ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, July 17, 2017

WANAOCHOCHEA SIASA KUPITIA WHATSAPP NCHINI KENYA WAONYWA.


TUME ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa nchini Kenya imetangaza kuwa, inachunguza makundi 21 ya Whatsapp yanayosambaza ujumbe wa chuki na uchochezi kuelekea uchaguzi mkuu mwezi ujao katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Mwenyekiti wa tume hiyo Francis Ole Kaparo amesema kuwa, tayari wameanza mchakato wa kuwahoji wamiliki wa makundi hayo ya Whatsapp kutoka kaunti 21 nchini humo.

Kaparo amesema kwamba, tume yake itawafungulia mashtaka wale wote wanaochochea au kutuma ujumbe wa chuki kwa lengo la kuzua machafuko kabla na baada ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika tarehe nane mwezi ujao. Serikali imetangaza kuwa, haitakubali watumiaji wa mitandao kuvuruga amani kwa kueneza habari za uzushi.

Wakenya wametakiwa kutumia vyema mitando ya kijamii na kujiepusha na uchochezi.
Wakati huo huo, Francis Wangusi, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya, amevionya vyombo vya habari nchini Kenya dhidi ya kutangaza matokeo ya uchaguzi kabla ya tume ya kusimamia uchaguzi na mipaka kufanya hivyo.

Kwa upande wa vyombo vya usalama, inspekta jenerali wa polisi Joseph Boinet amesema polisi watatumia nguvu kiasi kuwakabili wachochezi wa ghasia iwapo fujo zitazuka. Onyo lake linakumbusha matukio ya mwaka 2007/08 wakati polisi walipotuhumiwa kuhusika na  mauaji ya kiholela walipokuwa wakikabiliana na ghasia.

Huku hayo yakiripotiwa, wasiwasi umeendelea kutanda katika Kaunti ya Lamu kutokana na kuongezeka mashambulio ya wanamgambo wa kundi la al-Shabab katika siku za hivi karibuni. Sambamba na hayo, kampeni za uchaguzi zimeendelea kupambana moto huku vyama vikuu vya Jubilee na Muungano wa NASA vikiendelea kupiga debe la kuomba kura.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.