ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, September 21, 2016

SERIKALI SASA KULIVALIA NJUGA SUALA LA UFUNGAJI LUMBESA.

Na:  NEEMA  JOSEPH, MWANZA
Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa hivi karibuni alitoa tamko la kukataza ujazo wa kipimo cha dagaa kwa mtindo wa  lumbesa.

 Serikali imeona ombwe la usimamizi wa sharia ya Vipimo kwa kuamua kutoa tamko la kulinda maslahi ya wauzaji wa dagaa katika masoko ya mkoa wa Mwanza.

“Kitendo cha wanunuzi wa mazao kushindilia magunia na kushonelea kichuguu maarufu kama lumbesa huko ni kuwaibia wakulima na kukiuka sharia”, alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Hata hivyo, Daudi Makunguna na Swaumu Mtanki, wakazi wa Jumakisiwani, kambi ya Yataka Moyo wameeleza kwamba  wananchi hawana uelewa wowote wa vipimo na kwamba agizo  la serikali bado halijatekelezwa Kisiwani.

Walisema wamekuwa wakishuhudia wafanyabiashara wanaonunua dagaa  kwa kipimo cha ndoo  zilizojaa mlima kiasi cha dagaa wengine  wanamwagika. “ serikali ifike na kuangalia  namna ya kuwanusuru wavuvi na wauza Dagaa wa Jumakisiwani.”

Paulo Nghomele Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Jumakisiwani ameeleza kwamba, lumbesa ipo katika  uuzaji wa dagaa  Juma kisiwani kwasababu wananchi hawajawahi kupata elimu juu ya kutokomeza  wa lumbesa. “ Wakala wa Vipimo wangekuwa wanatufikia wanakijiji wangekuwa na uelewa wa vipimo na wangenufaika na biashara ya dagaa

Naye Afisa Uvuvi Mkaoa wa Mwanza Titus Kilo amesema kwamba mapato yanayotokana na uvuvi yamekuwa yakijumuishwa kwa pamoja bila kuainisha ni kiasi gani kinapatikana kutokana na Dagaa.

Kwa mujibu wa takwimu za uvuvi za mwaka 2010 mpaka 2015 wavuvi walipata jumla ya shilingi 261,137,759,859/= kutokana na mauzo ya tani 211,479,385 za samaki.

Hata hivyo, Wakala wa vipimo Mkoa wa Mwanza,  Hemed Kipengele amebainisha kwamba,wametekeleza agizo la serikali kwa kutoa elimu katika kanda ya ziwa mnamo wa Juni mwaka huu.

Aliongeza kwamba katika kipindi hicho kumekuwa na uangalizi wa matumizi sahihi ya mizani  kwa kuwaeleimisha wananchi namna ya kutambua mizani zinazopima sahihi na mizani zilizochezewa ili wasiibiwe.

“Sasa hivi tunaangalia matumizi sahihi ya mizani kama zimehakikiwa na wakala wa Vipimo na kwamba kama mizani hazijahakikiwa mwaka huu utaona imewekwa alama ya ngao ya Taifa na tarakimu ya 2015”, alisema Wakala wa Vipimo.  

Kwa mujibu wa taarifa ya utendaji kazi ya Wakala wa Vipimo Mkoa wa Mwanza,   watu  waliokamatwa kwa kosa la kufunga  lumbesa  ni 130 na kwamba katika operesheni iliyofanyika kati ya Aprili hadi Agosti mwaka huu, jumla  shilingi 16,770,000/= zilifililishwa kutoka kwenye masoko mbalimbali kwa mazao ya dagaa, viazi vitamu,vitunguu na mkaa.

Afisa wa Wakala wa Vipimo Mkoani, Hemedi Kipengele alisema kwamba  pamoja  na  kwamba  agizo la serikali la kukataza lumbesa lilitolewa kwa vyombo vyote vya serikali lakini linaonekana kuachiwa Wakala wa Vipimo pekee.

Alisema kwamba alichoona ni barua kutoka Tamisema kwenda  kwa Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya wakiagizwa kudhibiti lumbesa kwa kutunga kanuni ndogondogo za kutoza faini kwa watakaokamtwa na lumbesa lakini utekelezaji  bado upo kwa halmashauri.

 Aliwataka wananchi wafuate sheria  ya vipimo ili kuondokana  na usumbufu watakaoupata na kufuata sheria na kushiriki katika mchakato wa kutunga kanuni unaofanywa na vyombo vya kutunga sheria.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella amesema kwamba, agizo la serikali juu ya lumbesa kwa ofisi yake limetekelezwa  kwa kushirikiana  na  Wakala wa Vipimo.

Alisema kwa vile wakala wa vipimo hawapo kila maeneo lakini uongozi  na mfumo wa serikali upo mpaka kwenye ngazi ya kitongoji na mtaa na kwamba katika miezi minne iliyopita kulifanyika oparesheni mkoa wote wa Mwanza.

Hata hivyo, alisema kwamba wananchi hawezi kufanyabiashara kwa gharama ya kujimaliza wenyewe  na kutoa mfano wa uungwana wa mshumaa kwa kuangazia watu wengine wakati wenyewe  unatekeketea.

Alisema wafanyabiashara wananunua  dagaa Tanzania na kuwasafirisha Kongo lakini wakifika Kigoma wanawafungua na kuwafunga upya. “sasa kwa nini Tanzania tunaweka lumbesa?”

 Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba katika kijiji cha Jumakisiwani wanunuzi wa dagaa wamejipangia bei zao na kwamba muuzaji anapokataa bei zao wanagoma kununua dagaa zao na hivyo kulazimika kuuuza kwa bei za wanunuzi.

Hata hivyo, uchunguzi umegundua kwamba Serikali imefanikiwa kukomesha lumbesa kwa maeneo ya mjini tofauti na maeneo ya vijijini ambako lumbesa inaendele.

Serikali na hasa Wakala wa Vimipo waelekeze macho yao visiwani kwa sababu katika maeneo hayo  hakuna elimu ya ufungashaji kwa mujibu wa sheria ya vipimo.
Takwimu za Uzito/ Tani za uvuvi  wa Dagaa kwa kipindi cha miaka sita

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.