Picha ni sehemu ya bweni
iliyoathirika na moto na kuteketeza mali za Wanafunzi.
(Picha na Maktaba)
Na
Nasibu Mgosso.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ndicho chombo chenye
jukumu la kuzuia na kukabiliana na majanga mbalimbali
kama mafuriko , Tetemeko la Ardhi, ajali
za vyombo vya usafiri na usafirishaji,
kuporomoka kwa majengo, migodi, pamoja na matukio ya moto.
Mara kwa mara, majanga ya
moto yamekuwa yakitokea katika jamii yetu kwa sababu moto ni sehemu ya maisha
yetu ya kila siku. Utafiti
umethibitisha kwamba, vyanzo vingi vya moto ni sisi wenyewe
(binadamu) kutokana na uzembe, hujuma au kutokukuwa na elimu ya Tahadhali na Kinga Dhidi ya Moto.
Aidha, matukio ya moto
yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika
shule za bweni hapa nchini hususani
shule za sekondari, na kusababisha uharibifu wa miundo mbinu kama vile Mali, majengo
na wakati mwingine majeraha au vifo kwa wanafunzi wetu na kuleta simanzi na
sintofahamu kwa Wananchi na Taifa kwa ujumla .
Uchunguzi wa moto (Fire Investigation) umebaini
sababu za matukio hayo ni
matumizi mabaya ya umeme yanayofanywa na
wanafunzi kwa
kujiunganishia nyaya za umeme wenyewe bila kuwa na weledi iliwapate sehemu za kuchaji simu na heater za
kuchemshia maji kwa kificho kwa sababu Wanafunzi hawaruhusiwi kuwa na simu wala heater pindi
wanapokuwa shuleni.
Lakini pia sababu nyingine
ni matumizi ya mishumaa, unapokatika umeme wakati wa kujisomea. Shule
nyingi zinajaribu kuzuia mabweni
kutumika kama sehemu za kujisomea,
lakini bado wapo baadhi ya Wanafunzi
wanaamua kujisomea
ndani ya mabweni bila kuchukua
tahadhari yoyote na wanapopitiwa na usingizi, uacha mishumaa inaendelea kuwaka na hatimaye
kusababisha ajali ya moto.
Utakumbuka miaka kadhaa
iliyopita matukio kama haya ya kuungua kwa shule yalileta majonzi makubwa kwa kuangamiza maisha ya Wanafunzi wengi. Kuungua kwa shule ya Shauritanga Mkoani
Kilimanjaro mwaka 1994 ambapo zaidi ya wanafunzi 40 walipoteza Maisha pamoja na
Mali.
Mwaka 2009 shule ya
sekondari Idodi Mkoani Iringa iliteketea kwa moto na zaidi ya wanafunzi 20
walipoteza Maisha pamoja na Mali. Hiyo ni mifano tu lakini matukio ya kuungua
kwa shule ni mengi sana hapa nchini.
Ili kupunguza matukio hayo,
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeanzisha Fire klabu katika shule mbalimbali za Msingi na Sekondari ili kupata wajumbe watakaoliwakilisha katika shule na makazi yao.
Kwa kutumia fire klabu, Jeshi
la Zimamoto na Uokoaji limejenga ukaribu
mkubwa na Wanafunzi wa shule hizo, hatua
inayosaidia kuwapa elimu stahiki ya kukabiliana na majanga ya moto.
Changamoto iliyopo ni mapokeo ya baadhi ya Viongozi wa shule kutokuwa
tayari kuruhusu shule zao kuanzisha
klabu za Zimamoto zinazosimamiwa na
kuratibiwa na Jeshi hilo ambapo mpaka sasa ni shule 100 ndizo zilizofungua
klabu hizo kwa nchi nzima.
Kama nilivyo eleza hapo
mwanzo, lengo la klabu hizo ni kuwapa fursa wanafunzi kuwa familia moja na
wataalamu wa Zimamoto. Ukaribu huo hutumika kwa wazimamoto kuwapa mbinu
mbalimbali za kuzuia na kukabiliana na vyanzo vya moto.
Lakini kwa upande wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ni kupanua wigo wa kuwa na idadi kubwa
ya watu, wanaoifahamu vyema elimu
hiyo na kuwa mabalozi
wazuri watakao liunganisha Jeshi na jamii kwa kufikisha elimu hiyo, Mijini na Vijijini na hatimaye kuweza kupunguza na
kutokomeza kabisa majanga.
Wito wangu kwa wamiliki wa
shule, walipokee jambo hili kama ukombozi kwao kupunguza majanga ya moto katika shule zao.
Tukishirikiana tutapunguza majanga
ya moto, na Taifa litakuwa salama.
Mungu ibariki Afrika Mungu
ibariki Tanzania.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.