ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, March 21, 2016

RAIS MAGUFULI AWA WA KWANZA KUTEKELEZA AGIZO LA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa mtu kwanza kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam la kuhakiki silaha, ambapo bunduki zake mbili aina ya Shortgun na Pistol zimehakikiwa nyumbani kwake Ikulu Jijini Dar es salaam.
Uhakiki huo umefanywa na maafisa wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam, Kamishna Simon Sirro.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na Jeshi la Polisi kwa kuendesha zoezi la uhakiki wa Silaha, na ametoa wito kwa watu wote wanaomiliki silaha nchi nzima kuhakikisha zinahakikiwa.Dkt. Magufuli pia amelitaka Jeshi la Polisi kuongeza juhudi za kukabiliana na watu wanaojihusisha na vitendo vya uharifu ili kutokomeza kabisa vitendo hivyo.
"Ni aibu kumuona askari polisi mwenye silaha ananyang'anywa silaha, ni aibu, na nasema hiyo ni aibu, mpaka jambazi akunyang'anye silaha na wewe una silaha?" Amehoji Rais Magufuli.Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Kamishna Simon Sirro, amemshukuru Rais Magufuli kwa kuunga mkono zoezi hilo na amesema Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ametaka pande zinazogombea kiti cha Umeya katika Jiji la Dar es salaam, kukamilisha mchakato wa kumpata Meya katika uchaguzi uliopangwa kufanyika kesho tarehe 22 Machi, 2016 badala ya kuendelea kurumbana.

Dkt. Magufuli amesema upande wowote uwe tayari kupokea matokeo ya uchaguzi huo, ili Meya apatikane na Jiji liweze kuendelea na mipango yake ya kuwahudumia wananchi bila vikwazo.

"Mahali tunapostahili kushinda kama tumeshinda tushinde kweli, lakini mahali tunaposhindwa napo tukubali kushindwa, na hiyo ndio demokrasia ya kweli" ameongeza Rais Magufuli

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam

21 Machi, 2016

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.