tabaka la Ozoni yanayosababishwa na kemikali na bidhaa wanazoagiza, uhaba wa mitambo ya kunasa na kurejeleza vipoozi katika soko, ongezeko la mafundi vishoka wasiokuwa nataaluma na vifaa sahihi vya kuhudumia majokofu na viyoyozi ni baadhi ya changamoto zinazoikabili serikali katika juhudi zake za kukabiliana na uharibifu wa tabaka la Ozoni.

Hata hivyo Mkuu wa mkoa wa Mwanza Injinia Evarist Ndikilo amesema kuwa serikali itaendelea kukabiliana na changamoto hizo kwa kuongeza udhibiti mipakani kwa kila kitengo kusimamia nafasi yake ikiwa ni pamoja na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni za Kudhibiti Kemikali Zinazoharibu Tabaka la Ozoni za mwaka 2007.
Wadau mbalimbali kutoka sekta za usimamizi wa uingizaji bidhaa nchini wakiwa makini kusikiliza kinachojiri warshani.
Wakati juhudi za kuhamasisha wadau kuhusu faida ya kutumia kemikali mbadala na tekinolojia mpya katika vifaa na mitambo mbalimbali zinaendelea, matumizi ya kemikali haribifu bado yapo. Asilimia hamsini (50) ya matumizi ya kemikali hizi ni katika biashara na viwanda na asilimia nyingine hamsini (50) ni katikavifaa vya majumbani.
Malalamiko mengi ya wananchi yamekuwa ni juu ya vifaa vyao vingi kutofanya kazi ipaswavyo kama awali mara baada ya kufanyiwa matengenezo au kujazwa gesi baada ya kuishiwa gesi kwa vifaa kama viyoyozi, majokofu na mitungi ya kupikia.

Imegundulika kuwa katika biashara ya uingizaji gesi nchini kutoka nchi kama China au pengine Uarabuni na kwingineko, wafanyabiashara kwa kutaka faida wasiamini uharibifu unaoweza kutokea kupitia uingizaji wa gesi zenye kemikali zisizo rafiki na mazingira hususani tabaka la Ozoni au pengine kwa makusudi wakijua madhara, ukipima bidhaa zao utaona kiwango kikubwa cha asilimia ya gesi zisizofaa kimechanganywa na gesi iliyoainishwa juu ya mtungi.

Uchunguzi mwingine umebaini kuwa baadhi ya mitungi mingine imepimwa na kukutwa ikiwa na asilimia 25 tu ya gesi iliyopaswa kuwepo na kiasi cha gesi asilimia 75 inayobaki ni hewa ya kawaida ambayo haikupaswa kuwemo na kuwa sababu ya vifaa vingi kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.  
Mafunzo haya ya siku mbili  yamenuia kutumia muda wa kutosha kuwaelimisha wadau kuhusu tabaka la Ozoni na umuhimu wake.

Tabaka la Ozoni ni kama blanketi au mwavuli kati ya jua na uso wa dunia ambalo hutukinga tusidhurike dhidi ya mionzi ya kikiukaurujuani (Ultraviolet-B radiation) kutoka kwenye jua ambayo husababisha madhara kwa afya ya binadamu na mazingira. 

Tafiti zinaonyesha kuwa Tabaka la Ozoni lipo takribani kilometa 10 hadi 50 kutoka uso wa dunia katika anga za juu. Tafiti zaidi zaidi za kisayansi mwishoni mwa karne ya ishirini zimethibitisha kumomonyoka kwa tabaka hilo kutokana na kulundikana angani kwa kemikali aina ya Chloroflourocarbons (CFCs), halons, methyl chorofom, methyl bromide, carbon tertrachoride na nyinginezo.

Kemikali hizi hutumika katika majokofu, viyoyozi, vifaa vya  kuzimia moto, ushafishaji chuma, utengenezaji magodoro, madawa, manukato, kilimo na uhifadhi wa mazao katika maghala.

Moja kati ya hatua zilizofanyika kupitia mkataba wa Montreal, serikali iliandaa programu ya taifa ya kuondosha matumizi ya kemikali zisizofaa kwa kusambaza habari kuhusu kemikali na tekinolojia mbadala, kuweka taratibu za kudhibiti uingizaji na matumizi ya kemikali zilizopigwa marufuku pamoja na kubadilisha tekinolojia katika viwanda vinavyotumia kemikali haribifu.
Muelimishaji kutoka kutoka TRA akitoa ufafanuzi jinsi wadau wa sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa wanavyo simamia udhibiti wa bidhaa haribifu kwa mazingira licha ya kujulikana zaidi kwao kuhusika na ukusanyaji ushuru.

Jeshi la polisi, wasimamizi wa idara mbalimbali mipakani, maafisa forodha, waandishi wa habari ni sehemu ya wadu walioshiriki warsha hii inayoandaliwa na ofisi ya waziri mkuu.

Picha ya pamoja ya washiriki wa Warsha ya mafunzo ya usimamizi wa sheria ya mazingira na Mkuu wa mkoa wa Mwanza Injinia Evarist Ndikilo.

"Nawatakia warsha njema" says Ndikilo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.