ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, July 4, 2018

MWANAMKE ASWEKWA KOROKORONI MWANZA KWA KUPORA MTOTO.


Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza linamshikilia mwanamke  mmoja  kwa tuhuma za kuiba mtoto wa kiume mwenye umri wa wiki tatu.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, amesema mwanamke huyo aliyetambulika kwa jina la Paulina Mashiku (27) na mkazi wa kijiji cha Mbugani wilayani Sengerema Mkoani humo.

Msangi ameeleza kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa ameolewa na mwanamume anayeishi maeneo ya Bukoba visiwani anakojishughulisha na uvuvi na katika kipindi chote cha ndoa yao hawajawahi kupata mtoto jambo lililosababisha mwanamke huyo kumdanganya mumewe kuwa amepata ujauzito.

"Ni kwamba mnamo tarehe 2.7.2018 majira ya saa sita mchana katika kijiji cha Mbugani tarafa ya Buchosa Wilaya ya Sengerema mwanamke mmoja alifanya kitendo hicho lakini siku mbili kabla ya tukio, alipita katika kijiji cha Buliyaheke na kumwona mwanamke akinyonyesha mtoto mchanga ndipo kesho yake alipochukua jukumu la kumpigia simu mumewe na kuwaaga majirani anakwenda hospitalini kujifungua.

Alisema kesho yake alifika katika nyumba alipo mtoto huyo majira ya 4:00 usiku na kumwona mama wa mtoto akiwa nje akipika wakati huo mtoto akiwa amelala chumbani na yeye akatumia mlango wa uwani kuingia ndani na kumwiba mtoto huyo na kurudi naye nyumba kwake huku akiwaeleza majirani kuwa amejifungua salama.

Tukio hilo liliwapa wasiwasi majirani kwa kuwa walipata taarifa katika kijiji cha Buliyaheke kuna mwanamke ameibiwa mtoto, hivyo wakatoa taarifa kituo cha polisi.

Na baadae Polisi walifanya ufatiliaji wa haraka hadi eneo la tukio kisha mtuhumiwa aliwekwa nguvuni na alipohojiwa alikiri ni kweli alimwiba mtoto huyo". Alieleza Kamanda Msangi

Msangi aliongezea kuwa hali ya mtoto ni nzuri na tayari amekabidhiwa kwa mama yake mzazi na polisi wako katika mahojiano na mtuhumiwa na uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

Kamanda Msangi ametoa wito kwa wakazi wa Mwanza kuwa waangalifu na watoto wao dhidi ya watu wenye nia ovu huku akiwataka waendelee kutoa ushirikiano na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu mapema ili wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.