ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, June 14, 2012

HATIMAYE BAJETI 2012-2013 YAWASILISHWA BUNGENI



 Waziri wa fedha na uchumi Dk William Mgimwa leo amewasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ambayo nin sh Trilioni 15 tofauti na ile ya mwaka unaomalizika ya Sh Trilioni 13.5

Bajeti hiyo ina vipaumbele 7 ambavyo ni Miundombinu, kilimo, viwanda, rasilimali watu, huduma za jamii, utalii, pamoja na biashara ya ndani na nje na huduma za fedha.


Moja kati ya mapendekezo ya udiferenti yasema kuwa :- Ukitaka kuweka jina kwenye gari badala ya Plate number itakugharimu shilingi milioni 5 nayo itadumu kwa muda wa miaka mitatu.

Bajeti imelenga kuviwezesha viwanda vya ndani kuhimili soko la ushindani kwa bidhaa zake dhidi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.


Bajeti imetoa pendekezo la kulinda kazi za wasanii kwa kusajili kazi hizo ili kuwaingizia faida ya kipato kitakacho wawezesha kunufaika na kazi zao.

Hayo ndiyo ya udiferenti lakini pia ukweli ni kuwa inaonekana kama bajeti haina vitu vipya sanaaa, na imekaa kimjini mjini (isiyona manufaa kwa walio vijijini ) na baadhi ya vipengele vyake ni kama kuna marudio ya vile ambavyo vimewahi semwa huko nyuma kama ya kutuchapa bakora kwenye vinywaji na vileo .

Gharama za simu juu
Katika bajeti hiyo, Waziri Dk Mgimwa alisema muda wa maongezi (airtime) kwenye simu za mkononi umeongezeka kutoka asilimia 10 hadi 12. Alisema lengo la hatua hiyo ni kuoanisha ushuru wa bidhaa unaotozwa na huduma hiyo katika nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), kwa kipindi hiki ambacho nchi zipo katika Soko la Pamoja. Alisema hatua hizo za ongezeko la ushuru wa bidhaa kwa pamoja, zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh144,054.9 milioni.

Misamaha ya kodi ya magari

Waziri huyo alipendekeza kufanyika marekebisho kwenye sheria husika za kodi ya matangazo ya Serikali yanayotoa msamaha wa kodi kwenye magari kwa walengwa mbalimbali ili kuweka ukomo wa umri wa miaka minane kwa magari hayo badala ya miaka 10.

Alisema magari yenye umri wa zaidi ya miaka minane yatatozwa ushuru wa bidhaa wa asilimia 20. Lengo la hatua hiyo ni kupunguza wimbi la uingizaji magari chakavu na kulinda mazingira. Alitangaza pia marekebisho katika ushuru wa forodha, ikiwemo kufuta msamaha wa ushuru wa forodha katika vitu mbalimbali vikiwemo magari yenye ujazo wa CC 3000 huku pia ushuru wa forodha ukifutwa katika bidhaa nyingine nyingi muhimu.

Alisema katika kuhamasisha na kuchochea ukuaji wa sekta ya ufugaji wa nyuki, vifaa vinavyotumika katika ufugaji na kurina asali vimepewa msamaha wa ushuru wa forodha vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi na wafugaji wa nyuki.

Msamaha wa ushuru wa forodha kwenye migahawa ya majeshi ya ulinzi utaendelea kutolewa kwa kipindi cha mwaka mmoja. Alisema kumefanyika marekebisho katika Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya mwaka 2004 ili kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwa wazalishaji wa vyakula vinavyotengenezwa mahsusi kwa lishe ya watoto wenye utapiamlo na watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi.

Katika Bajeti hiyo, pia wametoa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye malighafi zinazotumika katika kutengeneza vifaa vya kufanyia uchunguzi wa magonjwa (medical diognastic kits) kwa kuwa vifaa hivyo hutozwa asilimia sifuri vinapoagizwa kutoka nje ya nchi.

Utatolewa msamaha kwenye mitambo (machinery) na vipuri vyake vinavyotumika kwenye uchimbaji wa madini lakini hautahusisha vipuri vya magari vitakavyoagizwa na makampuni yanayojihusisha na uchimbaji wa madini.

Katika bajeti hiyo, pia umetolewa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye vyuma vinavyowekwa kwenye kingo za barabara na lengo lake ni kutoa unafuu katika ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Alisema ushuru wa forodha umepunguzwa kwa ving’amuzi kutoka asilimia 25 hadi asilimia sifuri ili kuwezesha mabadiliko katika teknolojia ya analogia na kwenda katika teknologia ya digitali.

Ushuru wa ngano umeondolewa kuwa asilimia 0 badala ya asilimia 35 Serikali pia imesamehe VAT katika mashine za kutolea stakabadhi (electronic fiscal devices), ili kupunguza bei yake na kuwezesha wafanyabiashara wengi kuwa nazo, kuhamasisha matumizi yake na hivyo, kuongeza mapato ya Serikali.

Katika eneo hilo, Serikali imeondoa VAT kwa vifaa mbalimbali vya kuhifadhia, kusafirisha na kusambaza gesi asilia ili kuongeza matumizi ya nishati hiyo katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kwenye magari, majumbani na viwandani.

Kodi kwa wafanyabiashara
Wafanyabiashara ambao mapato yao hayazidi Sh3,000,000 hawatalipa kodi kuanzia Julai Mosi, mwaka huu. Dk Mgimwa alisema mpango huo umefanywa kulinda mapato ya Serikali. Kabla ya msamaha huo, wafanyabiashara hao ambao mapato yao hayazidi Sh3,000,000 walikuwa wanalipa Sh35,000. Marekebisho mengine ya kodi ya mapato ni kuwa wenye mapato kati ya Sh3 milioni –Sh7.5 milioni watalipa Sh100,000 badala ya Sh95,000.

Malengo ya Bajeti
Waziri Mgimwa alisema Bajeti hiyo imejielekeza katika Kukuza Pato la Taifa kwa asilimia 6.8 mwaka 2012 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.4 mwaka 2011. Malengo mengine ni kuimarisha miundombinu ya uchumi, ikijumuisha umeme, barabara, reli na bandari, kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na kuongezeka kwa mapato ya ndani yatakayofikia uwiano na Pato la Taifa wa asilimia 18 kwa mwaka 2012/13 kulinganisha na mwelekeo wa asilimia 16.9 mwaka 2011/12.

Dk Mgimwa alitaja malengo mengine kuwa ni pamoja na kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei ili urudi kwenye viwango vya tarakimu moja na kuwa na kiwango tengemavu cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha.

Malengo mengine ni kukuza mikopo kwa sekta binafsi kwa kiwango cha asilimia 20 ya Pato la Taifa ifikapo mwishoni mwa Juni 2013, sambamba na jitihada za kudhibiti mfumuko wa bei, kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wadogo na wa kati, kulinda na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta za huduma za jamii, kuimarisha utawala bora na uwajibikaji na kujenga uwezo wa nchi kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi na kifedha pamoja na kushiriki kwa ufanisi katika ushirikiano kikanda na kimataifa.

Matumizi ya Maendeleo
Kuhusu matumizi ya maendeleo, Waziri Mgimwa alisema itazingatia vipaumbele vya miundombinu ya umeme - mkazo ukiwa upatikanaji wake kwa kuongeza uzalishaji, usafirishaji na usambazaji na jumla Sh498.9 bilioni zimetengwa.

Serikali pia itatekeleza mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa mkopo kutoka Benki ya Exim ya China wenye thamani ya Dola za Marekani 1.2 milioni utakaosimamiwa na TPDC. Kuhusu usafirishaji na uchukuzi, alisema mkazo katika sekta hiyo utakuwa ni kuimarisha reli ya kati ikijumuisha ukarabati wa injini na mabehewa ya treni.

“Kwa upande wa barabara, miradi inayopewa kipaumbele ni pamoja na barabara zenye kufungua fursa za kiuchumi. Katika usafiri wa anga na majini, miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege na uendelezaji wa gati ya Ziwa Tanganyika. Jumla ya Sh 1,382.9 bilioni zimetengwa katika eneo hili,” alisema.

Kuhusu maji safi na salama, alisema lengo ni - kuongeza upatikanaji wake mijini na vijijini na kwamba kiasi cha Sh568.8 bilioni kimetengwa. Kwa upande wa kilimo, uvuvi na ufugaji alisema katika sekta hizo, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi itawekeza katika kilimo cha mpunga na miwa katika mabonde makuu ya Wami, Ruvu, Kilombero na Malagarasi pamoja na kuongeza tija na thamani, kubadilisha mfumo wa kilimo na kukuza kilimo cha misitu.

Kuhusu kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula pamoja na kuhakikisha uhakika wa chakula, Serikali itaimarisha utekelezaji wa dhana ya Kilimo Kwanza kwa kuhakikisha nguzo zake zote zinaendelea kuzingatiwa.

Alisema mikoa inatakiwa kuendelea kutenga ardhi na vijiji kutakiwa kupima na kurasimisha ardhi kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na wa nje na kwamba kiasi cha Sh192.2 bilioni kimetengwa katika eneo hilo.

Ikizungumzia maendeleo ya viwanda, alisema Serikali inakusudia kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini; viwanda vinavyoongeza thamani ya madini; viwanda vikubwa vya saruji na viwanda vya eletroniki na Tehama pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na kutenga maeneo maalumu ya uwekezaji mijini na vijijini na kukuza ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Tupe maoni yako

1 comments:

  1. I know this site presents quality based posts and additional stuff,
    is there any other website which presents such
    stuff in quality?
    Feel free to visit my weblog ; pizza games girls

    ReplyDelete

Note: Only a member of this blog may post a comment.