Afisa Tarafa wa Itiso Bw. Remidius Emmanuel akimhoji mtendaji wa kijiji cha Zajilwa Bw. Hamisi Mdimu juu ya uhalali wa muhtasari aliouandaa na kuelekezakwa mkurugenzi wa HalmashauriyaChamwino bila kuhusisha Serikali ya kijiji.
Baadhi ya wananchi wa kijiji Zajilwa wakiendelea kufuatilia kinachoendelea katika mkutano huo
Afisa Tarafa akizungumza na wajumbe wa Serikali a kijiji cha Zajilwa mara tu baada ya kumalizika kwa mkutano na wananchi panija na wananchi wa kijiji hicho
Na Mwandishi Wetu
Akizungumza katika Mkutano na wananchi wa kijiji Zajilwa wakati akisikiliza Kero za Wananchi juzi, Bw .Remidius Emmanuel ambaye ni Afisa Tarafa ya Itiso amewataka viongozi wa kijiji hicho kutumia muda mwingi kusikiliza Kero za Wananchi na kuzitatua, "Nimekwisha toa Maagizo katika Tarafa yangu na pengine nirudie kwa mara nyingine katika kijiji hiki, Viongozi wote tunatakiwa kupambana na viashiria vya migogoro kabla migogoro yenyewe kutokea, Kila mgogoro una chanzo chake . " Jamani leo unapoona mawingu lazima ujue hiyo ni dalili ya mvua" Alisema Bw. Remidius
Kiongozi huyo amesema hayo huku kukiwa na vuguvugu la Wananchi waliowengi kuonyesha hisia kali za kuipinga Serikali ya kijiji hicho kwa kumtaka Mwenyekiti wa kijiji hicho kuachia ngazi kutokana na wananchi hao kutoridhishwa na utendaji wa Serikali ya Kijiji.
Akizungumza mbele ya Afisa Tarafa kwa niaba ya Wananchi wenzake Bw. Chacha Marwa amesema Serikali ya kijiji hicho ni jipu linalotakiwa kutumbuliwa kwa kuwa imeshindwa kusoma mapato na Matumizi, "hatupati taarifa za miradi inayotekelezwa na Kijiji hiki. Tarehe 21/03/2016 Serikali ilihitisha Mkutano mkuu wa kijiji ambao ulivurugika kutokana na udanganyifu uliojitokeza. Mfano Tulisomewa Mapato ni Tsh 1,645,000 na Matumizi ni Tsh 4,510,000 taarifa inayoonyesha Matumizi kuzidi mapato ya kijiji je fedha nyingine walitoa wapi ? hakuna Umakini katika kuandaa taarifa hizo" Alisema Bw.Chacha huku akishangiliwa na Wananchi wengi na kuongeza kuwa "Tunashukuru sana Afisa Tarafa kwa kuja kusikiliza Kero zetu ,hapa kijijini zipo Kero nyingi sana na Tatizo ni Serikali ya kijiji"
Hata hivyo kwa nyakati tofauti Bw. Remidius Aliwasimamisha Mwenyekiti wa Kijiji hicho na Mtendaji wake kujibu hoja hizo mbele ya Mkutano huo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Zajilwa Bw. Athumani Salum Duda Alikiri kuvunjika kwa Mkutano wa Serikali ya Kijiji wa Tarehe 21/03/2016 nakusema Mkutano huo ulivunjika kutokana na Wananchi kutokubaliana na Taarifa za Mapato na Matumizi, hata hivyo Mwenyekiti huyo akionekana kuwa na kigugumizi alipotakiwa kueleza ni lini sasa Mkutano huo utafanyika.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji hicho Bw. Hamisi Mdimu, Alisema Mkutano huo ulifanyika na Tayari amekwisha andika Muhitasari hatua iliyopingana na Maelezo Mwenyekiti wa Kijiji Bw. Athumani baada ya kusema kuwa hatambui Muhtasari huo na kwamba hakuna saini yake katika Muhtasari huo , hata hivyo Wajumbe wa Serikali ya kijiji hicho kwa upande wao walionekana kushangazwa na Muhitasari huo ambao tayari uliandikwa na kuelekezwa kwa Mkurugenzi kuonyesha kwamba Mkutano mkuu ulifanyika salama kwa kujadili Mapato na Matumizi pasipo kuonyesha kama Mkutano huo ulivunjika.
Akihitimisha hoja hizo Afisa Tarafa Bw.Remidius Emmanuel ,Amesema viongozi wa kijiji hicho ndio chanzo kikubwa cha Migogoro na ameangiza ndani ya kipindi cha wiki moja Serikali hiyo wahitishe haraka Mkutano Mkuu wa kijiji kwa kuwasomea taarifa za Mapato na Matumizi na kujadili masuala mbalimbali ya Maendeleo katika kijiji hicho. " Naagiza Mkutano huo ufanyike mara moja ndani ya kipindi kisichozidi wiki moja, Wananchi wasomewe Taarifa za mapato na Matumizi , maana ni haki yao yao ya msingi, na nitaongea na mkurugenzi ili atume haraka sana wakaguzi wa ndani kwa ajili ya kukagua na kujiridhisha na Matumizi ya fedha katika kijiji hicho na kama itathibitika kuna Matumizi Mabaya ya fedha wahusika wote watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Alisema Bw.Remidius na kuwataka Viongozi hao kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa, Hata hivyo amemtaka Mtendaji wa kijiji hicho kujieleza kwa maandishi kwa nini alifanya udanganyifu wa kuandika Taarifa za Uongo kwa Mkurugenzi kama Muhtasari wa Mkutano uliovunjika pasipo kumshirikisha Mwenyekiti wa kijiji na Wajumbe wote wa Serikali ya kijiji hicho huku akifahamu taratibu zote za kuandika Mihtasari ya vijiji.
Bw.Remidius amewataka Wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya kijiji na kusema Maendeleo yanaletwa kwa ushirikiano kati ya Wananchi na Serikali. Hata hivyo Wananchi walionekana kufurahishwa na ujio wa kiongozi huyo na kukubaliana na maamuzi yaliyofikiwa.
Katika hatua nyingine Bw. Remidius ametoa muda wa Wiki moja kwa Wafanyabiashara wote ambao hawana leseni za Biashara wawe wamelipia leseni hizo kinyume na hapo hatua kali na msako mkali utafanyika mara moja. " Wapo wafanya biashara wengi hapa kijijini ambao hawana Leseni za Biashara , nawapa muda wa wiki moja wawe wamelipia leseni zao na hili ni agizo kwa Tarafa nzima ya Itiso, kinyume na hapo wajiandae kushughulikiwa kwa mujibu Sheria" Alisema Bw. Remidius
Wakati huo huo Afisa Tarafa huyo Ameivunja kamati ya Afya ya Zahanati ya kijiji hicho ( Zajilwa) kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kukwamisha ufanisi wa huduma ya Afya kijijini hapo ikiwa ni pamoja na kukwamisha juhudi za kijiji hicho katika kutekeleza Maagizo ya mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Farida Salum Mgomi ambaye pamoja na mambo mengine amekuwa mstari wa mbele kuhimiza utoaji bora wa huduma za Afya na kuhamasisha Wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya jamii (CHF) aidha Bw. Remidius amegiza kuundwa kwa Kamati mpya ili iendane na kasi ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.