Tafiti kutoka taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) mkoa wa Mwanza zinaonyesha kuwa ugonjwa wa kichocho ni hatari unaoathiri wakazi wengi wa kanda ya ziwa kama ilivyo kwa maradhi ya malaria na ukimwi hivyo kuwaomba watu wote wakiwemo wanasiasa kuzungumzia ugonjwa huo ili jamii ipate uelewa jinsi ya kupambana nao.
Ni ndani ya mkutano wa siku moja wenye lengo la kupashana habari kuhusu maendeleo ya utafiti wa mradi wa kichocho cha tumbo, uliohusisha waalimu wa shule za msingi, wakuu wa vijiji vya wilaya mbalimbali, wafanya biashara na wadau wa sekta mbalimbali mkoani Mwanza.
Lengo kuu la mradi wa huo ulio katika mpango wa taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ni kufanya utafiti wenye lengo la kuboresha mikakati ya kupambana na ugonjwa wa kichocho cha tumbo ikiwa ni pamoja na kutoa matibabu.
Zaidi ya vijiji 150 vya mkoa wa Mwanza vilivyoko kando kando ya ziwa Victoria vimehusishwa na utafiti huo ambapo jumla ya watoto wa shule wapatao 27,926 na watu wazima 5,446 wamepimwa ugonjwa huo huku takwimu zikionyesha kuwa kwa wastani kwa kila watu 10 waliopimwa watu 6 walikutwa na maambukizi ya ugonjwa wa kichocho cha tumbo.
Njia ya kuaminika ya kudhibiti ugonjwa wa kichocho na kupunguza madhara yatokanayo na maambukizi ni kwa kutibu kwa kutumia dawa aina ya praziquantel.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.