ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, July 13, 2018

AZAM FC MABINGWA TENA KOMBE LA KAGAME, WAINYUMA SIMBA 2-1



TIMU ya Azam FC imefanikiwa kutetea taji lake la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Simba SC jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. Shujaa wa Azam FC hii leo alikuwa ni Nahodha na beki, Aggrey Morris Ambroce aliyefunga bao la ushindi dakika ya 80 kwa shuti kali la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 30, baada ya kumchungulia kipa Deogratius Munishi ‘Dida’. 

Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua, Azam FC ilitangulia kwa bao la mshambuliaji wake hodari, Shaaban Iddi Chilunda dakikaya 33 ambaye leo alikuwa anacheza mechi ya mwisho kabla ya kwenda kuanza kuutumikia mkataba wa mkopo Tenerife ya Daraja la Kwanza Hispania.

Shahban Iddi ambaye anatimiza miaka 20 Julai 20 Mwaka huu tangu azaliwe mwaka 1998, alifunga bao hilo akiunganisha kona maridadi iliyopigwa na winga wa zamani wa Simba SC, Ramadhani Singano ‘Messi’.

Chilunda aliyejiunga na akademi ya Azam FC Jumamosi ya Julai 21, mwaka 2012 kabla ya miaka miwili baadaye kupandishwa kikosi cha kwanza, ameibuka mfungaji bora wa michuano hiyo kwa mabao yake saba.

Lakini Simba SC ilifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 62 kupitia kwa mshambuliaji wake mpya, Meddie Kagere iliyemsajili mwezi uliopita kutoka Gor Mahia ya Kenya.

Mchezaji huyo raia wa Rwanda mwenye asili ya Uganda, alifunga bao hilo akimalizia pasi ya kiungo Said Hamisi Ndemla baada ya kazi nzuri ilitofanywa na mshambuliaji Rashid Juma.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Thierry Nkurunziza kutoka Burundi, Simba ilicharuka dakika za mwishoni katika kusaka bao la kusawazisha, lakini safu ya ulinzi ya Azam FC ilikuwa makini kuondosha hatari zote.

Mapema katika mchezo uliotangulia, Gor Mahia Mahia ya Kenya ilifanikiwa kumaliza katika nafasi ya tatu, baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya JKU, mabao ya Francis Mustafa na Samuel Onyango.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razack Abalora, Aggrey Morris, Nicolas Wadada, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, Frank Domayo, Joseph Mahundi, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Shaaban Iddi/ Yahya Zayed dk87, Ditram Nchimbi na Ramadhani Singano ‘Messi’/ Oscar Masai dk77.

Simba SC: Deo Munishi, Mohammed Hussein, Nichoals Gyan, Paul Bukaba, Pascal Wawa, James Kotei, Mzamiru Yassin, Said Ndemla/ Moses Kitandu dk83, Meddie Kagere, Mohammed Rashid na Marcel Kaheza/Rashid Juma dk60.  

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.