ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, June 30, 2018

WAZIRI PROF. NDALICHAKO KUWA MGENI RASMI MKUTANO WA WANASAYANSI

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof Andrea Pembe akizungumza na Waandishi wa habarai juu ya Kongamano lake la sita la Kisayansi tarehe 2 na 3 Julai 2018. Kongamano hili litafanyika katika ukumbi wa LAPF Millenium Tower, jijini Dar es Salaam.

Ofisa Uhusiano wa Muhas akizungumza na Waandishi wa habari juu ya Mkutano huo utakaoanza jumatatu.

Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako anataraji kuwa mgeni rasmi katika kongamano la sita la kisayansi lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) litakalofanyka tarehe 2 na 3 Julai 2018 katika ukumbi wa LAPF Millenium Tower, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Waandishi wa habari mapema leo jijini Dar es Salaam Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Andrea Pembe amesema jukumu mojawapo la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi, Muhimbili (MUHAS) ni kutoa mafunzo ili kujenga rasilimali watu ya fazi za afya, kufanya tafiti na kushiriki kikamilifu utoaji huduma za afya kwa umma.

Amesema ili matokeo ya tafiti zinazofanywa yaweze kutumiwa na watekelezaji, wadau, wafanyakazi wa huduma za afya na wengine wanaofanya kazi katika maeneo husika ya kitaalamu, matokeo ya tafiti hizi hayana budi yasambazwe kwa ufanisi. 

“Hivyo basi, madhumuni ya kongamano hili la sita ni kushirikiana, kuelezana, kujifunza na kubadilishana ujuzi unaotokana na matokeo ya tafiti kati ya watafiti mbali mbali, watoa huduma wa afya, watekelezaji wa mikakati na sera mbalimbali na wadau wengine wote ndani na nje ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kushirikisha jamii kwa ujumla kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Katika Kongamano hili, Chuo kitaeleza mafanikio ya tafiti na athari zake kwa upande wa kijamii na maendeleo ya uchumi wa nchi. Katika Kongamano la sita la kisayansi, Chuo kitaonyesha matokeo ya tafiti za hivi karibuni ya kisayansi kutoka miradi mbali mbali ya tafiti zinazotoka ndani na nje ya nchi katika kipindi cha miaka ya nyuma. 

Kitu cha muhimu zaidi katika jamii ya wanataaluma wa MUHAS ni kuwa watapata fursa ya kushiriki matokeo yao na kubadilishana mawazo na wataalamu pamoja na wadau kutoka sehemu mbalimbali za nchi na duniani kote ikiwa lengo kuu ni kuboresha afya kupitia tafiti” amesema Prof. Pembe.

Amesema kuwa kauli mbiu ya Kongamano hili ni “Uimarishaji wa Uchumi wa Viwanda kupitia Tafiti za Afya kwenye nchi zenye kipato cha chini”. Kauli mbiu hii imechaguliwa mahususi kusisitiza umuhimu wa matumizi ya matokeo ya tafiti za Kisayansi za afya katika kuchangia uimarishaji wa uchumi wa viwanda hapa Tanzania na chi nyingine zenye uchumi wa kipato cha chini. Hii ni kutokana na ukweli kuwa ili kuimarisha uchumi wenye viwanda Taifa linatakiwa kuwa na majibu ya changamoto zinazokabili sekta ya Afya na kuboresha ukuaji wa uchumi.

Ametaja kuwa katika kongamano hili Makala za kisayansi 164 zitawasilishwa kwa njia ya maongezi (Oral Presentations). Makala zitakazo wakilishwa zimeangukia katika mada ndogo ndogo zifuatazo:

Tafiti za Afya ya Uzazi,Tafiti wa Magonjwa yasiyoambukiza, Tafiti wa Magonjwa yanayoambukiza,Utafiti wa Msingi katika Maswala ya Afya, Tafiti za Sera na Mifumo ya Afya, Tafiti za Teknolojia ya Habari mawasiliano pamoja na Afya, Tafiti za Afya ya Kinywa, Tafiti za Tiba Asili na Tiba Mbadala, Huduma za Dawa za Tiba,Tafiti za Maswala ya Jinsia na Afya.

Amesema jumla ya washiriki na wajumbe zaidi ya 400 kutoka nchini na nje ya nchi kutoka nchi za Rwanda, Uingreza, Japan, Uturuki, Italy na Marekani.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.