ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, February 3, 2018

TWENDE TUKAISHANGILIE ALLIANCE KUTINGA LIGI KUU TZ BARA.



 ....Uongozi wa Jembe Media Group kupitia kipindi chake #SportsRipoti kinachoruka hewani kila siku saa #3hadi4usiku, tofauti na siku ya IJUMAA tu ambapo huruka saa #2hadi3usiku kwa heshima kubwa tunaungana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mhe. John Mongella kuitakia kila la kheri timu ya nyumbani #AllianceSportsAcademy kupata ushindi hatimaye Tukutane #VPL 

"Tulianza na Mungu, Tunamaliza na Mungu" Amen @juma_ayo @elikanamathias @danyajr_219 @moseswilliamtz @gsengo @jembenijembe #Masamaki @loveess_lovie

MSANII RADIO AZIKWA KWAO UGANDA.

 Msanii Radio wa nchini Uganda ambaye alifariki Februari 1, amezikwa leo kijijini kwao Nakawuka nchini Uganda, na kuhdhuriwa na maelfu ya watu kutoka sehemu mbali mbali za nchi hiyo na wasanii wa nchi jirani.



Hapo jana Ijumaa ya Februari 2, wananchi wa Uganda na mashabiki wa muziki walipata fursa ya kufanya ibada ya mwisho ya kumuombea marehemu kanisani, na kisha baadaye mwili wake kupelekwa kwenye uwanja wa michezo wa Airstip, ambapo walikesha nao huku kukipigwa show ya nguvu kutoka kwa wasanii mbali mbali wa nchini Uganda.

Kabla ya mazishi hayo kuliibuka mvutano mkubwa wa nguo ya kuvalishwa marehemu, huku Lilian Mbabazi ambaye ni mama wa watoto wake wawili ambaye mwenyewe alimtambulisha kama mke wake akitaka marehemu azikwe na suti aliyovaa kwenye tamasha la 'Nakudata' ambayo ndio ngoma iliyompa umaarufu na kumfanya atoboe kwenye game, na mwanamke wake mzungu ambaye amezaa naye mtoto mmoja akisema marehemu alitaka akifa azikwe na nguo za jeshi kwani alipenda kuitwa mwanajeshi, na hatimaye akavalishwa gwanda za jeshi.


Asubuhi ya leo mwili huo ulipelekwa kijijni kwao Nakawuka na kuwekwa kwenye makazi yake ya milele, ambapo kwenye tukio hilo watu walionekana kuwa wengi na baadhi wakizimia.

Miongoni mwa wasanii waliohudhuria mazishi hayo ni msanii na mbunge Jaguar wa Kenya, wasanii mbali mbali wa Uganda na viongozi wa serikali.

YANGA YAILIPUA LIPULI NYUMBANI KWAO 2-0.


YANGA SC imejivuta kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Lipuli Uwanja wa Samora mjini Iringa.

Ushindi huo unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 31 baada ya kucheza mechi 16, ikipanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, sasa ikiwazidi kwa pointi Azam FC ambao wanacheza mechi yao ya 16 usiku dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Yanga pia imepunguza pengo la pointi inazozidiwa na vinara, Simba SC hadi kubaki tano – lakini Wekundu wa Msimbazi nao watacheza mechi yao ya 16 kesho dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Erick Onoka aliyesaidiwa na Geoffrey Kihwilio na Janeth Balama, Yanga ilipata bao moja kila kipindi.

Na mabao hayo yalikuja baada ya Yanga kupata pigo dakika ya 17 kufuatia kipa wake wa kwanza Mcameroon, Youthe Rostand kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo nafasi yake ikichukuliwa na chipukizi, Ramadhan Awam Kabwili.

Kiungo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Papy Kabamba Tshishimbi alifunga bao la kwanza dakika ya 19 kwa kichwa akimalizia mpira uliotemwa na kipa Agathon Anthony Mkwando baada ya kichwa cha kuparaza cha winga Emmanuel Martin kufuatia kona ya kiungo Pius Charles Buswita

Kipindi cha pili, Yanga ya kocha Mzambia, George Lwandamina ilirudi na mchezo mzuri na kufanikiwa kupata bao la pili lililofungwa na Buswita dakika ya 55, aliyempiga chenga kipa Mkwando baada ya pasi nzuri mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa kutokea pembeni kulia na kufunga bao zuri.

Yanga ilijitahidi kuendelea kusaka mabao zaidi, lakini Lipuli walikuwa imara na kumaliza mchezo kwa kipigo cha mabao 2-0.

Lipuli FC; Agathon Mkwando, Stephen Mganga, Ally Mtoni, Martin Kazila, Joseph Owino, Novaty Lufunga, Seif Karihe/Tola Mangonela dk69, Mussa Nampaka/Zawadi Mawiya dk71, Adam Salamba, Malimi Busungu na Jamal Mnyate/Jerome Lembele dk78.

Yanga SC; Youthe Rostand/Ramadhani Kabwili dk17, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’, Papy Kabamba Tshishimbi, Emmanuel Martin, Raphael Daudi/Raphael Daudi dk86, Obrey Chirwa, Pius Buswita na Geoffrey Mwashiuya/Maka Edward dk81.

MIRADI YA JAMII YA GGM UMIZA KICHWA MKOANI GEITA

Mkuu wa mkoa wa Geita,Mhandisi Robert Luhumbi akiwa ameongozana na baadhi ya wakuu wa idara wa halmashauri ya mji wa Geita pamoja na viongozi wa chama cha mapinduzi (CCM) na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na wilaya ya Geita kwenye mradi wa vijana na wanawake uliopo magogo .

Mkuu wa mkoa wa Geita,Mhandisi Robert Luhumbi akipokewa na katibu tawala wa wilaya ya Geita,Thomas Dimme wakati alipowasili kwenye mradi wa vijana na wanawake wa magogo.

Mkuu wa mkoa wa Geita,Mhandisi Robert Luhumbi ,akipokea taarifa ya uchunguzi ambao umefanyika juu ya mradi wa vijana na wanawake   kutoka kwa mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Geita,Mhandisi Modest Aporinaly.
Mkuu wa mkoa wa Geita,Mhandisi Robert Luhumbi  akikagua baadhi ya vifaa ambavyo vilikuwa kwenye sehemu ya chakula(Kantine).

Mkuu wa mkoa wa Geita,Mhandisi Robert Luhumbi ,akiwa kwenye kalakana ya uchomeleaji wakati alipofika kujionea vifaa vilivyopo kwenye mradi huo.

Mkuu wa mkoa wa Geita,Mhandisi Robert Luhumbi  akipokea maelezo ya mashine ya kuchomelea kutoka kwa mmoja kati ya wahusika kwenye kamati ya uchunguzi.

Mkuu wa mkoa wa Geita,Mhandisi Robert Luhumbi  akikagua mashine ya kufyatulia matofali ya kisasa.

Na,Joel Maduka,Geita


Serikali Mkoani Geita imeeleza kusikitishwa na uendeshwaji wa miradi ya mgodi wa dhahabu wa Geita, (GGM) kwa kutozingatia sheria ya ushirikishaji kwa Halmashauri zilizopo mkoani humo na kushindwa kujulikana kwa gharama za miradi ya jamii inayotekelezwa na mgodi huo.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku  chache baada ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM)  kukabidhi mradi wa Maendeleo ya uchumi kwa Vijana na Wanawake ulipo Mtaa wa Magogo Kata ya Bombambili Halmashauri ya Mji wa Geita.

Hali hiyo ilimlazimu Mkuu wa mkoa wa Geita ,Mhandisi Robert Luhumbi  kuzulu  kwenye mradi wa vijana na wanawake uliopo kata ya Bomba mbili ,mtaa wa magogo kwa lengo la kujiridhisha baadhi ya vifaa ambavyo vilitakiwa kuwepo kwenye mradi huo na hata hivyo amebaini kuwepo kwa udanganyifu mkubwa kwenye  vifaa ambavyo  vilitakiwa kuwepo kwenye mradi huo.

Luhumbi  alisema  baadhi ya watumishi kutoka serikalini  na baadhi yao kutoka GGM wameendelea kushirikiana  kwa pamoja  kuhujumu miradi mingi  ambayo imekuwa ikilenga kuleta chachu ya maendeleo kwa wakazi wa Geita ambao wamezungukwa na Mgodi huo na kufuatia hatua hiyo ameagiza uchunguzi wa kina ufanyike ili kuwabaini wale wote ambao wameshiriki kuchakachua fedha za miradi hiyo.

“Sasa katika miradi yote ishirini na sita (26) ambayo imekwenda yote ina matatizo  na ajabu mwaka huu niliambiwa kuna fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya CSR ya mwaka huu nilikagua baadhi ya  miradi kuna mradi  mmoja nilikuta ni wa bilioni moja nukta sita lakini mimi siwezi kuficha hata tukitumia fedha vibaya kidogo tunaweza kutumia milioni mia tatu (300)  lakini bilioni moja nukta tatu inapotea  na watu kutoka ofisi zetu walikwenda mgodini wakaa na kuweka mkataba  wakurugenzi hawakuwepo mkuu wa wilaya afahamu baadae tunaambiwa fedha ipo tayari kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo nimesema sisi kama mkoa hatubariki miradi hiyo  kabisa”Alisema Luhumbi.

Hata hivyo kutokana na kuonekana upungufu kwenye miradi ya jamii Mhandisi Luhumbi amewakataa maafisa mahusiano ya jamii wa mgodi wa GGM kutokana na kushindwa kufanya shughuli  zao kwa weledi kwenye maeneo waliyopangiwa na mgodi  huo.

Na pia ameviagiza vyombo vyote vya sheria kuhakikisha wanaingia kwa undani zaidi na kufanya uchunguzi wa kutosha na ndani ya wiki moja endapo kuna mtumishi wa serikali  atakayebainika kuhujumu basi sheria ichukuliwe dhidi yake ikiwa ni pamoja na kumwajibisha.

Afisa sheria wa Mkoa huo Bi Sarah Mwangole alisema mradi wa Magogo ambao umekabidhiwa hivi karibuni umefanyika bila ya makubaliano baina ya Halmashauri na mgodi wa GGM hivyo pia wameshauri vyombo vya sheria kuingilia na kufanya uchunguzi na kwamba hadi sasa ofisini kwao hawajapata nyaraka zozote za mradi huo licha ya kuzihitaji.

Mtandao huu  umezungumza na Msimamizi wa kitengo cha mahusiano kwenye mgodi wa GGM Bw Joseph Mangilima ambaye alisema mengi  ya mambo yaliyozungumziwa hawezi kuyazungumzia yeye kwa kuwa hayahusiani na kitengo chake moja kwa moja na kwamba kazi iliyompeleka kwenye mradi huo ni kupeleka funguo za majengo baada ya kusikia mkuu wa mkoa anautembelea mradi huo.

MTOTO MLEMAVU AKUTANA NA MKONO WA MGIMWA SASA ATAKWENDA SHULE.

Na Fredy Mgunda, Iringa
MBUNGE wa Jimbo la Mufindi Kaskazini Mahamud Mgimwa amemwokoa mtoto wa kike ambaye ni mlemavu wa viungo kwa kumpeleka shule baada ya wazazi wake kushindwa gharama za masomo.

Mtoto huyo Rosemary Lutego ambaye ana umri wa miaka 15 alichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule yawasichana Iringa lakini alishindwa gharama za masomo na matumizi shuleni baada ya wazazi wake kukimbia jukumu la kumpeleka shule.

Mbunge Mgimwa baada ya kugundua changamoto inayomkabili binti  huyo licha ya  kufaulu na kushindwa kujiunga na wenzake kuanza masomo ya kidato cha kwanza ndipo alipoamua kumsomesha katika shule  maalum ya Wasichana Iringa ambayo ni mchanganyiko.

Mwanafunzi huyo alijulikana kama yuko nyumbani baada ya ziara ya kikazi aliyofanya mbunge Mahamud Mgimwa katika kata mbalimbali na kubaini uwepo wa mwanafunzi ambaye alikosa vifaa mbalimbali vya shule na kuamua kuchukua jukumu la kumsomesha hadi anamaliza shule.
Mara baada ya kupata taarifa za mwanafunzi huyo,Mgimwa alizungumza na wazazi na walimu katika shule ya Msingi Ikweha na kuwataka uongozi wa kijiji cha Ikweha kuwatafuta wazazi hao na kuwapeleka katika vyombo vya sheria huku akichukua jukumu la kumnunulia vifaa vyote vinavyohitajika shuleni hapo.

Aidha aliwataka wazazi wote ambayo wana tabia ya kuwazuia watoto waliofaulu kujitokeza haraka kabla ya msako kuanza popote pale katika jimbo la Mufundi Kaskazini ambapo wawapeleke shule kutokana na sasa hakuna ada wala mchango katika shule za serikali.
Aidha aliwataka wazazi kuacha tabia ya kuwafundisha watoto wao tabia ya kujifelisha katika mitihani ili waweza kuolewa wakati uwezo wa kufaulu upo kwa mtoto husika.
Akizungumza mara baada ya kupata msaada huo mtoto Rosemary Lutego alisema kuwa ndoto yake ya kupata elimu na kuweza kuja kuwasaidia wazazi wakeimeanza kupata mwanga kwani alidhani ndoto zake zimeishia darasa la saba.

alimshukuru sana mbunge Mgimwa msaada huo mkubwa wa kufanikisha masomo yake kwani itakuwa mfano mkubwa  wa wazazi wengine ambayo hawataki mtoto wa kike aende shule.

Aliongeza kuwa wazazi wake walimwambia kuwa wanaenda kutafuta fedha za kununulia vifaa lakini hadi sasa hawakuweza  kufanikisha hali iliyomlazimu abaki nyumbani wakati wanafunzi wengine wakiendelea na masomo.

"Namshukuru sana mbunge kwa kusikia na kuamua kugharamia masomo yangu ya sekondari nitahakikisha nasoma kwa bidii licha ya ulemavu wangu ili kuweza kuikomboa familia yangu katika umaskini." alisema 

LSF YAKUTANA NA WADAU WA WATOA HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA, JIJINI DAR ES SALAAM

 Mwenyekiti wa Muda wa Asasi ya kiraia ya Legal Services Facilities (LSF) Dkt. Benson Bani , akitoa neno la ufunguzi wakati wa warsha ya wadau wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria.
 Mkurugenzi wa Asasi ya kiraia ya LSF Bw. Kees Groenendijk akitoa mada yake ambapo alizungumzia mambo mbalimbali ikiwa ni  pamoja na kuelezea malengo, mambo mbalimbali yaliyofanyika kwa mwaka 2017 pamoja na mwelekeo kwa mwaka 2018, wakati wa warsha ya wadau wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria.
 Meneja Miradi wa LSF Bw.Ramadhani masele akielezea kiundani juu ya utendaji , mrejesho na nini kifanyike wakati wa warsha ya wadau wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria.
 Baadhi ya wakurugenzi na wajumbe wa Bodi za  ya wadau wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria wakitoa maoni mbalimbali wakati wa warsha hiyo
Afisa ufuatiliaji na tathimini kutoka LSF Bi. Saada Mkangwa akitoa ufafanuzi juu ya ukusanywaji wa taarifa za wanufaika wa ruzuku.
 Mkurugenzi wa miradi wa LSF Bi.  Scholastica Julla akitoa ufafanuzi wa jambo wakati wa warsha ya wadau wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria.
 Makundi mbalimbali ya ya wakurugenzi pamoja na wajumbe wa bodi za wadau wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria wakijadili mambo mbalimbali na namna watakavyofanya kazi na LSF kwa mwaka 2018.
 Wawakilishi katika makundi wakitoa mrejesho wa kile ambacho walikuwa wamekijadili wakati wa warsha ya wadau wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria, ambapo wote walionesha kuwa watafanya kazi zao kwa weredi zaidi kwa mwaka 2018
 Meneja wa ufuatiliaji na matokeo kutoka LSF Bw. Said Chitung akielezea mambo mbalimbali pamoja na malengo ya LSF kufikia 2021 wakati wa warsha ya wadau wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria.
Wakurugenzi na wajumbe wa bodi wakati wakiendelea kufuatilia mambo mbalimbali ya warsha ya wadau wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria iliyofanyika jijini Dar es salaam.
Picha na Fredy Njeje/Blogs za Mikoa Tanzania

SHERIA MPYA YA MADINI YA MWAKA 2017 INATAKA KURUDISHA UCHUMI KWA WANANCHI: MHE BITEKO


Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza na Uongozi wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga ambapo amesisitiza viongozi kusimamia Kanuni na taratibu juu ya usimamizi wa madini, leo 3 Februari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal
Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Kahama ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Fadhil Nkulu wakisikiliza maelekezo mbalimbali kutoka kwa Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko alipozuru Wilayani humo kwa ziara ya kikazi, Leo Februari 2018.
Mgeni Rasmi-Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza wakati wa kikao cha kazi na Uongozi wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga aakiwa katika ziara ya kikazi, leo 3 Februari 2018.

Na Mathias Canal, Shinyanga

"Sheria mpya ya madini ya mwaka 2017 inataka kurudisha uchumi wa madini kuwa uchumi fungamanishi kwa sekta nyingine, Hatuwezi kuwa na Mgodi ndani ya nchi ambao ajira zote zinapelekwa nje ya nchi kupitia huduma mbalimbali, unaweza kuagiza bidhaa za kila aina kutoka nje ya nchi lakini huwezi kuagiza ajira za wananchi wako zitoke nje kuja ndani, kamwe haiwezekani" 

Ni Kauli ya Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko leo 3 Februari 2018 wakati akizungumza na Uongozi wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga ambapo amesisitiza zaidi viongozi wa serikali katika maeneo yao kusimamia Kanuni na taratibu juu ya usimamizi wa madini.

Mhe Biteko alikaririwa akisema kuwa usimamizi madhubuti wa sheria na taratibu zilizowekwa ni sehemu imara na makini itakayowanufaisha watanzania ambapo watakuwa wamemuunga mkono kwa vitendo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ambaye amejidhatiti kwa mtazamo wa kuwanufaisha watanzania kupitia rasilimali zao.

Kanuni ya madini ya mwaka 2018 imeelekeza kuwa mgodi wowote unapoanza asilimia 100% za watoa huduma za chakula wanapaswa kuwa watu wa wananchi wa Tanzania, Pia huduma za ulinzi kwa asilimia 100% zinapaswa kutolewa na kampuni za ndani. Hivyo wataalamu wa sekta ya madini ni lazima kusimamia Kanuni hizo kwa usahihi.

Mhe Biteko aliongeza kuwa kampuni ya kigeni inaweza kufanya huduma hizo lakini ni lazima iingie ubia na wananchi wa Tanzania na kanuni hizi serikali imeziweka kwa makusudi kabisa ikiwa na mtazamo wa kuwanufaisha wananchi kupitia rasilimali zao.

Mhe Biteko alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho kimeingia mkataba na wananchi katika kuwatumikia kwa usimamizi madhubuti kupitia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015-2020 hivyo viongozi wa CCM wanapaswa kusimamia vyema serikali ili kuongeza tija katika utendaji.

Sambamba na CCM kusimamia vyema serikali pia Naibu Waziri huyo wa Madini amewataka watendaji wote wa serikali kuwa na umoja katika utendaji wao kwa usimamizi madhubuti wa rasilimali madini huku akitoa onyo Kali kwa watendaji wa serikali, Viongozi, vyama vya siasa na wananchi kujihusisha na rushwa kwani kufanya hivyo ni kuzififisha juhudi za serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Magufuli ya kuwainua wananchi wanyonge ili kila mtanzania aweze kunufaika na rasilimali zilizopo.

"Ndugu zangu ni aibu mno dhahabu na madini yetu mengine kuchimbwa nchini lakini yanajenga nchi nyingine, Uhakika wa barabara bado hatuna katika maeneo mengi, maji bado hatuna, sekta ya afya haijaimarika, Zahanati zina shida lakini pia Karibu kila maeneo hatujajidhatiti kwa asilimia 100% Kwa hiyo Mhe Dc naomba sana msicheke na mtu yeyote anayecheza na rasilimali zetu This Must be a Serious business, Mimi najua we have the same spirit lazima tufanye kazi kwa weledi.

Aidha, Naibu Waziri huyo wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe Fadhil Nkulu sambamba na Mbunge wa Jimbo la Msalala Mhe Ezekiel Maige kwa jukumu kubwa la utendaji wao katika kuimarisha juhudi na ufanyaji kazi uliotukuka katika sekta ya madini kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla huku akisisitiza kuwa kila kiongozi atapimwa kwa matokeo ya utendaji kazi wake na si kwa cheo chake.

" Waheshimiwa Viongozi, Mhe. Rais na wanatanzania watatupima kwa matokeo si kwa nafasi na vyeo vyetu" alisisitiza Mheshimiwa Biteko wakati akihitimisha hotuba yake kwa uongozi wa serikali wilayani Kahama.

Friday, February 2, 2018

KIFO CHA MSANII RADIO KIMEZUA MAPYA WASANII WA WALIA NA SERIKALI YA UGANDA


Kifo cha msanii huyo cha fananishwa na baadhi ya matukio yaliyowahi kuwakuta wasanii wawili kutoka Uganda.

ZIARA YA MHE.SHANIF MANSOOR,MBUNGE WA JIMBO LA KWIMBA 2018

NA ZEPHANIA MANDIA WA G.SENGO TV.
TAREHE 01.02.2018

MBUNGE wa Jimbo la Kwimba mkoani Mwanza, Shanif Mansoor, amesema asilimia 80 ya vijiji jimboni hapa vipo mbioni kupata umeme.

Amesema miradi hiyo ya umeme wa Rea Vijijini, itapatikana kwa kipindi cha kuanzia sasa hadi kufikia mwaka 2020, ili kuwasaidia wananchi kupata maendeleo.

Mansoor aliyasema hayo juzi katika ziara yake ya kikazi jimboni hapa, na kwamba anahitaji kuwasaidia wananchi kupata maendeleo ya kisekta.

"Napenda kusema kazi tumeshaanza. Mwaka huu kuna mradi mkubwa sana wa umeme wa Rea Vijijini. Baadhi ya maeneo umeme haujafika....lakini tutapata umeme hadi Mwakilyambiti.

"Kwa hiyo apambana kuhakikisha asilimia 80 ya vijiji vya Jimbo la Kwimba vinapata umeme wa Rea, ifikapo mwaka 2020," alisema Mbunge huyo wa Jimbo la Kwimba na kuongeza:

“Naomba sana ushirikiano wenu wananchi, ili tuijenge Kwimba na taifa kwa ujumla katika maendeleo ya kweli.”

Katika hatua nyingine, Mansoor aligawa majembe ya kilimo 18,000 yenye thamani ya zaidi ya sh. Milioni 200, ambapo karibu kila kaya itanufaika na vifaa hivyo.

Alisema lengo la kuwawezesha wananchi vifaa hivyo vya kilimo, ni kuwawezesha kuzalisha mazao ya chakula na biashara.

Alisema kuwa, licha ya kuahidi kutoa vifaa hivyo kwa wananchi lakini pia amelenga kuinua uchumi wa kila mwananchi kupitia kilimo, ndani ya
Jimbo la Kwimba.

"Staki mpate tabu wakati mbunge wenu nipo. Halmashauri yetu ya wilaya nayo nimeipatia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara, katika Shule ya Sekondari Bujiku Sakila.”

Aliipongeza pia Serikali kwa kujenga mradi wa maji jimboni Kwimba, unaogharimu zaidi ya sh. Milioni 576.

Kwa mujibu wa mh.Mansoor, mradi huo tayari umeshakamilika kwa kiwango cha
asilimia 80, ambapo umelenga kupunguza kama si kuondoa kabisa adha ya maji katika jimbo la kwimba.

“Mimi mwenyewe nataka kila kijiji kiwe na mradi wa maji safi na salama ya kunywa kutoka ziwa victoria,umeme na miundombinu rafiki pamoja na kutengeneza barabara za mitaa ya miji inayoendelea katika jimbo la kwimba.

“Nimechimba mabwawa na visima zaidi ya 35 vya maji kwa nguvu zangu. Lengo langu ni kuwasaidia wananchi walioniamini na kunipa kura za kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa 2015,” alisema Mansoor.

Wakati huo huo, Mansoor amewakatia bima za afya viongozi wote wa Halmashauri za Kata wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Kwimba.

Alisema kuwakatia kwake bima viongozi hao ni lengo la kutaka kuwasaidia, katika changamoto za masuala ya afya, hivyo anahitaji kuona jamii inatekeleza vema majukumu yake.
Mbunge wa Jimbo la Kwimba mkoani Mwanza, Shanif Mansoor akigawa majembe kwa kikundi cha akinamama waliofika kwenye kusanyiko lake, ambapo pia alipata nafasi ya kusikiliza kero za wananchi.
Jembe ni mali.
Mimi ni jembe.
Mansoor aligawa majembe ya kilimo 18,000 yenye thamani ya zaidi ya sh. Milioni 200, ambapo karibu kila kaya itanufaika na vifaa hivyo.
Karibu kila kaya itanufaika na vifaa hivyo vya kilimo.
Mkutano wa ndani na wanachama wa CCM.
  Mansoor alikutana na wananchi wa jimbo lake kupokea ushauri na pia kuwasilisha mipango mikakati kwa hatua zijazo.
Kikao kikiendelea.
Mansoor na wana Kwimba.
Kwimba na umakini.

VIDEO:- MASUALA MUHIMU YALIYOSISITIZWA NA KAMATI YA MAUDHUI YA TCRA KWA WANAHABARI KANDA YA ZIWA



MAUDHUI YANAYOLENGA MAENDELEO
Mada Iliyowasilishwa na Bwana Joseph M. Mapunda, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Katika Warsha ya Wahariri na Watengenezaji wa Vipindi vya Redio na Televisheni, Mwanza ,Februari01, 2018.

Utangulizi
Nchi yetu imejaliwa  kuwa na rasilimali nyingi za kuiwezesha kupata maendeleo  makubwa katika nyanja zote za uchumi, huduma  za jamii, utamaduni, habari na michezo bila kusahau suala zima la demokrasia (siasa). Kuna fursa nyingi za kuliwezesha Taifa kupata maendeleo ya haraka ikiwa rasilimali zilizopo zitatumika kikamilifu  na kwa umakini mkubwa.

Kwa upande wa sekta ya habari na utangazaji, sera na sheria zilizopo zimetoa  nafasi na uhuru mkubwa kwa sekta ya umma(Serikali) na sekta binafsi kumiliki na kuendesha vyombo vya habari na utangazaji kwa lengo kuu la kuvifanya viwe  chachu ya kuhamasisha  wananchi na wadau wengine ndani na nje ya nchi yetu kushiriki kikamilifu katika kutekeleza mipango ya maendeleo kwa faida ya vyombo vyenyewe, wananchi na Taifa kwa ujumla.


Ukuaji wa Sekta ya Habari na Utangazaji
Vyombo vingi vya habari na utangazaji vimeanzishwa hapa nchini tangu miaka ya 1990 wakati mfumo wa uchumi ulipoanza kushirikisha rasmi Sekta binafsi tofauti na huko nyuma ambapo shughuli zote kuu za uchumi na kijamii  zilikuwa zikimilikiwa na kuendeshwa na Serikali.

Utaratibu huo pia ulihusisha masuala ya kisiasa ambapo nchi ilikuwa ikitawaliwa  katika misingi ya demokrasia ya Chama kimoja cha siasa (one Party democracy).

Idadi ya Vyombo vya Habari na Utangazaji
Hadi sasa kuna vituo 32 vya televisheni; vituo 155 vya redio na idadi kubwa ya mitandao ya kijamii. Hali kadhalika kuna magazeti na majarida 432 yaliyosajiliwa kisheria. Vyombo vingi zaidi vya habari na utangazaji vinaendelea kusajiliwa na hivyo kutoa fursa nyingi za uwekezaji na ajira katika Sekta hii muhimu ambayo baadhi ya watu wamezoea kuiita Mhimili wa Nne (Fourth Estate). Zaidi ya asilimia tisini na tisa (99 per cent) ya vyombo vilivyopo  vinamilikiwa na Sekta binafsi.

Utajiri huu mkubwa wa idadi ya vyombo vya habari na utangazaji ni ushahidi tosha kuwa sekta hii ni nyenzo  muhimu na ya kutegemewa katika kuwapa habari,  kuwaelimisha  na pia kuwahamashisha wananchi kushiriki kikamilifu na kwa uelewa mkubwa katika kuibua na kutekeleza mipango ya maendeleo ya nchi yetu.

Kwa vile zaidi ya asilimia sabini na tano (75 per cent) ya Watanzania wanaishi vijijini wakishughulika na kilimo---ambacho ni uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa--- ni wazi kuwa vyombo vya habari na utangazaji vina wajibu mkubwa wa kuelekeza nguvu na rasilimali zake huko ili kutangaza mafanikio, matarajio na changamoto za kilimo, ufugaji, afya, maji, elimu, utamaduni na michezo pamoja na mambo mengine mengi ya msingi.

Hali Ipoje?
Pamoja na idadi hiyo kubwa ya vyombo vya habari na utangazaji, sehemu kubwa ya makala na habari zinazorushwa na vyombo hivi zinahusu matukio na shughuli za mijini ambako kuna wananchi wachache. Hali hii inamaanisha  kuwa juhudi na matukio ya watu wengi waishio vijijini na wilayani hupewa nafasi kidogo sana katika matangazo ya vyombo vyetu.

Natoa rai kwa wamiliki na watendaji wakuu wa vyombo vyote vya habari na utangazaji kuonyesha uzalendo usioyumba (unshakable patriotism) ili kuhakikisha kuna kuwa na uwiano mzuri/sawia wa habari na matukio ya mijini na zile za vijijini ili kutoa fursa na hamasa kubwa kwa wananchi wote kujuzwa juu ya mambo muhimu yanayoendelea nchini na hivyo kuwawezesha kuwa mstari wa mbele katika kutekeleza mipango mbali mbali ya maendeleo.

Kuelekea Uchumi wa Kati
Serikali imedhamiria  kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati ( middle income economy) ifikapo mwaka 2020. Mkazo hapa umewekwa katika kujenga na kuimarisha Sekta ya Viwanda kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa bidhaa  za viwandani hasa zile zinazotokana na malighafi za kilimo na ufugaji na shughuli nyingine  nyingi za kiuchumi kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa. Mkakati huu pia unahusu ufufuaji wa viwanda vilivyokufa na vile ambavyo ujenzi wake haujakamilika. Mafanikio ya juhudi hizi yatawezesha kupatikana ajira nyingi, ongezeko la uzalishaji mali,  mapato ya Serikali na maslahi ya wananchi kwa ujumla.

Vyombo vya habari na utangazaji vina nafasi kubwa ya kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kuielewa dhana  nzima ya uchumi wa viwanda na jinsi wanavyoweza kushiriki katika utekelezaji wa azma hii ya Serikali kwa vitendo.

Twende Vipi?
Uchumi wa viwanda ni dhana pana sana. Inahusisha sekta zote za uchumi na jamii (production and service sectors). Sekta zote hizi zinaingiliana na kushabihiana katika mfumo wake wa utendaji. Naomba tuangalie kwa muhtasari baadhi ya sekta na jinsi gani vyombo vya habari  na utangazaji vinaweza kuchukua nafasi yake katika kurusha matangazo yenye kuendana na dhana ya viwanda nchini.

Kilimo
Hii ni  sekta kiongozi katika uchumi wa Taifa letu na itaendelea kushika nafasi hiyo kwa miaka mingi ijayo. Kwa kuzingatia hilo, ni vema wakulima na wafugaji wakaelimishwa mbinu za kilimo cha kisasa ili kuzalisha mazao bora yenye kukidhi mahitaji ya ndani ya nchi na ziada kwa ajili ya soko la nje.

Matangazo yazingatie kuwaelimisha wananchi juu ya misingi bora ya kilimo na ufugaji hasaupatikanaji kwa wakati wa pembejeo na zana nyingine muhimu za uzalishaji na pia jinsi ya kuyafikia masoko kirahisi ili bidhaa zitakazo zalishwa zisiozee mashambani.
Elimu zaidi pia itolewe na kutiliwa mkazo kuhusu uanzanzishwaji wa viwanda vinavyotegemea mazao ya kilimo katika ngazi ya vijiji ili kuyaongezea thamani. Mkakati huu utawahakikishia wananchi ajira nyingi, mapato makubwa, afya bora na huduma muhimu za kijamii.

Kupitia viwanda, wananchi wataweza kula vyakula safi na salama vilivyosindikwa hapa nchini. Hali hii itatuondolea  tatizo sugu la kula vyakula vibovu na hatarishi  kutoka nje ya nchi. Wengi wetu hapa tumewahi kusikia uvumi kupitia mitandao ya kijamii na kwingineko kuwa soko letu limevamiwa na mchele wa plastiki, samaki wa plastiki, mayai bandia ya kuku, maziwa, nyama, na bidhaa nyingine  zisizokuwa na viwango vinavyokubalika kiafya.

Hali kadhalika, Watanzania wengi huvaa nguo na viatu vya mitumba wakati tuna pamba na ngozi nyingi zinazoweza kuzalisha bidhaa bora. Suala la viwanda vidogo vidogo vilivyoanzishwa na wananchi wenyewe katika ngazi ya vijiji na wilaya litiliwe mkazo.
Wananchi waelezwe na kuelemishwa ipasavyo kuhusu masuala haya muhimu na jinsi ya kuyakabili ili kutuwezesha kujitegemea, kulinda afya zetu na kujijengea miili imara na akili timamu.

 Elimu ni Kila Kitu
Wote tunafahamu umuhimu wa elimu katika uchumi na ustawi wa jamii. Shule na vyuo vyetu katika ngazi zote vihamasishwe  na viwezeshwe kutoa wahitimu au wataalam wa fani mbali mbali watakaoweza  kulisaidia Taifa kwa vitendo kuleta maendeleo na mapinduzi katika maisha yao.

Vyombo wa habari na utangazaji vijikite katika kurusha matangazo yanayolenga  maendeleo na kuhakikisha watu wote, hasa maskini, wanaondokana na hofu ya njaa na shida nyingine nyingi za daima ili kufikia kiwango cha maisha yanayomstahili  binadamu.

Kwa mfano, akina mama huko vijijini na baadhi ya miji yetu wakipunguziwa mzigo wa kujitwika mitungi na ndoo za maji kilometa nyingi wanaweza kupata fursa  za kujihusisha kikamilifu katika uzalishaji mali kwa upeo na ufanisi mkubwa. Tutilie mkazo dhana ya watu kujiletea maendeleo yao wenyewe.

Kupitia tafiti mbali mbali vyombo vya utangazaji vinaweza kuandaa  makala na vipindi maalum vitakavyoonyesha au kuelekeza  mambo yanayowezekana kufanywa  na jinsi yanavyoweza kufanyika. Ni dhahiri kuwa watu wenye elimu na ujuzi wanaweza tu kuwa na manufaa kama watachanganyika na kushirikiana kwa dhati na jamii inayowazunguka. Haya yote yanaweza kutendeka  ikiwa moyo wa uzalendo utajengeka na kuimarishwa ndani ya vyombo vya habari na utangazaji.

Afya na Ustawi wa Jamii
Hii ni dondoo  yenye uzito mkubwa katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo. Tunahitaji kuwa na watu wenye siha nzuri na ya kutegemewa  katika shughuli nzito na muhimu za maendeleo. Ili tuweze kupata  maendeleo ya kweli na ya haraka inabidi  suala la afya litiliwe mkazo maalum  na vyombo vya habari na utangazaji. Jukumu la msingi hapa ni kuandaa na kurusha vipindi na makala zenye kuelimisha watu kuhusu namna ya kuzuia na kujikinga na maradhi, kutunza mazingira, kula vyakula vyenye kujenga mwili, kunywa maji safi na salamana kuondokana na unywaji wa pombe zilizotengenezwa bila kuzingatia masharti na viwango vinavyokubalika kiafya.

Uzoefu unaonyesha kuwa makala na taarifa nyingi zinazorushwa  zinahusu matukio ya magonjwa ya mlipuko na majanga mengine ya kiafya na ya kijamii. Tuandike na tutangaze habari zinazowahamisisha na kuwashawishi watu  kuishi vizuri kwa kuzingatia masharti na matakwa ya afya bora.

Watu wengi wamezoea au wanalazimika kula vyakula vya mitaani katika mazingira machafu.  Juhudi za dhati zifanyike kuwahimiza mamalise na babalishe kupika vyakula bora na ambavyo vimeandiliwa kwenye mazingira bora na kupakuliwa kwenye vyombo  vinavyokubalika kiafya.

 Siku hizi Watanzania wenzetu wengi wanasumbuliwa na magonjwa yasiyotibika kama saratani, ambayo kwa kiwango kikubwa chanzo chake ni kula vyakula visivyokuwa na viwango sahihi. Shughuli za taasisi kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Vyakula na Madawa Tanzania (TFDA) zipewe kipaumbele katika matangazo ili mchango wao uweze kuwa wa manufaa zaidi kwa wananchi na ustawi wa jamii.

Vile vile, elimu ya kina itolewe kuhusu faida zinazotokana na kula vyakula vya asili (fresh foods) kama vile mboga zilizolimwa  katika mazingira safi na salama, matunda, nafaka za mafuta kama karanga, ufuta, alizeti, nazi na vingine vingi. Kwa bahati nzuri bidhaa hizi zote zinazalishwa kwa uwingi hapa nchini kwa bei ambazo watu wengi wanaweza kuzimudu. Tujihadhari na bidhaa zilizosindikwa  kutumia madawa/chemikali ili kuepuka athari za kiafya.

Utamaduni, Muziki na Burudani
Sekta  hii pia ina mchango mkubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu. Vituo vya utangazaji viandae na kurusha vipindi vinavyohamasisha  ukuaji na uendelezaji wa muziki na burudani zenye  maudhui ya yanayoendana nautamaduni wetu wa Kitanzania. Pamoja na kuwepo umuhimu wa kurusha muziki na ngoma kutoka nje ya nchi ni vema busara ikatumika kuchagua maudhui yenye kulenga uendelezaji na udumishaji wa mila na desturi za  Kitanzania.

Ngoja niwashirikishe kitu kimoja hapa. Siku chache zilizopita nilipigiwa simu na mtu mmoja ambaye alinidokeza kuwa alikiona  kipindi cha muziki katika kituo kimoja cha televisheni cha Dar es Salaam ambacho kilirusha wimbo wenye maudhui ya kulidhalilisha Taifa letu. Sehemu ya wimbo husika una maudhui yanayosomeka “…..Bongo kubaya twende zetu Ulaya; Bongo maisha mabaya, Ulaya kuna raha tele…..”.Je, kwa maudhui kama haya tunaitendea haki nchi yetu?

Tuijengee heshima nchi yetu kwa kurusha vipindi vyenye maudhui ya kizalendo na yale yanayohamasisha sifa nzuri na umoja na mshikamano wa Taifa letu.

Amani na Utlivu
Nchi yetu imejizolea sifa nyingi sana duniani kama mahali penye amani, usalama na utulivu. Sifa hii imetujengea heshima namazingira mazuri kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Sekta yetu ya utalii na sekta za uwekezaji zimevutia wageni wengi kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza katika uchumi wetu kutokana na sifa nzuri za Watanzania. Kwa kuzingatia ukweli huo, vyombo vyetu vinapaswa kuendelea kutangaza kwa nguvu zote taswira ya Tanzania yenye amani, utulivu na usalama.

Jukumu hili lichukuliwe kwa uzito mkubwa hasa tukizingatia  kuwa tabia ya wageni kwa maana ya watalii na wawekezaji ni kwenda mahali ambapo usalama  wao na wa mali zao unalindwa kama mboni za jicho lako!

 Kutangaza kwa ushabiki vitendo vya uhalifu na matamshi ya kisiasa yanayoashiria uvunjifu wa amani yana athari kubwa sana katika juhudi zetu za maendeleo. Tuwahakikishie wageni wetu kuwa Tanzania ni nchi tulivu, inazingatia utawala wa kisheria na pia inaendesha mambo yake kwa uwazi na inazingatia kwa dhati suala zima la haki za binadamu. Dondoo yetu kubwa iwe kutangaza habari zenye maslahi kwa Taifa kiuchumi, kisiasa na kijamii.

HITIMISHO
Tanzania ni nchi yetu nzuri sana. Ina watu wapole na wakarimu. Majirani zetu na watu wengine duniani  wanaimezea mate. Tuna haki na wajibu kuilinda, kuiheshimu na kuienzi kwa uzalendo wa hali ya juu ili tuweze kuijengea mazingiria imara ya maendeleo katika nyanja zote.

Dhamana tuliyopewa ya kulitumikia Taifa hili kupitia vyombo vya habari na utangazaji tuiheshimu na tuitumie vizuri kwa maslahi ya Taifa na ya wananchi wote. Nawatakia mafanikio katika kazi zenu. Mungu awalinde na awaongoze daima.