ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, June 10, 2018

NI GORMAHIA MABINGWA SPORTSPESA


KWA mara ya pili mfululizo, Gor Mahia ya Kenya imebeba taji la SportPesa Super Cup baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba SC ya Dar es Salaam, Tanzania.

Mashujaa wa Gor Mahia leo wameendelekuwa wanasoka wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere na Jaqcues Tuyisenge waliofunga mabao hayo, moja kila kipindi na kurudia mafanikio ya mwaka jana mjini Dar es Salaam wakiwafunga mahasimu wao wa Kenya, AFC Leopard 3-0 na kutwaa taji hilo. 
Kagere alianza kufunga bao zuri dakika ya sita akimalizia kazi nzuri ya George Odhiambo ‘Blackberry’ kabla ya Tuyisenge kufunga la pili akimalizia krosi ya Humphrey Mieno dakika ya 54.


Simba SC ilicheza ovyo kipindi cha kwanza na kuzidiwa kabisa na Gor Mahia, lakini kipindi cha pili ilibadilika na kutulia kujaribu kucheza soka ya maelewano, ingawa tayari wapinzani wao walikuwa wamekwishajipanga kuulinda ushindi wao.

Kwa ushindi huo, Gor Mahia inayofundishwa na kocha wa zamani wa Simba, Muingereza Dylan Kerr pamoja na kuzawadiwa dola za Kimarekani 30,000 lakini watakwenda kucheza na klabu ya Everton Uwanja wa Goodison Park mjini Liverpool, England. 


Simba SC watajipatia dola za Kimarekani 10,000, Singida United waliomaliza nafasi ya tatu kwa kuifunga Kakamega Homeboyz kwa penalty 5-1 baada ya sare ya 1-1 watapatiwa dola 7, 500 na wa washindi wa nne watapewa dola 5,000.


Kariobangi Sharks ya Kenya, Yanga ya Tanzania Bara na JKU ya Zanzibar kila moja itapata dola 2,500 baada ya kutolewa hatua ya kwanza ya mashindano. 


Shaaban Odhoji amekuwa kipa bora na Kagere, wote wachezaji wa Gor Mahia inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa Kundi moja na Yanga, amekuwa mfungaji bora kwa mabao yake manne.


Kikosi cha Gor Mahia kilikuwa; Shaaban Odhoji, Harun Shakava, Godfrey Walusimbi, Pjilemon Otieno, Ernest Wendo, Francis Kahata, George Odhiambo/Juma dk82, Humphrey Mieno/Innocent Wafula dk67, Meddie Kagere/Bernard Omondi dk91, Jaqcues Tuyisenge/Bernard Ondiek dk93 na Joash Onyango.


Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe/Ally Shomari dk68, Erasto Nyoni, Paul Bukaba, Yussuf Mlipili/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk59, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Mohammed Ibrahim dk89, Muzamil Yassin, Adam Salamba, Rashid Mohammed na Rashid Juma/Marcel Kaheza dk57.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.