ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, March 27, 2017

TAIFA STARS USO KWA USO NA BURUNDI KATIKA MCHEZO WA KIRAFIKI WA KIMATAIFA.

Timu ya Tanzania "Taifa Stars" inatarajiwa kushuka tena kesho Machi 28 katika mchezo wa pili wa kirafiki unaotarajiwa kuanza majira ya saa 10:00 jioni kumenyana na timu ya taifa ya Burundi.

Stars inaingia tena Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kucheza na Intamba Murugamba ya Burundi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, kwa mujibu wa kalenda ya wiki ya mechi za kimataifa ya FIFA.

Huu ni mchezo wa pili kwa Taifa Stars kucheza ndani ya wiki moja baada ya ule wa awali dhidi ya The Zebras ‘Pundamilia’ wa Botswana uliofanyika Uwanja huo wa Taifa, jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.

Katika mchezo huo wa Jumamosi, Taifa Stars ambayo kwa sasa inanolewa na Salum Mayanga akisaidiwa na Patrick Mwangata ambao ni makocha wapya wa kikosi hicho, walishinda kwa mabao 2-0.

Tayari Intamba Murugamba wametua nchini tangu jana Jumapili saa 4.30 asubuhi na kufikia Hoteli ya De Mag iliyoko, Kinondoni, Dar es Salaam na jioni yake walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini. Leo Jumatatu, inafanya mazoezi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Mayanga alifurahishwa na ushindi wa Jumamosi iliyopita dhidi ya The Zebras ya Botswana na hivyo amehimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa kesho.

Katika kuunga mkono wito wa Kocha Mayanga, TFF imebakiza viingilio vya mchezo huo kuwa sawa na vile vya Jumamosi iliyopita kwani katika mzunguko ambao unachukua mashabiki wengi kiingilio kitakuwa ni Sh 3,000.

Kwa upande wa VIP “A” Kiingilio kitakuwa ni Sh 15,000 wakati VIP “B” na VIP “C” kiingilio kitakuwa ni Sh 10,000. Viingilio hivyo vimelenga kuwaalika Watanzania wengine kwenda uwanjani.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.