ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, July 5, 2017

TAIFA STARS YATOKA KIUME NUSU: FAINALI YAPIGWA 4 - 2 NA ZAMBIA.

TANZANIA itawania nafasi ya tatu katika Kombe la COSAFA Castle baada ya leo kufungwa mabao 4-2 na Zambia katika mchezo wa Nusu Fainali Uwanja wa Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini.

Zambia inatangulia fainali na Julai 9 itamenyana na mshindi kati ya Lesotho na Zimbabwe zinazomenyana kuanzia Saa 2:00 usiku wa leo.

Mkongwe Erasto Nyoni alianza kuifungia Taifa Stars kwa shuti zuri la mpira wa adhabu dakika ya 14 na bao hilo lilikaribia kudumu hadi kipindi cha pili, kama si Zambia kupata mabao mawili ya haraka haraka mwishoni mwa kipindi hicho.

Brian Mwila alianza kuifungia Chipolopolo bao la kusawazisha dakika yaa 44, kabla ya Justin Shonga kufunga la pili dakika ya 45 na Zambia ikaenda kupumzika inaongoza 2-1.

Jackson Chirwa akaifungia Zambia bao la tatu kwa mkwaju wa penalti dakika ya 55, baada ya mpira kumgonga mkononi kwa nyuma beki wa kushoto, Gardiel Michael na la nne dakika 67 kwa shuti la mpira wa adhabu.

Simon Msuva akaipunguzia macungu Tanzania kwa kufunga bao la pili dakika ya 84 akimalizia mpira uliorudi baada yaa krosi ya Gardiel Michael.  Taifa Stars wakaongeza kasi ya mashambulizi baada ya bao hilo, lakini bahati mbaya ‘muda haukuruhusu’.

Taifa Stars inapoteza mechi ya kwanza chini ya kocha Salum Mayanga aliyeanza kazi Machi mwaka huu akimpokea Charles Boniface Mkwasa, baada ya kucheza mechi saba bila kupoteza, ikishinda tatu na kutoa sare nne.

Zambia leo imeifunga Tanzania kwa mara ya 17 katika mechi 31 walizokutana, wakifungwa tano  na sare tisa.

Tanzania ilianzia hatua ya mchujo kwenye Kundi A ambako iliongoza kwa pointi zake tano sawa na Angola baada ya sare mbili 0-0 na Angola, 1-1 na Mauritius na ushindi wa 2-0 dhidi ya Malawi, hivyo kutengeneza wastani mzuri wa mabao na kuwapiku wapinzani kusonga Nusu Fainali.

Zambia yenyewe ilianzia moja kwa moja hatua ya Robo Fainali sawa na Afrika Kusini, Botswana,
Namibia, Lesotho na Swaziland huku Zimbabwe ikiongoza Kundi B. Lesotho na Zimbabwe zitamenyana katika Nusu Fainali ya pili Saa 2:00 usiku.

Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gardiel Michael, Abdi Banda/Nurdin Chona dk69, Salim Mbonde, Himid Mao, Erasto Nyoni/Raphael Daudi dk45, Muamil Yassin, Elias Maguri/Thomas Ulimwengu dk80, Simon Msuva na Shiza Kichuya.

Zambia; Alan Chibwe, Lawrence Chungu, Adrian Chama, Diamond Chikwekwe/Lubinda Mundia dk61, Justin Shonga/Godfrey Ngwenya dk90, Donashano Malama, Mike Katiba, Jackson Chirwa, Webster Mulenga, Isaac Shamujompa na Brian Mwila/Chitia Mususu dk82.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.