Afisa Uhusiano Airtel Tanzania Jane Matinde akiongea wakati
wa kuchezesha droo ya fainali za taifa ya michuano ya vijana chini ya umri 17
ya Airtel Rising Stars. Kushoto ni Mkurungenzi wa maendeleo ya soka la wanawake
TFF Amina Karuma na katikati Mkurugenzi wa Ufundi TFF Salum Madadi.
Mkurungenzi wa maendeleo ya soka la wanawake Tanzania Amina
Karuma akiongea na waandishi wa habari wakati wa kuchezesha droo ya michuano ya
vijana chini ya umri 17 ya Airtel Rising Stars ngazi ya taifa. Katikati ni
Mkurungenzi wa Ufundi TFF na kulia Afisa Uhusiano Airtel Tanzania Jana Matinde.
Mkurungenzi wa Ufundi TFF Salum Madadi akiongea na waandishi
wa habari wakati wa kuchezesha droo ya michuano ya vijana chini ya umri 17 ya
Airtel Rising Stars ngazi ya Taifa. Kushoto ni Mkurungenzi wa maendeleo ya soka
la wanawake Tanzania Amina Karuma.
Lindi, Arusha kufungua dimba Airtel Rising Stars Taifa
Timu za soka za wasichana za Lindi na
Arusha zimepangwa kukutana katika mechi ya fungua dimba ya mashindano ya vijana
chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Statrs ngazi ya taifa katika uwanja
wa Kumbukumbu ya Karume, jijini Dar es Salaam, Jumanne, Septemba 6, 2016.
Mashindano hayo yanayojumuisha timu
za wasichana na wavulana yatafunguliwa rasmi siku hiyo ya Jumanne mchana na
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Paul Makonda ambaye atashuhudia mechi
ngumu ya wavulana kati ya Mwanza na Ilala.
Timu nyingine zinazoshiriki katika
michuano hiyo yenye lengo la kuibua vipaji ni Temeke, Kinondoni, Morogoro,
Arusha, Mbeya, Lindi na Zanzibar. Tayari timu zimeshawasili na kupiga kambi
katika shule ya Filbert Bayi iliyoko Kibaha.
Akizungumza wakati wa hafla ya
kupanga makundi iliyofanyika katika ofisi za shirikisho la mpira wa miguu nchini
(TFF), Mkurungenzi wa Ufundi Mwalimu Salum Madadi alisema kuwa maandalizi yote
ya mashindano hayo ngazi ya taifa yamekamilika.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na
mkurengenzi wa maendeleo ya soka la wanawake nchini Bi Amina Karuma ambaye
aliyaelezea mashindano ya Airtel Rising Stars kuwa ni chemchem ya wanasoka
chipukizi wasichana kwa wavulana.
“Mashindano ya Airtel Rising Stars
yametusaidia kupata wachezaji wenye vipaji vya ajabu ambao wanaunda timu za
Serengeti Boys na timu ya taifa ya wanawake yaani Twiga Stars”, alisema na
kuwashukuru Airtel Tanzania kwa kuendelea kudhamini mashindano hayo.
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Airtel
Tanzania Jane Matinde alisema kuwa kampuni yake inajivunia kuweza kutoa mchango
katika soka la Tanzania. “Airtel Rising Stars imekuwa chanzo cha kutumainiwa
kwa klabu na timu za Taifa kupata vijana chipukizi wenye vipaji. Tunaona fahari
kuweza kupata fursa ya kudhamini soka nchini Tanzania“alisema Matinde.
Michuano ya Airtel Rising Stars ngazi
ya Taifa inatarajia kufikia tamati siku ya Jumapili, Septemba 11, 2016 ambapo
bingwa kwa upande wa wasichana na wavulana watapatikana na kukanidhiwa vikombe
vya ubingwa.
Vilevile TFF itatangaza wachezaji
nyota kwa wasichana na wavulana wataochaguliwa kuunda timu ya Airtel Rising
Stars mwaka 2016.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.