ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, November 2, 2017

VIFARANGA VILIVYO TEKETEZWA KWA MOTO VYAZUA MJADALA.

Watetezi wa haki za wanyama wametoa maoni wakilaani kuteketezwa vifaranga vya kuku 6,400 vilivyoingizwa nchini kinyume cha sheria.

Vifaranga hivyo mali ya Mary Matia (23), vyenye thamani ya Sh12.5 milioni vilikamatwa mpakani Namanga vikitokea nchini Kenya.

Kuteketezwa kwa vifaranga hivyo juzi kumeibua mjadala ikielezwa kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria.

Kazi ya kuviteketeza eneo la Namanga wilayani Longido ilifanyika ikishuhudiwa na maofisa wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Wizara ya Mifugo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Akizungumza wakati wa kuviteketeza vifaranga hivyo, ofisa mfawidhi wa kituo cha udhibiti wa magonjwa ya mifugo Kanda ya Kaskazini, Obedi Nyasebwa alisema kazi hiyo imefanyika kwa kuzingatia Sheria ya Magonjwa ya Wanyama namba 17 ya mwaka 2003.

Pia, alisema Serikali mwaka 2007 ilitoa tangazo kupiga marufuku kuingizwa nchini vifaranga vya kuku na mayai.

Hata hivyo, watu mbalimbali wamehoji ulazima wa kuviteketeza vifaranga hivyo badala ya kuvirudisha vilikotoka kama alivyoomba mmiliki wake Matia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ustawi wa Wanyama (Taweso), Dk Thomas Kahema akizungumza na Mwananchi jana alisema anatambua dhamira ya Serikali ya kuzuia magonjwa ya kuambukizwa kutoka nchi jirani, lakini kulikuwa na njia mbadala ya kufanikisha suala hilo.

Dk Kahema alisema mamlaka za Serikali zilitakiwa kuvirudisha vifaranga hivyo vilikotoka ili visieneze magonjwa kama inavyohofiwa. Alisema kuviteketeza ni ukatili ambao hauungi mkono na kwamba, wanalaani kitendo hicho ambacho kinatoa taswira mbaya kwa Taifa linaloonekana halijali haki za wanyama.

“Zipo njia nyingi ambazo wangeweza kutumia mbali na kuchoma, mbona wakikamata ng’ombe hawawachomi moto?” alihoji Dk Kahema.

Alisema Sheria ya Ustawi wa Wanyama ya mwaka 2008 inasisitiza kutambuliwa kwa haki za wanyama, kwa hiyo kuteketezwa vifaranga hivyo kunaonyesha jinsi utekelezaji wa sheria unavyoibua utata.

Dk Kahema alisema vifaranga hivyo vingepimwa kubaini kama vina maambukizo na ingebainika havina vingetaifishwa au kugawiwa wajasiriamali, magereza au vituo vya watoto yatima.

Alisema hana uhakika kama sheria iliyotumika kuteketeza vifaranga hivyo inaeleza wazi kwamba viteketezwe.

Mkurugenzi mtendaji huyo amesema mamlaka hazikuweka wazi kama vifaranga hivyo vilikuwa na maambukizo.

Alisema vifaranga havina hatia bali aliyevileta ndiye anayetakiwa kuchukuliwa hatua.

Baadhi ya wananchi kupitia mitandao ya kijamii wameonyesha kutoridhishwa na hatua iliyochukuliwa na mamlaka za Serikali wakieleza ni ukatili dhidi ya wanyama.

Abbas King aliandika kwenye ukurasa wa Facebook wa Mwananchi kuwa, “Hivyo vifaranga vina roho au vinaendeshwa kwa umeme? Kwa nini msivigawe kwa watoto yatima wakafuge vikue wafanye kitoweo, kama vina madhara virejeshwe kwao, walioleta wapigwe faini.”

Tumaini Kyama aliandika katika ukurasa huo kuwa, “Swali langu ni kuwa kama alikuwa kachukua mkopo wa biashara huyo mmiliki wa hivyo vifaranga mkopo ataurudisha na nani sitaki kujua hayo mengine nimewaza kwa sauti tu. Tunapambana na umasikini au tunafurahia umasikini wa baadhi ya watu.”

“Ukiukwaji wa sheria ya wanyama na pia wamerudisha maendeleo nyuma. Vilevile hawajavipima vifaranga na kutufahamisha vina magonjwa gani na hata hivyo si wangevirudisha vilikotoka ili aliyevinunua arejeshewe fedha yake na kama ni faini apigwe ili iwe funzo kwa wafanyabiashara,” aliandika Lightdod Shayo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.