ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, January 26, 2017

WACHIMBAJI 14 GEITA WAFUKIWA NA KIFUSI CHA UDONGO KWENYE MGODI WA DHAHABU.

NA. GSENGO BLOG.
GEITA: Takribani wachimbaji 14 akiwemo raia mmoja wa China anayejulikana kwa jina la Men Jung Ping, wamefukiwa na kifusi cha udongo katika mgodi wa dhahabu wa RZ ulioko katika kijiji cha Nyarugusu unaomilikiwa na Kampuni ya mwekezaji toka nchini China.

Juhudi za kuwaokoa watu hao zinaendelea.

Kifusi kimefunika mlango wa kuingilia shimo la mgodi huo na kusababisha wachimbaji hao kubaki chini ardhini ambako hakuna mawasiliaano.

Aidha vikosi vya uokoaji vinaendelea na jitihada zake kuwaokoa watu hao ambapo katika hatua ya awali, mpira toka pump ya hewa umeelekezwa shimoni humo nazo jitihada za kufukuwa udongo uliotitia zikiendelea kwa haraka kuwanasua wachimbaji hao  wakiwa hai.

Taarifa zimeifikia ofisi ya mkoa wa Geita leo majira ya saa 1 asubuhi ingawa ajali hiyo imetokea majira ya saa 7 usiku.

Mara baada ya taarifa, Kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Geita ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga, ilifika eneo la tukio kutoa msaada sanjari kuwahoji baadhi ya mashuhuda waliokuwa karibu wakati ajali likitokea.

Sababu za kuporomoka udongo  zimetajwa kuwa ni kutokana na mgodi kuchimbwa  zamani na Wajerumani hivyo kupelekea baadhi ya maeneo hayo kuwa na nyufa na vyuma kushindwa kushikilia udongo wa juu hali ambayo imepelekea kuzidiwa na mwisho wa siku kuporomoka.

Baadhi ya mashuhuda wanadai kuwa shimo hilo lenye urefu wa zaidi ya mita 38 lilititia majira hayo ya usiku mnene, kuta za juu kwenye mlango zilishuka polepole na wakati huo taarifa zikafikishwa kwa watu wa chini wakimbilie eneo la tahadhari, lakini baada ya muda mlango wa kuingilia ukafungwa na udongo na hivyo kupoteza mawasiliano na watu waliomo shimoni humo.

"Udongo ulizidiwa uzito ukaporomoka na kujifukia na baada ya hapo taarifa zilienea na wafanyakazi wa migodi mingine jirani wakakimbilia hapa kutoa msaada" alisema mmoja wa mashuhuda.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji Mkoa wa Geita. Elisha Mugisha, amesema kuwa eneo la chini ambalo limefukiwa na udongo ndio ambalo kwa sasa wanaendelea kulitanua ili sehemu hiyo iwe kubwa watu waweze kupita.

Wakiwa na nyenzo imara zaidi za uokoaji waokoazi kutoka mgodi wa Geita wako eneo la ajali huku wale waokoaji toka mgodi wa Bulyanhulu wilayani Kahama wakiwa njiani kufika eneo la tukio kuongeza nguvu. 

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.