Mahakama ya Wilaya ya Chato imemkuta na hatia Aliyekuwa Mtendaji wa kata
ya Bwanga Bw. Protase Polycarp Kyakatamba Ambaye ameshitakiwa kwa makosa mawili ya Kuomba Rushwa ya kiasi
cha Tshs. 300,000/= na kupokea Rushwa ya kiasi cha Tshs. 170,000/= kinyume na Kifungu
cha 15(1)(a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, hukumu hiyo
imesomwa na hakimu Mfawidhi wa mahakama ya Wilaya ya Chato Mheshimiwa JOVITH
KATO.
Akisoma
hukumu hiyo, mbele ya mwendesha mashitaka wa TAKUKURU Bw. AUGUSTINO MTAKI, Mheshimiwa
Kato alisema mahakama imemkuta na hatia Mshitakiwa katika makosa yote mawili
kama alivyoshitakiwa, na kwamba mahakama imejiridhisha pasipokuwa na shaka lolote
na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa Jamhuri kwamba mnamo tarehe
5/2/2016 Mshitakiwa aliomba kiasi cha Tshs. 300,000/= kutoka kwa Bw. Jackson
Madereke ili aweze kumwachia Ndugu yake Bw. Kulwa Charles aliyewekwa chini ya
ulinzi katika ofisi ya kata ya Bwanga kwa zaidi ya siku Nne, na kwamba mnamo
tarehe 6/2/2016 alimtuma Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyarututu Bw. Silvester
Nalompa akutane na Bw Jackson Madereke ili aweze kupokea fedha hizo kwa niaba
yake ambazo baada ya makubaliano kwa njia ya simu Mtendaji huyo alikubali
kupokea kiasi cha Tshs. 170,000/= badala ya Tshs. 300,000/= alizoomba awali.
Baada ya
kusomewa hukumu hiyo mshitakiwa alipewa nafasi ya kujitetea kabla ya kutolewa
adhabu ambapo mahakama imempa adhabu ya kulipa faini ya Tshs. 500,000/= kwa
kosa la kwanza au kifungo jela miaka mitatu (3) na faini ya Tshs. 500,000/= au
kifungo cha miaka mitatu (3) jela kwa kosa la pili, na makosa yote yatatumikiwa
kwa pamoja.
Mkuu wa
TAKUKURU Mkoa wa Geita Bw. Thobias Ndaro ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa
Geita kuendelea kuunga mkono TAKUKURU na serikali kwa ujumla katika mapambano dhidi
ya Rushwa kwa kutoa taarifa mbalimbali za vitendo vya Rushwa katika ofisi za
serikali za mitaa, mahakama na Halmashauri ili watuhumiwa waweze kuchukuliwa
hatua za kisheria na hivyo kushiriki kutokomeza vitendo vya Rushwa, Ubadhilifu
na Ufisadi katika jamii zetu na hivyo mwananchi atakuwa ameshiriki kukata
mnyororo wa Rushwa.
IMEANDALIWA NA MADUKA ONLINE
IMEANDALIWA NA MADUKA ONLINE
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.