Nicholas Biwott waziri wa zamani wa Kenya amefariki dunia leo mjini Nairobi wakati alipokuwa akiendelea kupata matibabu.
Nicholas Biwott aliyekuwa waziri
katika serikali ya Rais Mstaafu Daniel Arap Moi amefariki dunia katika
hospitali moja jijini Nairobi baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Biwott aliyejulikana wakati huo akiwa
waziri kama 'Total Man" ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 77, hayo
yameelezwa na msaidizi wake binafsi.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, mwendazake
Biwott alikuwa akiugua kwa muda mrefu na mara kwa mara alikuwa akilazwa
hospitali na hata kuna kipindi aliwahi kuzushiwa kifo. Kwa mujibu wa
duru za karibu na familia yake ni kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja
uliopita maradhi yalikuwa yakimzidia mara kwa mara Nicholas Biwott.
Biwott anakumbukwa na wengi katika siasa
za Kenya hasa katika kipindi cha utawala wa Rais mstaafu Daniel Arap
Moi, ambapo alitambulika kuwa waziri mwenye nguvu katika serikali hiyo.
Biwott alihudumu kama waziri wa masuala ya taifa akisimamia idara za
Sayansi na Teknolojia vile vile waziri wa masuala ya ardhi na kilimo cha
unyunyizaji.Mara ya mwisho kuhudumu waziri ilikuwa 2001-2001 ambapo alihudumu kama Waziri wa Biashara, Viwanda na Utalii wa Afrika Mashariki wakati wa utawala wa Rais Daniel Moi.
Nicholas Biwott (kushoto) enzi za uhai wake akiwa na Rais wa wakati huo wa Kenya Daniel Arap Moi
Aidha Biwott alihudumu kama mbunge wa Keiyo-Marakwet na Keiyo South kwa kipindi cha miaka 28 (1979 – 2007) kabla ya kuwa waziri kwenye utawala wa Rais Mstaafu Daniel Moi. Alianza utumishi wa umma kama mkuu wa wilaya (DO) Meru kati ya mwaka wa 1965 hadi 1966.
Mwanasiasa huyu mkongwe na maarufu
ambaye alizaliwa mwaka wa 1940, chama chake cha National Vision Party of
Kenya (NVP) kilikuwa kimetangaza kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta
katika uchaguzi ujao. Kifo cha Biwwot kinakuja siku chake tu baada ya
Kenya kuondokea na waziri wake wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery
aliyeaga dunia Jumamosi iliyopita.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.