Ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere katika Bohari ya Dawa (MSD) umebaini taasisi hiyo ya umma kutumia jumla ya Sh215.99 milioni kulipa watumishi watatu posho ya kujikimu walipokwenda China.
Mbali na hilo, CAG alibaini taasisi hiyo kushindwa kwa asilimia 66 kutimiza mahitaji ya bidhaa za dawa na vifaatiba kwa wateja, ununuzi usiozingatia sheria pamoja na kuwepo kwa mikataba iliyosainiwa bila kupekuliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika ripoti yake kwenye ukaguzi na ufanisi uliofanywa MSD, Kichere alibaini barua yenye Kumb. Na. CEA.169/178/03/18 ya Oktoba 13, 2020 ya uteuzi wa maofisa watatu kwenda China kwa ajili ya kutafuta watengenezaji ili kusambaza mashine 71 za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo ‘hemodialysis’ na kutoa ushauri kwa Serikali juu ya ununuzi wa mashine hizo.
Alisema mchakato huo haukuhusisha kitengo cha usimamizi wa ununuzi na bodi ya zabuni, bali mchakato mzima ulifanywa na watu watatu wakiwa China kwa Sh2.79 bilioni. “Nilibaini kuwa, ili kuwezesha ununuzi wa mashine hizo, MSD ilitumia Sh215.99 milioni kulipa watumishi watatu posho ya kujikimu kwa siku 61 pamoja na gharama za usafiri kwenda China kwa madhumuni ya mazungumzo na kutafuta viwanda. Nina shaka na mchakato mzima wa ununuzi na matumizi ya fedha za umma,” alisema Kichere.
Kiwanda cha Idofi
Katika ripoti ya mapitio ya uwekezaji katika mashirika ya umma, Kichere alieleza kuchelewa kuanza uzalishaji kwa viwanda vinavyomilikiwa na mashirika ya umma huku akigusia uanzishwaji wa kiwanda cha kutengeneza glovu bila kufanya upembuzi yakinifu wa kibiashara.
Alisema baada ya kupitia muhtasari wa mkutano wa 157 wa Bodi ya Wadhamini ya MSD, iliibua wasiwasi wa upembuzi yakinifu na kuiagiza taasisi hiyo kueleza kwa uwazi uwezo wao katika masuala ya fedha, utaalamu, teknolojia na kuonyesha chanzo cha asilimia 10 ya malighafi kwa ajili ya uzalishaji kutoka vyanzo vya ndani.
CAG alibaini ripoti ya upembuzi yakinifu ya MSD ya Septemba 2020 juu ya kuanzishwa kwa eneo hilo la viwanda haikujumuisha mchanganuo wa biashara pamoja na mpango wa kina ulioandaliwa ili kupata hoja za kuanzisha mradi na kutathmini faida, gharama na vihatarishi vya biashara.
Ununuzi
Katika ripoti hiyo, Kichere alisema taasisi hiyo ilifanya ununuzi wa bidhaa bila mikataba wenye thamani ya Sh9.90 bilioni na Dola 1.42 milioni za Marekani kinyume na kanuni ya 233(1) (2) na kanuni ya 75 ya kanuni za ununuzi wa umma za mwaka 2013.
Katika hatua nyingine, CAG amebaini mikataba yenye thamani Sh17.92 bilioni iliyotolewa na kusainiwa bila kupekuliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kinyume na kanuni ya 59 (1)(2) na kanuni ya 2 ya kanuni za ununuzi wa umma za mwaka 2013.
Hata hivyo, CAG Kichere alisema katika ukaguzi wa ununuzi alibaini utekelezaji wa mikataba sita ya ununuzi ya Sh43.98 bilioni katika bohari hiyo ambayo haikuwa katika bajeti wala kujumuishwa katika mpango wa ununuzi wa mwaka.
Akichangia mada bungeni Aprili 13, mbunge wa Handeni, Reuben Kwagilwa alisema kuna haja kwa sheria ya ununuzi wa dawa irekebishwe kwa kuwa inatoa mianya mitatu mibaya inayosababisha dawa kununuliwa kwa bei isiyo halisi.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema, “sheria inaweza kuwa na changamoto, tatizo lililo MSD siyo sheria ya ununuzi ya umma, lakini mipango mibaya ya utekelezaji, MSD hiyohiyo kwa sheria hii hii tulianza kufanya vizuri, sheria tunayo lakini tunaweza kubadilisha sheria, lakini kama hatuna mipango mizuri hatutafanikiwa, Mheshimiwa Rais alishatoa maelekezo tunalifanyia kazi.”
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.