Machi 8, Bodi ya Sukari (SBT) ilitangaza kushusha bei ya sukari kutoka Sh2,000 hadi Sh1,800 ikisema kiwango kilichopo cha bidhaa hiyo ni cha kuridhisha licha ya baadhi ya viwanda kusimamisha uzalishaji kutokana na msimu wa uvunaji mali ghafi kuisha.
Siku hiyo, mkurugenzi mkuu wa SBT, Henry Simwanza alionya wafanyabiashara dhidi ya upandishaji wa bei ya sukari na kuhodhi ili iwe adimu, akisema kitendo hicho ni kuhujumu uchumi wa nchi na atakayegundulika atachukuliwa hatua.
Alitoa agizo hilo siku chache baada ya Rais John Magufuli kupiga marufuku uagizaji sukari kutoka nje hadi kwa kibali cha Ikulu.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti la |Mwananchi katika sehemu kubwa ya nchi umebaini kuwa hivi sasa wananchi wanatoboa zaidi mifuko yao kununua bidhaa hiyo kwa tofauti ya Sh600 kulinganisha na bei hiyo elekezi.
Upandaji huo wa bei ya sukari umeelezwa na wafanyabiashara na wazalishaji kuwa ni matokeo ya uhaba wa bidhaa hiyo muhimu kutokana na viwanda vingi kusimamisha uzalishaji wakati huu.
Jijini Dar es Salaam ambako sukari hupatikana kwa wingi, bei imeendelea kuwa ya wastani wa Sh2,200 kwa kilo moja sawa na mkoani Kilimanjaro ambako kuna kiwanda maarufu cha sukari cha TPC.
Ni sehemu chache mjini Moshi ambako sukari inauzwa Sh1, 800.
Mmiliki wa duka la rejareja lililopo Manispaa ya Moshi, Mary Mosha alisema wamepandisha bei kutokana na wauzaji wa jumla kuongeza bei kutoka Sh75,000 kwa mfuko wa kilo 50 hadi kufikia Sh99,000.
Hali hiyo ipo pia mikoa ya Kanda ya Ziwa ambako bei ya sukari imeongezeka na kuwa kati ya Sh2, 000 na Sh2, 500.
Taarifa kutoka mikoa ya Geita, Mara, Tabora, Shinyanga, Kagera zinaonyesha kuwa sukari imeadimika, hali inayotoa mwanya kwa wauzaji wa rejareja na jumla kupandisha bei.
Mmoja wa wauzaji wa sukari mjini Geita, Pendo James alisema amelazimika kuuza kilo moja ya sukari kwa Sh2,500 kutokana na wauzaji wa jumla kuwapandishia bei kutoka Sh98, 000 kwa mfuko wa kilo 50 hadi Sh100, 500.
“Wakati tulipokuwa tukiuza kilo ya sukari kwa Sh1,800, tulikuwa tukinunua mfuko wa kilo 50 kwa kati ya Sh80, 000 hadi Sh85, 000,” alisema Pendo.
Katika wilaya za Karagwe na Bukoba mkoani Kagera ambako kuna kiwanda cha Kagera Sugar, kilo moja ya sukari inauzwa kati ya Sh2,200 hadi Sh2,400.
“Mfumuko huu unatokana na aidha baadhi ya viwanda vya sukari au wauzaji wa jumla kuficha bidhaa hiyo,” alisema mmoja wa wafanyabiashara wakubwa wilayani Karagwe kwa sharti la kutotajwa jina
Hali hiyo ipo pia katika wilaya za Chato mkoani Geita, Kahama na Shinyanga mkoani Shinyanga na Tarime mkoani Mara ambako bidhaa hiyo inauzwa kwa bei ya juu kuliko bei elekezi.
Katika baadhi ya maeneo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, bei ya jumla kwa mfuko wa kilo 50 imefikia Sh115, 000, huku bei ya kilo moja inaweza kufikia Sh3, 000 iwapo Serikali haitaingilia kati na kudhibiti mfumuko huo.
Mjini Shinyanga, mfuko wa kilo 25 uliokuwa ukiuzwa kwa Sh47, 000 hivi sasa unauzwa Sh53,000 kwa bei ya jumla.
Habari kutoka Bukoba zilizothibitishwa na baadhi ya wafanyakazi wa wakala mkuu wa sukari wa kiwanda cha Kagera waliozungumza kwa sharti la kusitiriwa majina yao, maghala ya wakala huyo hayana akiba ya bidhaa hiyo, hali inayosababisha bei kupanda.
Wafanyabiashara wadogo na wananchi wanaotumia sukari katika shughuli zao nao wanasikitishwa na suala hilo huku wakituhumu Serikali kushindwa kusimamia na kuhakikisha bei elekezi inafuatwa.
Wafanyabiashara nao walilalamika bei ya jumla ya sukari na kudai kuwa ndio husababisha wao kushindwa kuuza kwa bei elekezi.
Awali wizara ilisema inashirikiana na maofisa biashara wa kila halmashauri na tayari mawakala wake wanazunguka kubaini wanaokiuka agizo la bei elekezi na kuchukua hatua stahiki, lakini hadi sasa haijawekwa bayana wafanyabiashara walioadhibiwa.
Ofisa habari wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Edward Nkomola alipoulizwa kama kuna watu wameshakamatwa kwa kosa la kuficha au kuuza sukari kwa bei juu, alisema kuwa suala hilo lipo chini ya idara ya utafiti na masoko na bado linafanyiwa kazi.
Alipoulizwa kuhusu hali iliyopo sasa sokoni, mkurugenzi mkuu wa SBT, Henry Simwanza alitaka kutumiwa maswali ili ayajibu mara baada ya kurudi ofisini kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi kwenye kikao.
Mwenyekiti wa umoja wa wazalishaji wa sukari Tanzania, Ammy Mpungwe alisema huenda ongezeko la bei linatokana na upungufu uliopo sasa kwa kuwa viwanda vingi kwa sasa vimesimamisha uzalishaji baada ya msimu wa uvunaji kuisha.
“Kwa mfano kiwanda chetu cha Kilombero, tulipeleka maombi Ofisi ya Waziri Mkuu kama taratibu zinavyotaka kuomba kuagiza sukari kutoka nje tangu wiki nane zilizopita, lakini mpaka sasa hatujapata majibu,” alisema na kuomba Serikali itoe idhini.
Mpungwe, ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kiwanda cha Kilombero, alisema huenda bei ya sukari itapanda zaidi kutokana na uhaba utakaojitokeza kwa kuwa hata wakiagiza sasa bado upungufu utakuwepo.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.