ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, January 23, 2017

WALIMU MBARONI KWA KUMDANGANYA MWAJIRI.

NA ANNASTAZIA MAGINGA, 
GSENGO BLOG, Mwanza
WALIMU watatu wa shule tofauti za sekondari wamekamatwa na jeshi la polisi leo Jijini Mwanza baada ya kubainika kufundisha kwenye shule binafsi  wakati wameajiliwa serikalini.

Tukio hilo limetokea Shule ya Sekondari Museba iliyoko Buhongwa jijini hapa ambapo walimu wawili waliaga kwa wakurugenzi (waajiri) wao kuwa wanakwenda masomoni  na mmoja kuwa anakwenda kutibiwa wakati kumbe wanafundisha katika shule hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, amewataja walimu hao mbele ya waandishi wa habari jijini hapa leo kuwa ni Rwiza Ntale (27) wa Shule ya Sekondari Kigongo iliyopo wilayani Chato, mkoa wa Geita, ambaye aliaga kwa mwajiri wake mwaka 2015 akidai anatakiwa kwenda Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza kutibiwa macho na vidonda vya tumbo.

Wengine ni Mwalimu Richard Mgendi (30) wa Shule ya Sekondari Misasi wilayani Misungwi, Mwanza ambaye aliaga kwa mwajiri wake mwaka 2012 kuwa anakwenda kujiendeleza kwa kusoma shahada ya pili (masters) ya Lugha.

“Mwingine tuliyemkamata ni Mwalimu Gilbert Makwaya (33) wa Shule ya Sekondari Rwanim, anayedaiwa kuaga kwa mwajiri wake mwaka 2015 kuwa anakwenda kujiendeleza kielimu kwa shahada ya pili ya Hesabu katika Chuo Kikuu cha Mwenge kilichopo Moshi, mkoani Kilimanjaro,” amesema Msangi.

Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, amesema walimu hao walikuwa wakipokea mishahara mara mbili kinyume na utaratibu wakati ni waajiriwa wa serikali.

Hata hivyo, kufuatia tukio hilo Mkurugenzi huyo amesema  watachambua  maombi ya walimu walioko masomoni na kuandika barua kwenye vyuo walivyoomba kwenda kusoma na kwamba ikibainika watatakiwa kurudisha fedha za mishahara walizolipwa.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.