ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, October 6, 2018

NYUNDO YA MONGELLA YAANZA KUWASHUGHULIKIA WALIOHUSIKA NA WIZI WA MTIHANI DARASA LA 7 MWANZA



GSENGOtv

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella ameagiza vyombo vya dola mkoani hapa kuchukua hatua dhidi watu waliohusika kuvujisha mtihani wa darasa la saba na kusababisha serikali kuingia gharama ya kurudiwa kwa mtihani huo.

Akizungumza jijini hapa,  Mongella ameagiza jeshi la Polisi na taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa –TAKUKURU, mkoani Mwanza  kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wakuu wa shule za Alliance, New Alliance na Kisiwani za jijini hapa na wote wanaotuhumiwa kuhusika na udanganyifu wa mitihani ya kitaifa ya darasa la saba 2018.

Akionesha kukerwa na kitendo hicho alichokiita cha aibu na fedheha kwa mustakbar wa elimu ya Tanzania, Mongella amesema serikali itachukua hatua kali dhidi ya wale wote waliohusika kuvujisha mitihani hiyo bila ya kumuonea mtu yeyote.

Kufuatia tukio hilo serikali imetoa nafasi kwa wanafunzi wa shule hizo kurudia mitihani hiyo tarehe 8 na tarehe 9 mwezi huu katika vituo vitakavyotangazwa na serikali.

BREAKING NEWS: KITUO CHA BASI NA HOTELI YA STARCOM NANGURUKURU KINATEKETEA KWA MOTO.

Kituo kikubwa cha mabasi yanayotoka mikoa ya kusini (Lindi, Mtwara na Ruvuma) ambacho pia ni hoteli inayofahamika kwa jina la Starcom kilichopo Nangurukuru wilaya ya Kilwa, mkoa wa Lindi kimeteketea kwa moto.

Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika. 


Habari zaidi kuwajia wakati juhudi za kupata taarifa zaidi kuhusiana na tukio hilo zikiendelea.

WANANCHI WANAENDELEA KUNUFAIKA NA MFUMO WA USHIRIKI-DKT TIZEBA

Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba akitoa taarifa ya ukusanyaji, Ukoboaji na uuzaji wa kahawa Mkoani Kagera katika msimu wa mwaka 2018/2019 kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) kwenye mkutano wa wadau wa kahawa katika ukumbi wa ELCT Mjini Bukoba. (Picha Na Mathias Canal-WK)

Na Mathias Canal-WK, Bukoba-Kagera

Imebainika kuwa pamoja na changamoto zilizojitokeza katika msimu wa kahawa wa mwaka 2018/2019 lakini bado mfumo wa uuzaji wa kahawa kupitia ushirika umekuwa wa manufaa kwa mkulima kutokana na mkulima kupata uhakika wa kilo za kahawa alizozipeleka chamani tofauti na ilivyokuwa hapo awali. 

Manufaa hayo yamejili kutokana na kuingia mikataba ya kuuza moja kwa moja, ambapo matarajio ya serikali ni kuhakikisha kuwa mkulima analipwa malipo ya awali na kiasi kingine kubaki kwa ajili ya kuendelea kukusanya kahawa na kufanya maandalizi ya malipo ya pili. 

Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba amebainisha hayo Leo tarehe 6 Octoba 2018 wakati akitoa taarifa fupi ya ukusanyaji, Ukoboaji na uuzaji wa kahawa Mkoani Kagera katika msimu wa mwaka 2018/2019 hadi kuishia tarehe 2 Octoba 2018 kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) kwenye mkutano wa wadau wa kahawa.

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi ELCT Mjini Bukoba na kueleza kuwa ubora wa kahawa umeongezeka kwa kiasi kikubwa tofauti na misimu iliyopita. 

Waziri Tizeba alizitaja changamoto zinazovikabili vyama vya ushirika kwenye zao la kahawa kwa msimu wa mwaka 2018/2019 kuwa ni pamoja na Bei za mnadani, Kahawa kununuliwa kwa kiwango kidogo mnadani na wakati mwingine kutonunuliwa kabisa.

Kuwepo kwa taarifa za upotoshaji kwa wakulima toka kwa Walanguzi za kuzuia wakulima kukusanya kahawa yao kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi kuwa wao (Walanguzi)  watanunua na kuwapatia bei nzuri na Kuwepo kwa katizo la umeme mara kwa mara linalopelekea ukoboaji wa kahawa kutofanyika kwa wakati  (hususani Wilayani Ngara).

Aidha, aliutaja mkakati wa kukabiliana na changamoto hizo kuwa ni pamoja na kuuza kahawa kupitia mnada wa Moshi na mauzo ya moja kwa moja nje ya nchi “Direct Export” ambao umeonesha kuwa na bei nzuri ukilinganisha na ile inayotolewa mnadani Moshi, na Kuomba mkopo wa nyongeza toka TADB kwa ajili ya kuwalipa wakulima malipo yao ya Awali. 

Alisema Chama Cha Ushirika cha Karagwe KCU wanatarajiwa kupata mkopo wa Tshs. 2,000,000,000/= kwa wiki hii na kiasi cha Tshs. 2,000,000,000/= kinaendelea kushughulikiwa ili kiweze  kutolewa wiki ijayo ambapo wanatarajiwa kupata malipo ya mauzo ya kahawa yao kwa wiki ijayo kiasi cha Tshs Bilioni 2.1

Mikakati mingine ya kukabiliana na changamoto ya zao la kahawa ni pamoja na Vyama kuingia mikataba mbalimbali ya kuuza kahawa moja kwa moja nje. KDCU Ltd wana mikataba ya mauzo nje yenye thamani ya Tshs 20,819,815,820.66 ambapo malipo yake yanatarajiwa kulipwa kuanzia wiki hii. Kwa KCU Ltd wana mkataba wa Tshs Bilioni 1.3 na wanatarajia kuingia mikataba mingine na wanunuzi wengine kwa wiki ijayo. 

Dambamba na jitihada za kupatikana kwa umeme wa uhakika katika kiwanda kilichoko Wilayani Ngara zinaendelea kufanyika kwa kushirikiana na mamlaka husika.

Katika hatua nyingine alieleza kuwa mpaka sasa Kahawa iliyoko ghalani ni Kiasi cha Kilo 3,000,464 za kahawa maganda ambayo ilikuwa bado kukobolewa huku Kilo 8,191,867 za kahawa safi kilikuwa bado hakijauzwa na kilikuwepo kwenye maghala ya vyama.

Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa ameanza ziara ya kikazi Mkoani Kagera kuanzia Leo tarehe 6 mpaka tarehe 9 Octoba 2018 ambapo pamoja na mambo mengine lengo kuu la ziara hiyo ni kukagua Maendeleo ya zao la kahawa Mkoani humu.

MBUNGE COSATO CHUMI ABANWA NA WANANCHI TATIZO LA UMEME KATIKA KIJIJI CHA RUNGEMBA

Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini Cosato Chumi akitolea ufafanuzi juu ya swala la tatizo la umeme mara baada ya kupigia simu meneja wa tanesco wilaya ya Mufindi mkoani Iringa

NA FREDY MGUNDA,IRINGA.

Wananchi wa kata ya Rungemba mkoani Iringa wamemuweka kikaangoni mbunge wa jimbo la Mafinga mjini Cosato Chumi juu ya kukosekana kwa umeme katika baadhi ya vitongiji ya kata hiyo.

Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara wananchio hao wamesema kuwa wamekuwa walinzi wa umeme ambao umepita katika kijiji cha Rungemba.

“Sisi watu wa Makwawa na Njia Panda tumekuwa walinzi wa huu umeme ambao umepita kwenye hiki kijiji cha Rungemba na kata kwa ujumla maana hakuna hata laini ndogo ambayo inasemekana imepita lakini tumekuwa tunashangaa maana hakuna hata hiyo laini” walisema wananchi hao

Wananchi hao wameendelea kwa kusema kuwa umeme huo toka umefika hauna faida kwa wananchi wa kijiji hicho kwa kuwa wamepelekewa transifoma yenye nguvu ndogo kulingana na mahitaji ya wananchi.

“Tumewekewa transifoma haina uwezo kwa kuwa inashindwa hata kusukuma mashine za kusagia mahindi hivyo inatulazimu kusafiri zaidi ya kilometa saba kwa bodaboda kupata huduma ya kusaga mahindi” alisema wananchi

Aidha wananchi hao wamesema kuwa wapo tayari kulipia nguzo za umeme ili waweze kupata nishati hiyo kwa maendeleo ya wananchi na kijiji hicho.

Naye mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini Cosato Chumi akaamua kumpigia simu meneja wa tanesco wilaya ya Mufindi Omary Ally kupata ufumbuzi wa tatizo hilo mbele ya wananchi.
“Meneja nimebanwa hapa kwenye mkutano wa hadhara na wananchi juu ya tatizo la umeme hapa Rungemba hali ipoje” aliuliza swali kwa meneja?

Akijibu hoja hizo meneja wa Tanesco wilaya ya Mufindi Omary Ally kuwa kulikuwa kunatatizo la transifoma hiyo baada ya wiki moja watafunga na wananchi watapata nishati ya umeme ya uhakika kabisa

Hata hivyo Ally akawatoa hofu wananchi kwa kuwaahidi kuletea transiafoma ambayo itakidhi mahitaji ya wananchi wa kijiji hicho na kuondokana na kero hiyo ambayo inarudisha nyuma maendeleo.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya wananchi kata ya Rungemba kukaa kwa kipindi cha muda mrefu bila kuwa na huduma hiyo ya umeme.


"SIJAWAHI KUNUNUA WALA KUUZA GARI LOLOTE LA KANISA" ASKOFU MKUU WA KANISA LA EAGT

Askofu mkuu wa kanisa la Evangelistic assemblies of God Tanzania (EAGT) Dk.Brown Abell Mwakipesile.
 AMIRI KILAGALILA/GSENGOtV
NJOMBE

Askofu mkuu wa kanisa la Evangelistic assemblies of God Tanzania (EAGT) Dk.Brown Abell Mwakipesile ameendelea kuwa na msimamo wake wa kuto kuhusika hata kidogo na tuhuma za matumizi mabaya ya uongozi zilizokuwa zikielekezwa dhidi yake na baadhi ya viongozi wa kanisa hilo kwa kuuza majengo ya kanisa na kununua magari huku akiwataka waumini wa kanisa hilo kuelewa ukweli wa mambo hayo na kwamba kwa sasa kanisa hilo liko salama na limekwisha kwa kuwa yeye na viongozi wake hawakuhusika kwa lolote.

Askofu mwakipesile aliyazungumza hayo wakati alipokuwa akifundisha wachungaji zaidi ya mia mbili 200 katika semina ya  siku mbili  ya uamsho kwa kanisa iliyowakutanisha wachungaji na maaskofu wa majimbo sita ya Kanda ya Nyanda za juu Kusini Mashariki yaani Jimbo la Iringa, jimbo la Mufindi, Jimbo la Njombe, jimbo la Ludewa, jimbo la Songea pamoja na jimbo Mbinga na kufanyika katika kanisa la EAGT lililopo katika mtaa wa sido jimbo la Njombe mkoani Njombe.

Askofu Mwakipesile amesema yeye binafsi hakuwahi kuhusika na uuzaji wa jengo hata moja na kuwataka wachungaji kufika katika majengo yao yaliyopo mkoani Dar es salaam na kujionea majengo yao kwa kuwa yapo salama.

‘Kwa hiyo mimi nizungumze hapa kwenu nizungumze na ukweli wangu sijawahi kununua gari hata moja ya kanisa nawaambia tena sijawahi kununua gari hata moja la kanisa pamoja na kwamba nilikuwa katibu mkuu, wala Moses kulola marehemu hakuwahi kuniagiza kununua gari la kanisa hata siku moja, sijawahi kumsainia document yeyote msharika au mchungaji ya kununua gari akiwepo aseme’alisema askofu.

Aidha askofu huyo amesema hajawahi kuuza jengo hata moja na kuwatangazia wa chungaji kuanzia leo kutafuta majengo ya Eagt yalipo ili kujionea usalama wa mali zao.

Mnamo Desember 18 mwaka 2017 bodi ya wadhamini ya kanisa la Evangelistic Assembles of God Tanzania EAGT ilitangaza kumsimamisha kazi askofu mkuu wa kanisa hilo Dk.Brown mwakipesile na wenzake akiwemo katibu mkuu mchungaji Leonard mwizarubi na mhasibu mkuu mchungaji Praygod mgonja ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizokuwa zikiwakabili.

Aidha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam Desemba 21 ilifuta  amri ya kumzuia kwa muda Askofu Mkuu wa Kanisa hilo na wenzake, kujishughulisha na mambo ya kanisa hilo kwa nafasi zao, ikiwemo kufanya miamala kwenye akaunti  ya kanisa.

 Pamoja na kufuta amri hiyo, pia mahakama iliwataka wachungaji waliochaguliwa kuwa viongozi mbadala wa kanisa hilo katika uchaguzi uliofanyika katika mkutano ulioitishwa na mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa kanisa hilo Mchungaji John Mfuko na kufanyika Msimbazi Centre jijini Dar es Salaam, kuacha mara moja kufanya shughuli za uongozi wa EAGT na wakikaidi wakamatwe mara moja.

Katika hatua nyingine kwa kuwa hali ya kanisa hilo imekwisha tengamaa askofu Mwakipesile aliwaeleza wachungaji kuwa walikwishaunda bodi inayoundwa na maaskofu wa kanda tisa kuchunguza mikataba na mapato na kuludisha majibu katika taarifa za wachungaji.

‘Kwa hiyo tulishaunda bodi baada ya kuona wale wenzetu hawaeleiki waende pale wachunguze kilichopo,wachunguze kila kitu waone mikataba halafu baada ya hapo watuletee majibu kwa hiyo tumewaachia maaskofu wa kanda mimi simo na mimi ninangoja taarifa kama ninyi’ alisema.

Aidha pamoja na kukamilika kwa mgogoro huo ndani ya kanisa hilo baadhi ya maaskofu wa majimbo ya kanda ya nyanda za juu kusini mashariki katika taarifa zao kwa askofu mkuu wa kanda wamesema kuwa mgogoro huo ulisababisha sintofahamu kwa waumini na wachungaji huku baadhi yao wakiamua kuhama dhehebu.

Miongoni mwa majimbo yalioathirika kwa kiasi kikubwa ni pamoja na jimbo la Mufindi ambapo katika taarifa ya jimbo hilo iliyosomwa na katibu wa jimbo mchungaji Julius Donald kikoti  kwa askofu wa kanda inaeleza kuwa .

Jimbo la Mufindi liliingia kwenye shida tangia aliyekuwa askofu Flangson ndimbwa kuto kuwa na unyenyekevu na nidhamu kwa uongozi wa kanda, kwani mwezi April mwaka 2017 uongozi wa kanisa uliagiza kufungua kazi ya mungu eneo la MITI A  na baadaye alianza kupiga chenga kufanya kazi hiyo na kupelekea kusimamishwa nafasi hiyo.

Aidha taarifa imeendelea kuonyesha kuwa may 2017 baada ya kusimamishwa nafasi hiyo ndipo migogoro ilipoanza kuathiri jimbo zima kwa maana wachungaji kugawanyika kimitizamo.

Katibu aliendelea kueleza kuwa ilipofika tarehe 8,October 2017 baada ya vikao kufanyika ilipelekea uongozi wa kanda kumrudisha katika nafasi hiyo ambayo aliitumikia kwa mda wa miezi mine tu kwa kuwa mnamo tarehe 23/2/2018 wakiwa katika kikao cha kawaida cha jimbo Askofu Flagnson ndimbwa pamoja na aliyekuwa makamu wake mch.Essau Ngeyekwa waliaga rasmi mbele ya kikao au mkutano wa jimbo kwa madai wao ni wanachama wa upande wa pili wa mdhamini ili kupigania haki za EAGT.

Hata hivyo katibu huyo amesema kuwa licha ya mgogoro mkubwa uliojitokeza katika kanisa hilo kitaifa na sasa umekwisha basi yeye na viongozi wengine wamepata nguvu na na kuanza upya kwa sasa kufanya kazi.

Kwa upande wake Askofu Joseph mbwilo wa jimbo la Njombe ambaye ndie mwenyeji wa mkutano wa semina hiyo ya wachungaji anasema kuwa kilichobaki ni kuyafanyia kazi na kuyasimamia mafundisho yaliyo tolewa na Askofu mkuu ili kuwafnya washirika wadumu katika wokovu na kuwataka washirika kumtegemea mungu kwa kila jambo alilo fanya.

‘Mimi nadhani washirika sasa washirika wendelee kumtumikia bwana na mungu wetu ameshafanya kanisa letu lina amani wasijasahau waendelea kuliombea kanisa letu liwe salama zaidi’alisema.

Naye Askofu wa kanda ya nyanda za juu kusini mashariki Askofu Kayombo anasema kuwa lengo la semina hiyo kwa wachungaji ilikuwa ni matengenezo na marejesho kwa kanisa na hivyo tegemeo kubwa ni kuifanya injili ihubiliwe watu waokolewe  na watu wawe viumbe wapya wasiwe kama zamani na hilo litawezekana kwa umoja wao.

Kuhusu changamoto zilizojitokeza kwa wingi siku za nyuma katika jimbo la Mufindi kama taarifa ilivyoeleza Askofu huyo wa kanda amesema kwa sasa jimbo hilo limepata viongozi wapya na makini na hawategemei vurugu zozote katika jimbo hilo.

‘Kwa sasa hivi kwanza tumechagua uongozi mpya na uongozi makini na tumewapa maelekezo ya kutosha kabisa hatutegemi kama kuta kuwa na vurugu tena pale mufindi nategemea yaani muelekeo mpya na maendeleo mapya ya kanisa pale mufindi hizi vurugu vurugu pale hutaziona tena hilo nakuhakikishia’alisema.

JAMBAZI 'BISHOO' LANASWA MWANZA.



GSENGOTv

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limefanikiwa kumtia nguvuni mtu mmoja aitwaye Peter Thomas Nyanchiwa, anayedaiwa kuwa jambazi sugu, akiwa ameiba gari na kutaka kutoroka nalo kwenda kuliuza nchini Uganda.

Taarifa ya Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza imeeleza kuwa mtuhumiwa huyo na wenzake wawili, waliiba gari aina ya Toyota Costa lenye namba za usajili T 122 DLY mali ya Ismail Abdallah mkazi wa Mwanza.

Siku ya tukio la wizi huo inadaiwa mtuhumiwa akiwa na wenzake wawili walikodi gari hilo kuelekea Serengeti kwa madai ya kubebea watalii waliokuwa wameharibikiwa gari njiani wakati wakiendelea kutalii.

Ismail Abdallah alikubaliana nao na kuanza safari hadi walipofika eneo la Nata Serengeti ambapo mtuhumiwa na wenzake walimbadilikia na kumfyatulia risasi ya kwenye taya na kudondoka chini na watuhumiwa kuamini kuwa tayari wamemuua.

Baada ya kutekeleza tukio hilo walianza safari ya kuelekea Mkoani Geita kwa kupitia barabara ya Bariadi, Shinyanga hadi Kahama kwa lengo la kulipeleka gari hilo nchini Uganda kwa ajili ya kuliuza.

Taarifa za wananchi kwa jeshi la polisi zilisaidia kufanyika kwa msako na kufanikiwa kukamata gari hilo katika eneo la Runzewe mkoani Geita pamoja na Bastola yenye namba H44780Y ikiw ana risasi 12 ndani ya magazine.

Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani muda wowote upelelezi utakapokamilika. Hali ya Ismail Abdallah imeelezwa kuwa inaendelea kuimarika baada ya wananchi kumkimbiza katika hospitali ya wilaya ya Serengeti kwaajili ya matibabu.

HIVI NDIVYO 'ELIMIKA NA JEMBE FM' ILIVYOMWAGA MADINI SHULE YA SEKONDARY LORETO



GSENGOtV

🕎....Kazi nzuri imefanyika Jumamosi ya 29Sept2018 katika viwanja vya shule ya Sekondari Loreto ambapo @jembefm inaendelea kutoa nyenzo muhimu za masomo  kwa ajili ya elimu. Ni katika kuonesha nia ya dhati ya kuisaidia jamii katika nyanja husika.

Shuhudia jinsi wadau walivyoshusha madini. 

ImekaajE? 
#ElimikaNaJembeFm
 #LoretOsecSchooL 
#Mwanza
Time kupandikiza madini......👉 #TimeKupandikizaMadini

Friday, October 5, 2018

DAKTARI FEKI ANASWA BUGANDO, AWALIZA WENGI.



GSENGOtv


Walinzi katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) ya Jijini Mwanza wamemnasa mtu mmoja ambaye inadaiwa amekuwa akijifanya daktari na kujichumia fedha kwa kuwarubuni wagonjwa na watu wenye shida mbalimbali.
Wauguzi na Madaktari walikuwa wakimfuatilia kwa muda mrefu wakishirikiana na walinzi wa hospitalini hapo, baada ya kupokea malalamiko ya mara kwa mara toka kwa wananchi wanaokimbilia hospitalini hapo kupata huduma ndipo JUZI Jumatano ya tarehe 3/september 2018) majira  ya saa moja usiku, wakamnasa daktari huyo feki akiwa katika harakati zake za kufanya kinachodhaniwa kuwa ni utapeli.
Joseph Samwel (26) alikamatwa kwenye viunga vya hospitali hiyo akiwa kwenye harakati za kujifanya mtoa huduma akiwa na sare zenye kufanana na watumishi hospitalini hapo.      
Lucy Mogele ni Afisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa Bugando Mwanza naye anafunguka zaidi juu ya daktari huyu feki......

Thursday, October 4, 2018

BEKI YANGA AMALIZANA NA KIUNGO MGHANA WA SIMBA.



BEKI wa Yanga SC Gardiel Michael amemsamehe kiungo Mghana wa Simba SC, James Kotei aliyempiga ngumi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baina ya watani hao wa jadi Jumapili Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Hiyo ni kufuatia Mghana wa Simba SC kuomba radhi kwa kitendo chake kisicho cha kiuanamichezo Septemba 30 katika mchezo uliomalizika kwa sare ya 0-0.

“Wapendwa mashabiki wa soka, ningependa kuomba radhi kwa rafiki yangu Gardiel Michael na mashabiki wote wa soka kwa kilichotokea wakati wa mechi ya wapinzani ambayo haikuwa kitendo cha uanamichezo. Nina uhakika haitatokea tena,” amesema Kotei mapema leo

Na hiyo ilifuatia baada ya jana Msemaji wa klabu Yanga, Dismass Ten kusikitishwa na kitendo cha mchezaji huyo kushindwa japo  kuombwa radhi, hivyo kudai wamepeleka mashitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi dhidi ya Mghana huyo kwa kumpiga ngumi Gardiel. 

“James Kotei ni mchezaji mzuri, hajawa na rekodi ya kufanya mambo ya kihuni uwanjani, hizi mechi zina mambo mengi, yawezekana alikutwa na mambo ambayo hata yeye hajui ni kitu gani kilimkumba kimsingi ilitosha yeye kuomba radhi hata kwa kutumia mitandao ya kijamii kama mchezaji muungwana” alisema Ten jana.

“Ninashukuru kaka (James Kotei), msamaha umekubaliwa, heshima mno na upendo, yaliyotokea yamepita sasa, sisi wote ni familia moja ya soka, acha tugange yajayo,” alisema.

Pamoja na tukio hilo, pia Msemaji wa Simba SC, Hajji Sunday Manara alilalamikia kitendo cha beki Andrew Vincent ‘Dante’ wa Yanga SC kumpiga kichwa Nahodha wao, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

"Hatukuwa wajinga tulipoamua kukaa kimya, tumewasaidia wale waliokwenda kushitaki TFF na Bodi ya Ligi na hili pia walipeleke. Yule karusha ngumi na huyu kapiga kichwa,”amesema Manara na kuongeza; “Tukemee vitendo vyote vya kihuni Uwanjani siyo vya Simba tu,".

Manara amesema kwamba mchezaji anaporusha kichwa kwa mwenzake kwa dhamira ovu,haijalishi kimemuathiri kwa kiasi – lakini anastahili kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na dhamira pekee.

“Kama ilivyokuwa kwa Kotei, mliokwenda kumshitaki, sawa ni hivi, hatuungi mkono vitendo hivi na tunavikemea, ila tusiegemee upande mmoja, si Dante wala Kotei waliofanya sahihi, adhabu ikija ije kwa wote, wakiachiwa ni wote,”amesema Manara.

MKUU WA MKOA WA IRINGA ATEMBELEA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI MAKAO MAKUU – DAR ES SALAAM


 Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi, akiweka sahihi kwenye kitabu cha wageni alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Jijini Dar es Salaam, mapema leo tarehe 04/10/2018.
 Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF) Thobias Andengenye (wa pili kushoto) akitoa maelezo ya utendaji kazi wa Jeshi hilo kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini Dar es Salaam mapema leo tarehe 04/10/2018.
 Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi, akifuatilia kwa karibu maelezo aliyokuwa akiyatoa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji CGF Thobias Andengenye, alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini Dar es Salaam, mapema leo tarehe 04/10/2018.
 Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF) Thobias Andengenye akisalimiana na Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi, alipotembelea  Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini Dar es Salaam mapema leo tarehe 04/10/2018.
 Kamishna wa Operesheni Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CF) Billy Mwakatage akisalimiana na Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi, alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini Dar es Salaam mapema leo tarehe 04/10/2018.
Picha ya Pamoja, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF) Thobias Andengenye (wa kwanza kushoto) akiwa na Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi, pamoja na Kamishna wa Operesheni (CF) Billy Mwakatage (wa kwanza Kulia), mara baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika Makao Makuu ya Jeshi hilo, Jijini Dar es Salaam mapema leo tarehe 04/10/2018. (Picha na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji)
IMEANDALIWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO NA ELIMU KWA UMMA - JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI

SUMATRA YAFUNGUKA KUHUSU VISHOKA, WAMILIKI WA KAMPUNI WAPEWA NENO.





Mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa majini na nchi kavu SUMATRA jijini Mwanza umefunguka sababu za kusimamisha ruti kwa baadhi ya barabara huku wakikatiza ruti ndefu kwa gari ambazo hazina uwezo wa kubeba abiri 25.

Akizungumza na wandishi wa habari leo, Meneja wa Sumatra jijini humo, Gabriel Anthony amesema wao kama wenye mamlaka ya udhibiti wa usafiri wanayo mamlaka ya kulinda maslahi ya watoaji huduma wenye ufanisi pamoja na maslahi ya watumiaji huduma huku akisema wanayo jukumu la kutoa na kufuta leseni za usafirishaji.

 Anthony amesema Sumatra imepambana kuhakikisha inamaliza tatizo la vishoka ambao wamekuwa wakichukua leseni jambo ambalo lilikuwa linasababisha utapeli kwa wananchi huku akisema kwa sasa mmiliki au mfanyakazi mwenye kitambulisho cha kampuni ndio watapatiwa leseni za usafirishaji pekee.

" Siku hizi lile suala la mtu mmoja anakuja kuchukua leseni 50 au 100 halipo tena, na nitoe rai kwa wamiliki wa kampuni za usafirishaji kutokubali kuchukuliwa na vishoka na badala yake wafike wenyewe Sumatra na watahudumiwa kwa bei za kawaida kulinganisha na zile wanazotoa kwa vishoka," amesema Meneja huyo wa Sumatra.

MAAFISA MAENDELEO YA JAMII KIGOMA WANOLEWA UELEWA KUHUSU UALBINO

Mashirika ya Under The Same Sun, CEFA Tanzania na GNRC Tanzania, yaendelea kuelimisha jamii kuhusiana na ualbino
  • Mradi wa HAKI YETU wakutana na Maafisa Maendeleo  na ustawi wa jamii Kigoma na kuzungumza  madhara ya kuwatenga watu wenye ualbino
  • Maafisa Maendeleo ya Jamii, na ustawi wa jamii Kigoma wapigwa msasa uelewa kuhusu Ualbino
Maafisa Maendeleo ya Jamii, na ustawi wa jamii, kutoka manispaa ya kigoma Ujiji leo wamehudhuria mafunzo ya uelewa kuhusu ualbino na elimu ya Amani na maadili iliyotolewa na mradi wa Haki Yetu mkoani Kigoma.

Mradi huu huu umekua ukiendeshwa tokea mwezi Aprili mwaka huu katika Mikoa ya kigoma na maeneo ya jirani kwa ushirika wa wadau Mbalimbali lengo lao likiwa ni kutoa msaada kwa jamii kuelewa zaidi kuhusu ualbino, kupunguza imani potofu, kuwajengea watu wenye ualbino misingi ya kujiamini  ualbino pamoja na kutengeneza jamii shirikishi isiyokuwa na ma waa ya ubaguzi wa aina yoyote kwa watu wenye ualbini

Katika mradi huu misingi muhimu ambayo imekua ikiwekewa msisitizo ni pamoja na kuzingatia utu, kuwapa nafasi watu wenye ualbino bila kuwabagua, kushirikiana nao kwenye maswala ya elimu na uchumi lengo likiwa ni kujenga Taifa bora

Mradi wa Haki Yetu unatekelezwa na Mashirika ya Under The Same Sun, CEFA Tanzania na GNRC Tanzania, ukilenga kuelimisha jamii kuhusiana na ualbino.

DKT TIZEBA AIPONGEZA MVIWATA KWA KUWAUNGANISHA WAKULIMA NCHINI

Waziri wa kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akitoa salamu za Wizara ya kilimo mbele ya Mgeni rasmi ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) kwenye Maadhimisho ya miaka 25 ya mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) Leo tarehe 3 Octoba 2018 katika uwanja wa Jamhuri Mjini Morogoro. (Picha Zote Na Mathias Canal-WK)
Baadhi ya wakulima wakifatilia Maadhimisho ya miaka 25 ya mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) Leo tarehe 3 Octoba 2018 katika uwanja wa Jamhuri Mjini Morogoro
Naibu Waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) aakisalimiana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) kwenye Maadhimisho ya miaka 25 ya mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) Leo tarehe 3 Octoba 2018 katika uwanja wa Jamhuri Mjini Morogoro.
Waziri wa kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akisalimiana na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dkt Bashiru Ally mara baada ya kuwasili kwenye Maadhimisho ya miaka 25 ya mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) Leo tarehe 3 Octoba 2018 katika uwanja wa Jamhuri Mjini Morogoro.

Na Mathias Canal-WK, Morogoro

Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba (Mb) ameupongeza mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 kwa kuwa dira na Muungano wenye sauti moja yenye mshikamano na mafanikio makubwa kwa wakulima nchini.

Waziri Tizeba ametoa pongezi hizo Leo tarehe 3 Octoba 2018 wakati akitoa salamu za Wizara ya kilimo mbele ya Mgeni rasmi ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) kwenye Maadhimisho ya miaka 25 ya mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA).

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dkt Bashiri Ally, Waziri Tizeba alisema kuwa kipindi cha miaka 25 MVIWATA imekuwa mtandao wenye dhamira chanya kwa kuwaunganisha wakulima wadogo kwa kutetea maslahi yao na kujenga mikakati ya pamoja ya kujikwamua kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.

Aliitaka MVIWATA kuwa inapaswa kusimamia zaidi maslahi ya wakulima nchini kwa kuwa wahusika wakuu na wamiliki wa mfumo wa uzalishaji na kuwa sehemu ya mfumo wa maamuzi ya masuala yahusuyo maisha ya wakulima wadogo hususani mfumo wa uzalishaji na rasilimali ardhi.

Dkt Tizeba aliwahakikishia wananchama hao zaidi ya 2000 walioshiriki katika kongamano hilo la siku tatu kuwa wakulima wanapaswa kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka iwezekanavyo.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mtandao wa wakulima Tanzania (MVIWATA) Ndg Stephen Ruvuga akisoma risala ya maadhimisho hayo ameipongeza serikali katika kujenga uchumi wa Taifa katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini.

Alisema kuwa kwa kutambua hilo na hususani katika matumizi ya fedha za umma aliongeza kuwa kunapaswa kuongeza msisitizo katika usimamizi wa matumizi ya fedha za umma na kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Alisema kuwa pamoja na jitihada kubwa za serikali za kuimarisha sekta ya kilimo wakulima kwa ujumla bado wanachangamoto mbalimbali ikiwemo swala la ardhi, bei ya Mazao na soko la uhakika na mitaji ya uwezeshaji wakulima.

SHERIA MPYA YA JINAI RWANDA YAPOKELEWA KWA HISIA TOFAUTI.

Mabadiliko yaliyofanywa kwenye sheria ya jinai nchini Rwanda yamepokelewa kwa hisia tofauti miongoni mwa wadau wake katika jamii.

Mabadiliko hayo ni pamoja marufuku kwa waandishi wa habari kuchora vibonzo vinavyowakashifu viongozi wa ngazi za juu akiwemo rais wa nchi .

Waandishi wa habari wanahisi hilo linaloweza kusababisha wao kuwa matatani kwa njia rahisi.

RC MAKONDA AKUTANA NA WATENDAJI TPSF, WAWEKA MIKAKATI MADHUBUTI YA KUWASAIDIA WAFANYABIASHARA NA WAWEKEZAJI.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo ametembelea ofisi za Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania TPSF na kufanya mazungumzo ya kutafuta namna bora ya kuweka mazingira bora ya kibiashara ilikuondoa kero zinazowakabili wawekezaji na wafanyabiashara jijini humo. 

Miongoni mwa mambo waliyoridhia kushirikiana ni pamoja na utoaji wa elimu ya biashara, usimamizi wa fedha pamoja na namna bora ya kutumia fursa ya 10% za mkopo zinazotolewa na serikali kwaajili ya vijana, Wanawake na walemavu ili fedha hizo ziwe na tija.

Aidha RC Makonda amezungumza ushiriki wa TPSF katika ziara ya Rais Dkt. John Magufuli jijini Dar es salaam ambayo tunaamini itakuwa fursa kubwa kwa sekta zote ikiwemo Biashara, uchumi, afya, elimu, miundombinu na maji ambapo amewahimiza kuitumia vizuri ziara hiyo ili kufikia ndoto ya Dar es salaam kuwa jiji la kibiashara.

Pamoja na hayo RC Makonda ameelezea mpango wa kuweka kitengo cha uwekezaji (one stop center) itakayohusisha watendaji kutoka taasisi za TIC, TRA, TBS, BRELA, Uhamiaji na wadau wote wanaohusika na biashara ilikuondokana na ukiritimba uliokuwa ukipelekea mianya ya rushwa kwa wawekezaji na mwisho wa siku wawekezaji kukata tamaa ya kuwekeza Dar es salaam.

Kwa upande wake mkurugenzi wa taasisi ya sekta binafsi Tanzania TPSF Bwana Godfrey Simbeye amemuahidi ushirikiano wa kutosha kwa RC Makonda katika masuala mbalimbali yanayolenga kuliboresha jiji la Dar es salaam.

Wednesday, October 3, 2018

RAIS DKT.JOHN MAGUFULI AMUAPISHA KATIBU MKUU WIZARA YA MAMBO YA NJE NA SKAUTI MKUU



GSENGOtV

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 03 Oktoba, 2018 amemuapisha Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Hajat Mwantumu Bakari Mahiza kuwa Skauti Mkuu Tanzania.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Skauti Wabunge Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili na Mdhamini wa Chama cha Skauti Tanzania Alhaji Dkt. Ali Hassan Mwinyi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Rais wa Chama cha Skauti Tanzania Prof. Joyce Ndalichako, Makatibu Wakuu na viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli ambaye ni Mlezi wa Skauti Tanzania amekipongeza Chama cha Skauti Tanzania kwa kazi nzuri kinayoifanya ya kuwalea vijana kuwa wazalendo, kusaidia jamii hasa wakati wa matukio mabaya na majanga, kuwajengea tabia njema na kuwa na upendo.
Pamoja na kutoa pongezi kwa Skauti wote nchini, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili na kwamba ipo tayari kushirikiana nao kuzitatua.
Amempongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi kwa moyo wake wa upendo, unyenyekevu na jinsi anavyoendelea kushiriki katika shughuli za kijamii licha ya umri mkubwa alionao na amemhakikishia kuwa yeye na Watanzania wote wanampenda na wanamtakia kila la heri katika maisha yake.
Kwa upande wake Alhaji Ali Hassan Mwinyi ameelezea kufurahishwa kwake na kazi nzuri inayofanywa na Mhe. Rais Magufuli katika kuliletea Taifa maendeleo na amesisitiza kuwa “Ninakuhusudu Mhe. Rais Magufuli kwa kazi nzuri uyoifanya”.
Alhaji Mwinyi ambaye ni Mdhamini wa Chama cha Skauti Tanzania pia amemuomba Mhe. Rais Magufuli kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na chama hicho hapa nchini, na amewasihi viongozi wa Skauti Tanzania kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za nchi.
Kwa upande wao Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe na Skauti Mkuu wa Tanzania Hajat Mwantumu Bakari Mahiza wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwaapisha kushika nyadhifa hizo na wamemuahidi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viapo vyao, sheria, taratibu na kanuni za nchi.

PANGANI YAANDIKI HISTORIA SIKU YA WAZEE DUNIANI


 NAIBU Waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso kushoto akila na wazee wilayani Pangani IKIWA ni kilele cha siku ya wazee Duniani ambako kiwilaya yalifanyika kwenye viwanja vya Bomani wilayani humo
 MKUU wa wilaya ya Pangani,Zainabu Abdallah katika akiwa na wakazi wa mji wa Pangani wakati wa maadhimisho hayo
NAIBU Waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wazee

Afisa Tawala wa wilaya ya Pangani Gipson George akizungumza katika maadhimisho hayo



 Afisa Tawala wa wilaya ya Pangani Gipson George kushoto akishirikiana na wananchi wengine kubeba chakula kwa ajili ya kugawa kwa wazee
 Wazee wakipatiwa vipimo
 Wazee wakiwa kwenye maadhimisho hayo

 Sehemu ya wazee wilayani Pangani wakiwa kwenye maadhimisho hayoi
 Sehemu ya vyakula walivyoandaliwa wazee


NA MWANDISHI WETU, PANGANI.

IKIWA ni kilele cha siku ya wazee Duniani kwa wiki nzima iliyopita jana ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Pangani,Mbunge wa Jimbo hilo na Halmashauri imefanya kampeni ya “Nashukuru Mzee” ambayo imeacha alama kubwa na kuandika historia katika wilaya ya Pangani.

Maadhimisho hayo yalifanyika kwenye viwanja vya Bomani Pangani na baadae kujumuika kwa chakula cha pamoja nyumbani kwa Mkuu wa wilaya ya Pangani.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Mkuu wa wilaya ya Pangani Zainabu Abdallah alisema wanawashukuru wazee hao kwa kazi nzito walioifanya hadi sasa kuijenga wilaya hiyo na Taifa kwa ujumla.

“Kuwapa zawadi ya uhakika ambayo ni sekta ya afya kama jambo muhimu zaidi kwao nyakati hizi ikiwa ni kuhakikisha wazee wote ndani ya siku wanapata vitambulisho vyao vya matibabu bure kama inavyoelekeza sera ya wazee”Alisema.

“Lakini pia matibabu, upasuaji, vipimo na matibabu bure maalumu toka kwa wataalamu ndani na nje ya Pangani kwa wiki hii hadi kilele huku vipimo vya macho na ambao watapatikana na tatizo watapatiwa miwani”Alisema.

Hata hivyo alisema wataendelea kuwajengea uwezo na kuwapa tumaini jipya na mikakati sambamba na kusikiliza changamoto ambazo zinawakabilia

Kwa upande wake,Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso aliitaka jamii kuwaenzi wazee na kuwathamani kutokana na kuwa na mchango mkubwa kwao