ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, June 19, 2018

UELEWA FINYU, NA MFUMO DUME BADO VIKWAZO KATIKA VITA DHIDI YA SELI MUNDU (SIKO SELI) NCHINI.



GSENGOtV
MWANZA. Kila mwaka zaidi ya watoto 10,000 nchini huzaliwa wakiwa na matatizo  kwenye chembe chembe nyekundu za damu zao na hivyo kupata ugonjwa wa selimundu (sickle cell anemia).

Hali hiyo inatokana na ufahamu mdogo wa jamii na kutokuwa na utamaduni wa kupima afya.

Hali hiyo inaifanya Tanzania kuwa nchi ya nne duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa seli mundu ambapo nchi inayoongoza ni Nigeria, India na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC) huku katika Afrika ikiwa ya tatu.

Emmanuela Ambrose ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto, Kitengo cha damu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) jijini Mwanza, anasema sababu kubwa inayochangia kuwepo kwa idadi hiyo nchini  ni uelewa mdogo wa jamii juu ya ufahamu wa ugonjwa huo.

Dr. Ambrose anasema hapa nchini asilimia 15 ya Watanzania wanavinasaba vya ugonjwa huo hivyo juhudi za makusudi zinahitajika kwa jamii kwa kupatiwa elimu kuhusiana na ugonjwa huo.

Anasema asilimia 90 ya watoto hao zaidi ya 10,000 wanaozaliwa kila mwaka hapa nchini wasipopata huduma  stahiki ya matibabu kuna uwezekano wa kupoteza maisha kabla ya kufikisha mwaka wa pili tangu wazaliwe.

Sickle cell ni nini?

Ugonjwa wa siko seli ni ugonjwa wa kurithi unaosababisha mabadiliko yasiyo ya kawaida katika chembechembe nyekundu za damu.

Kwa kawaida chembechembe nyekundu za damu zina umbo la mviringo ambalo huzirahisisha kupita kwenye mishipa midogo ya damu ili kusafirisha hewa safi ya oksijeni katika sehemu mbalimbali za mwili.

Nini kinachosababisha ugonjwa wa sickle cell

Licha ya ugonjwa huo kuwa wa kuruthi, ugonjwa huo hurithiwa katika njia sawa na ambavyo mtu hurithi rangi yake ya mwili au macho, urefu na hivyo basi mtu huzaliwa na ugonjwa huo.

Vinasaba vya siko seli hurithiwa sawasawa kutoka kwa wazazi wote wawili yaani baba na mama.

“Mtu hawezi kupata ugonjwa wa siko seli kwa kuambukizwa kwa njia yeyote ile kama vile kuishi na kushirikiana kwa ukaribu na mtu mwenye ugonjwa huo kwa kula, kucheza au kulala na mtu mwenye siko seli,” anasisitiza.

Anasema lengo la matibabu ya sikoseli ni kupunguza madhara na dalili zitokanazo na ugonjwa, huku kama  vile kutibu na kuzuia maumivu, kuzuia maambukizi ya vimelea vya magonjwa , upungufu wa damu na kiharusi.

Hata hivyo, anasema hakuna tiba moja mahususi kwa wagonjwa wa siko seli hivyo matibabu hutofautiana kutokana na dalili za  mgonjwa mfano kuongezwa damu au maji mwilini na dawa za maumivu.

Tiba ya  seli mundu

Hadi sasa tiba pekee ya ugonjwa huu ni kuwekewa uboho au kupandikizwa kiini kwenye shina la mfupa kitaalamu (bone marrow transplant).

Tiba hii hufanywa kwa kuchukua urojo wa mifupa ya kutoka kwa mtu asiye na  siko seli na hupandikizwa kwenye mifupa ya mgonjwa na hivyo husaidia  kuzalisha chembe za damu zilizo nzima.

Upande mwingine tiba hii licha ya kutokupatikana hapa nchini ni hatarishi na husababisha madhara makubwa kwa wagonjwa na mara nyingine hata kifo.

Matatizo ya kiafya ambayo husababishwa na siko seli

Chembe nyekundu za siko seli hushindwa kupita kwa urahisi katika mishipa midogo ya damu na hivyo kukwama na kuziba mazunguko wa damu na hali hiyo  husababisha maumivu yenye ukali tofauti.

Wagonjwa wa siko seli  hasa watoto hupata maambukizi ya vimelea vya magonjwa mbalimbali kama vichomi, homa ya uti wa mgongo na homa ya ini.

Tatizo lingine, anasema kutokana na chembe nyekundu za siko seli kuwa na muda mfupi wa kuishi, humuweka mgonjwa wa siko  katika hatari ya kupata upungufu mkubwa wa damu.

Kuvimba mikono na miguu mara nyingi huambatana na homa, hali inayosababishwa na chembe nyekundu za  siko seli kukwama na kuziba mzunguko wa damu kwenda kwenye  mikono na miguu.

Matatizo mengi ya kiafya ambayo husababisha ugonjwa huo ni kubanwa na kifua ambapo  mgonjwa  huziba mzunguko wa damu kwenda kwenye mapafu hali inayosababisha matatizo katika njia ya upumuaji.

Vilevile, kukwama na kuziba kwa mzunguko wa damu kwenda kichwani husababisha kiharusi ambacho  huweza kumsababishia mgonjwa ulemavu na wakati mwingine kushindwa kufanya vizuri shuleni.

Nini kifanyike

Naye Pascazia Mazeze ambaye ni mzazi wa Shujaa anasema kuwa juhudi za ziada zinahitajika katika kueliemisha jamii juu ya umuhimu wa kupima afya zao ili kujua kama wana vinasaba vya ugonjwa huo ili kupatiwa matibabu kwa wakati.

Mikoa yenye idadi kubwa ya wagonjwa hapa nchini ni mikoa ya pwani,  kanda ya ziwa na mikao ya kanda ya kati.

Mikoa hiyo ni Tanga, Dar es Salaam, Pwani , Mara, Mwanza, Bukoba, Shinyanga, Tabora na Dodoma.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.