ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, December 14, 2017

WALIOSHINDWA KUENDELEZA MAENEO UCHIMBAJI WA JASI KUFUTIWA LESENI

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akitembelea Kiwanda cha kuzalisha Chaki cha Dobercolor kilichopo katika Kijiji cha Majengo, Itigi. Kulia ni Mlinzi Mkuu wa Kiwanda hicho, John Kitika akielekeza eneo linalotumiwa kwa ajili ya kuanikia Chaki (halionekani pichani). Kuhoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Pius Luhende.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa tatu kushoto) akitazama mtambo wa kusaga Madini ya Jasi na kisha unga wake (gypsum powder) hutumika kutengeneza Chaki katika kiwanda cha Dobercolor kilichopo katika Kijiji cha Majengo, Itigi.

Eneo la kuchomea Madini ya Jasi kabla hayajasagwa na kuwa unga (Gypsum powder) katika Kiwanda cha Kusaga Mawe ya Jasi cha RSR kinachomilikiwa na Mtanzania, Rashid Rashid kilichopo katika Kijiji cha Sanjaranda, Itigi.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa pili kushoto) akitazama hatua ya uchomaji wa Madini ya Jasi kwenye kiwanda cha kampuni ya mzawa cha RSR kinachomilikiwa na Rashid Rashid (kushoto) kilichopo katika Kijiji cha Sanjaranda, Itigi kabla ya kusagwa kuwa unga (Gypsum powder) na baadaye kusafirishwa hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kuuzwa.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (aliyesimama) akizungumza na Wafanyakazi, Wachimbaji na Wafanyabiashara wa Madini ya Jasi (hawapo pichani) wakati wa ziara yake Itigi Mkoani Singida. Kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Pius Luhende.


Baadhi ya Wafanyakazi wa Machimbo ya Jasi, Wachimbaji na Wafanyabiashara wa Madini ya Jasi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) wakati wa ziara yake Itigi Mkoani Singida.


WALIOSHINDWA KUCHIMBA JASI KUFUTIWA LESENI

Serikali imesema Wachimbaji wa Madini ya Jasi walioshindwa kuendeleza maeneo yao sheria itachukua mkondo wake ikiwemo kufutiwa leseni zao na maeneo yao kumilikishwa Wachimbaji wengine wenye nia ya kufanya uchimbaji.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alisema hayo Desemba 11, 2017 wakati wa ziara yake kwenye machimbo ya Jasi Wilayani Manyoni, Mkoani Singida.

Nyongo alitoa kauli hiyo kufuatia malalamiko ya baadhi ya wachimbaji wa madini hayo ya kukosa maeneo ya kutosha kufanya shughuli za uchimbaji husika na huku maeneo mengi yakiwa chini ya umiliki wa watu wasioyaendeleza.

Alisema leseni zilitolewa ili uchimbaji ufanyike na kwakua waliopewa leseni wameshindwa kuendeleza maeneo husika, sheria itachukua mkondo wake ikiwemo kuwaandikia hati ya makosa (default notice) na endapo watashindwa kutekeleza maelekezo watakayopewa, leseni za uchimbaji wa madini husika zitafutwa na maeneo yao kumilikishwa wengine.

Alimuagiza Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati, Singida, Sosthenes Massola kufuatilia suala hilo ili hatua stahiki zichukuliwe mapema iwezekanavyo. 

Vilevile, Naibu Waziri Nyongo alitoa onyo kwa wachimbaji wanaoshindwa kulipa fidia ya umiliki wa ardhi kwenye maeneo yaliyokuwa yanamilikiwa na watu wengine wakiwemo wakulima. 

Alitoa onyo hilo kufuatia malalamiko kutoka kwa wananchi ambao walisema baadhi ya wachimbaji wa Madini ya Jasi walianza kufanya shughuli zao za uchimbaji bila ya kukubaliana na wenyeji waliowakuta kwenye maeneo hayo jambo ambalo walisema limewaletea usumbufu na kuwarudisha nyuma kimaendeleo.

"Sisi wakulima tunanyasika, mchimbaji anakuja na kuanza kuchimba bila makubaliano yoyote," alisema Hamis Said ambaye aliwatuhumu wachimbaji kuvamia eneo lake bila ridhaa yake.

Naye Hamisa Rashid ambaye alijitambulisha kuwa ni mkulima alishauri kwamba wachimbaji kabla hawajaanza shughuli zao wawatafutie maeneo mbadala ili wakaendeleze shughuli zao za kilimo.

Naibu Waziri Nyongo alisema haiwezekani mchimbaji apewe leseni hali ya kuwa hana uwezo wa kulipa fidia kwa wananchi ambao amewakuta katika eneo analotaraji kufanya shughuli za uchimbaji.

"Hii ni Serikali inayojali wanyonge, hatuwezi kumvumilia mtu ambaye ananyanyasa wananchi; kama huna uwezo wa kulipa fidia usiombe leseni," alisisitiza Nyongo.

Alimuagiza Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda husika na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Manyoni kukutana na wananchi wenye malalamiko ili hatua stahiki zichukuliwe na haki itendeke.

"Taratibu za kumilikisha watu maeneo zifuatwe ikiwemo suala la ulipaji wa fidia," aliagiza Waziri Nyongo.

Aidha, Waziri Nyongo alimuagiza Kamishna wa Madini kutenga maeneo zaidi kwa wananchi wenye nia ya kuchimba Madini ya Jasi.

Naibu Waziri Nyongo yupo Mkoani Singida kwa ziara ya siku Tatu ya kutembelea shughuli za uchimbaji wa Madini mkoani humo na kuzungumza na wachimbaji ili kubaini changamoto zinazowakabili kwa lengo la kutafutia ufumbuzi.
-Mwisho-

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.