ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, January 18, 2018

MHE BITEKO AMUAGIZA KAMISHNA WA MADINI KANDA YA KUSINI KUANZISHA OFISI YA MADINI WILAYANI RUANGWA

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza na wachimbaji wadogo kwenye mkutano wa hadhara katika kitongoji cha Namungo Kata ya Megembekenyela Wilaya ya Ruangwa wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Lindi, Leo 8 Januari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal
Wachimbaji wadogo wa dhahabu katika kitongoji cha Namungo Kata ya Megembekenyela Wilaya ya Ruangwa wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko kwenye mkutano wa hadhara wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Lindi, Leo 8 Januari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akikagua mgodi wa kampuni ya uchimbaji dhahabu na Green Garnet ya Gemini Exploration & Mining Services (GEMS) kabla ya kuzungumza na wachimbaji wadogo kwenye mkutano wa hadhara katika kitongoji cha Namungo Kata ya Megembekenyela Wilaya ya Ruangwa wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Lindi, Leo 8 Januari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akikagua baadhi ya maeneo ya uzalishaji madini ya dhababu kwenye kampuni ya uchimbaji dhahabu na Green Garnet ya Gemini Exploration & Mining Services (GEMS) wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Lindi, Leo 8 Januari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza na wachimbaji wadogo kwenye mkutano wa hadhara katika kitongoji cha Namungo Kata ya Megembekenyela Wilaya ya Ruangwa wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Lindi, Leo 8 Januari 2018.

Na Mathias Canal, Lindi

Kamishna msaidizi wa madini kanda ya kusini Ndg Mayigi Makorobela ameagizwa kuanzisha haraka ofisi ya Madini Wilayani Ruangwa ikiwemo kupeleka wataalamu ili kurahisisha huduma za kitaalamu kwa wachimbaji wadogo ikiwemo elimu ya usalama kazini.

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko ametoa agizo hilo leo tarehe 18 Januari 2018 wakati akizungumza na wachimbaji wadogo waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara katika kitongoji cha Namungo Kata ya Megembekenyela wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Lindi.

Alisema kuwa Wizara ya Madini imeamua kuanzisha ofisi hiyo kutokana na maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa aliyoyatoa hivi karibuni wakati alipokuwa ziarani Mkoani humo ambapo alibaini kuwa wachimbaji wadogo wanapata kadhia kubwa kutokana na umbali wa ofisi kwani wanalazimika kutumia zaidi ya kilomita 45 kuzifikia ofisi za madini zilizopo Wilayani Nachingwea.

Alisema kuwa Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa anawapenda wachimbaji wadogo nchini ambao hata hivyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu alibainisha kukusudia kuwanufanisha watanzania kupitia rasilimali zao ikiwemo madini.

"Mhe Rais Magufuli anataka wananchi wote wanaoishi karibu na mgodi kunufaika na rasilimali zao, nyote mtakuwa mashahidi, tangu nchi iliporuhusu uchimbaji wa madini hakuna manufaa ya moja kwa moja kwa watanzania badala yake madini yamekuwa yakinufaisha mataifa mengine ambayo baadaye tunayapigia magoti kuyaomba msaada" Alikaririwa Mhe Biteko huku akipigiwa makofi na wananchi waliohudhuria katika mkutano huo

Mhe Biteko alisema kuwa lengo la kuanzisha ofisi ya madini katika Wilayani hiyo ya Ruangwa ni kuwarahisishia wachimbaji kuwa na jukumu moja la kuchimba na kuuza rasilimali wanazozipata kwani watakuwa sehemu ya kuchagiza maendeleo sambamba na kuinufaisha serikali kutokana na ulipaji kodi.

Aliwasihi wachimbaji hao kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya Tano chini ya Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli kwani tangu ameingia madarakani katika kipindi kifupi ameimarisha nidhamu mpya kwa kila mtanzania na usimamizi madhubuti wa rasilimali za Taifa.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko ameipongeza kampuni ya uchimbaji dhahabu na Green Garnet ya Gemini Exploration & Mining Services (GEMS) ambayo ni kampuni ya wazawa kwa kufanya kazi kwa kufuata vyema sheria na taratibu za uchimbaji.

Alisema kuwa kampuni zingine zinapaswa kujifunza kwa kampuni hiyo ya GEMS kutokana kulipa kodi mbalimbali kwa uwazi na ushiriki wa shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kusaidia sekta ya afya, Maji, sekta ya elimu sambamba na michezo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.