Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua mwongozo wa uanzishaji na uendeshaji wa nyumba za kuwahudumia walioathirika na dawa za kulevya unaoweka utaratibu utakaohakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa na mfumo na ubora unaolingana kote nchini.
Mwongozo huo umezinduliwa jijini Mwanza wakati wa uzinduzi wa kliniki ya tiba saidizi kwa waathirika wa dawa za kulevya katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure.
Ukarabati wa kliniki hiyo umefanywa kwa kwa pamoja na Mamlaka ya Uratibu wa dawa za kulevya, Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali ya ICap na Agpah kwa gharama ya zaidi ya Sh132 milioni.
“Kila anayeanzisha nyumba za kuhudumia waathirika sasa lazima afuate na kuzingatia utaratibu maalum kwa mujibu wa mwongozo huu,” amesema Waziri Mkuu
Kamishina wa Mamlaka ya kudhibiti dawa za kulevya nchini, Rogers Sianga alisema mkoa wa Mwanza ni kati ya mikoa nchini yenye matukio mengi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya, hivyo ofisi yake imepanga kuweka timu maalum mkoani humo kukabiliana na matukio hayo.
Mkoa wa Mwanza, kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk Leonard Subi, una waathirika wa dawa za kulevya kati ya 10, 000 hadi 15, 000.
Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Dk Subi alisema mwaka 2017 hospitali ya Sekou-Toure ilihudumia waathirika 113, asilimia 70 wakiwa ni watu wa umri katika ya miaka 15 hadi 45.
Ili kutambulika na kusaidiwa wakati wowote, Kamishna Sianga amesema waathirika wanaopata tiba watapewa kadi maalum watakazoonyesha kwenye vituo vya huduma na kwa vyombo vya dola.
Mwonekano wa Kliniki hiyo kwa nje. |
Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto, Dk Faustine Ndungulile alisema Serikali imeweka mikakati wa kuagiza dawa aina ya methadone inayotumika kuwatibu waathirika wa dawa za kulevya ili ipatikane kwa bei nafuu kuwezesha wengi kumudu gharama.
Baraka Mpango mkazi wa eneo la Kirumba jijini Mwanza, mmoja waathirika wa dawa za kulevya aliishukuru Serikali kwa kusaidia matibabu kwa waathirika na kuomba fedha zaidi zitengwe kwa ajili ya kununulia dawa na kuwawezesha kiuchumi wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya.
“Waathirika wengi nikiwemo mimi mwenyewe niliyetumia dawa hizo kwa karibia miaka 20 hutengwa na familia na jamii; ni vema pakawepo mpango maalum wa kuwawezesha kiuchumi ili warejee katika maisha ya kawaida,” amesema Mpango.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.