ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, September 19, 2018

MTOTO WA MFALME PRINCE WILLIAM KUKUTANA NA RAIS MAGUFULI.




Mwanamfalme William wa Uingereza anapangiwa kukutana na rais wa Tanzania Dkt John Magufuli wiki ijayo wakati wa ziara yake ya siku saba Afrika.

Anatarajiwa kuzuru pia Kenya na Namibia katika ziara hiyo ambayo si ya kikazi. Ziara hiyo itafanyika kuanzia 24 Septemba hadi 30 Septemba.

Lengo kuu la mwanamfalme huyo litakuwa kufuatilia juhudi za kukabiliana na ujangili na uhifadhi wa wanyama.

Atafanya ziara hiyo katika wadhifa wake kama rais wa mashirika yanayotetea uhifadhi wa wanyama ya United for Wildlife na Tusk Trust.

Amekuwa pia mlezi wa shirika la Royal African Society linalolenga kukuza uhusiano kati ya Afrika na Uingereza na hushiriki sana juhudi za kukabiliana na ujangili.

Akiwa ziarani Tanzania, Mtawala huyo wa Cambridge, atafanya mashauriano na Rais Magufuli kuhusu juhudi zinazopigwa na taifa hilo katika kukabiliana na ujangili na ulanguzi wa wanyama pori kwa mujibu wa shirika la habari la Press Association.

Kadhalika, atazuru bandari ya Dar es Salaam kujifahamisha zaidi kuhusu juhudi zinazopigwa na taifa hilo, Tanzania imekuwa ikifanya juhudi kukabiliana na ujangili na ulanguzi wa wanyama.

Mwaka 2013, mwezi Oktoba, ilizindua Operation Tokomeza Ujangili ingawa ilisitishwa takriban mwezi mmoja baadaye, huku watetezi wa haki wakiwalaumu waliokuwa wanaendesha operesheni hiyo kwa ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Tanzania ilikuwa na tembo 110,000 mwaka 2009 lakini idadi hiyo imeporomoka hadi kufikia tembo 43,000 kutokana na ujangili.

Moja ya malengo ya ziara ya Mwanamfalme William Afrika ni kupigia debe mkutano mkuu wa kukabiliana na ulanguzi wa wanyamapori ambao utaandaliwa jijini London kati ya 11-12 Oktoba.

Mkutano huo ambao kwa kirefu unafahamika kama Illegal Wildlife Trade Conference, unalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na ulanguzi wa wanyamapori, kwa kuangazia mambo matatu makuu: ulanguzi wa wanyama, wadudu na mimea kama uhalifu, kujenga ushirikiano na kufunga masoko yanayotumiwa na wahalifu kulangua wanyamapori.

Taarifa ya Kensington Palace inasema ingawa atakuwa katika ziara ya kibinafsi, ameombwa na Malkia kutekeleza shughuli kadha rasmi kwa niaba yake.

Akiwa nchini Kenya, Mwanamfalme William atatembelea kikosi cha wanajeshi wa Uingereza cha 1st Battalion cha Irish Guards Battlegroup.

William huwa na cheo cha kanali wa jeshi la Ireland, na anatarajiwa kujifahamisha ni jinsi gani wanajeshi wa Uingereza na Kenya wanafanya kazi kwa pamoja kuimarisha shughuli zao.

Kikosi hicho cha Irish Guards Battlegroup hujumuisha wanajeshi wa Ireland na kundi la wanajeshi wa kenya ambao wamekuwa wakipokea mafunzo kutoka kwa kikosi cha jeshi la Uingereza.

Nchini Namibia, mtawala huyo anatarajiwa kukutana na makamu wa rais Nangolo Mbumba na pia ahudhurie hafla ya kusherehekea ushirikiano kati ya Uingereza na Namibia katika makazi ya balozi wa Uingereza nchini humo Kate Airey.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.