ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, August 12, 2017

NI UHURU KENYETA TENA.

HATIMAYE na baada ya mjadala mkubwa kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 8 Agosti, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) jana usiku ilimtangaza Uhuru Kenyatta kuwa ndiye aliyeibuka na ushindi wa kiti cha rais wa nchi hiyo. 

Tangazo la ushindi wa Uhuru Kenyatta lilitolewa huku kambi ya upinzani ya muungano wa NASA ukikituhumu chama tawala cha Jubilee kuwa kimefanya udanganyifu na kuiba kura. Kinara wa chama hicho Raila Odinga amesema kuwa, kuongoza kwa Uhuru Kenyatta katika matokeo ya uchaguzi wa rais kulitiliwa shaka tangu mwanzoni mwa kutangazwa matokeo ya uchauzi huo na kwamba hakukuoana na ripoti zilizotolewa na maafisa wa chama chake.

Matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa IEBC Bw. Wafula Chebukati yameonyesha kuwa Uhuru Kenyatta aliyegombea kwa tiketi ya chama cha Jubilee alipata ushindi baada ya kujizolea kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27 ya kura zote huku mshindani wake mkuu Raila Odinga wa muungano wa upinzani wa NASA akipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74 ya kura zote. 

Mwenyekiti wa IEBC Bw. Wafula Chebukati 
Kwa matokeo hayo, Rais Uhuru Kenyatta wa mrengo wa Jubilee na Naibu wake William Ruto wataongoza tena Jamhuri ya Kenya kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Baada tu ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Kenya, mamia ya wafuasi wa chama cha NASA walimiminika mitaani wakiandamana kupinga matokeo hayo. Ripoti kutoka Nairobi zinaeleza kuwa polisi wamelazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kudhibiti malalamiko ya kisiasa yaliyoibuka katika mji wa Kisumu magharibimwa Kenya iliko ngome kuu ya upinzani, eneo la mabanda la Mathare katika mji mkuu wa nchi hiyo, Nairobi, Siaya, Homa Bay and Migori.


Raila Odinga ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa Uhuru kenyatta katika uchaguzi wa mwaka huu wa rais aligombea kiti hicho kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa mwaka 1997 na hii ilikuwa mara ya nne kwa mwanasiasa huyo kuchuana kwa ajili ya kuingia Ikulu ya Nairobi bila ya mafanikio. Katika uchaguzi wa mwaka 2007 Raila Odinga na mrengo wake walidai kwamba, kulifanyika udanganyifu mkubwa katika matokeo ya uchaguzi, suala mbalo lilizusha machafuko makubwa kote nchini Kenya.

 Zaidi ya watu 1200 waliuawa katika machafuko hayo na malaki ya wengine walilazimika kuwa wakimbizi. Wakati huo Odinga aliwasilisha malalamiko mahakamani ingawa mara hii NASA imesisitiza kuwa, haitaelekea mahakamani kukata rufaa na hadi sasa haijulikani iwapo itabadilisha mawazo yake na kutaka haki katika idara ya mahakama au la. 

Kinara wa Nasa, Raila Odinga
Madai ya kufanyika udanganyifu katika uchaguzi wa Kenya yametolewa huku wasimamizi wa kimataifa waliofuatilia kwa karibu zoezi hilo wakisema umefanyika kwa uhuru, uwazi na uadilifu. Aghalabu ya timu za waangalizi wa uchaguzi huo zikiwemo za Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Kieneo ya IGAD zinasema kuwa, uchaguzi huo ulikuwa huru, wa haki na wa wazi.


Akihutubia mara baada ya kutangazwa mshindi na kukabidhiwa cheti cha kuchaguliwa, Rais mteule Uhuru Kenyatta amewaomba Wakenya wadumishe amani na kushirikiana na serikali yake kukuza taifa hilo. Vilevile amemshauri kinara wa Nasa, Raila Odinga kwamba uchaguzi huo ulikuwa mashindano tu na haufai kuleta chuki.


Matamshi hayo ya Uhuru Kenyatta yanapata maana kwa kuzingatia muundo wa kikabila wa siasa za Kenya ambao umekuwa na nafasi na ushawishi mkubwa katika masuala muhimu kama chaguzi za rais Bunge la kadhalika.

Uhuru Kenyatta
Alaa kulli hal, Uhuru Kenyatta ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa Rais wa Kenya wakati nchi hiyo ikikabiliwa na changamoto kadhaa, kubwa zaidi ikiwa ni tishio la kundi la kigaidi la al Shabab kwa usalama na maisha ya raia wa nchi hiyo. Mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi hilo pia yameathiri sana sekta ya utalii ambayo inahesabiwa kuwa miongozi mwa nguzo kuu za uchumi wa Kenya.


Changamoto nyingine kubwa ni maradhi ya malaria, virusi vya Ukimwi, kifua kikuu na matatizo ya kichumi ambayo rais mteule Uhuru Kenyatta aliahidi kukabiliana nayo katika kampeni zake za uchaguzi.

Inatarajiwa kuwa Wakenya wa kambi zote wataikitia wito wa busara na mantiki na kujiepusha na machafuko, ghasia na chuki za kikabila ambazo jeraha na maumivu yake yangali yanahisika baada ya machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.