ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, June 19, 2017

WAZIRI - MARUFUKU KUSAJILI SHULE MPYA BILA KUWA NA VIWANJA VYA MICHEZO.




Na Atley Kuni- Mwanza
Serikali imesema ni marufuku kwa shule ambayo itakuwa haina viwanja vya michezo kupatiwa kibali cha kufungua shule ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Elimu namba 25 ya mwaka 1978.

Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Masindano ya kwashule za msingi nchini UMITASHUMTA mkoani Mwanza, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMO) Mh. George Simbachawene, amemuagiza Kamishna wa Elimu nchini, kutozipatia vibali shule zinazo hitaji kufunguliwa endapo zitakuwa hazina viwanja vya michezo.

Simbachawene, amesema kutokana na sheria ya Elimu namba 25 ya mwaka 1978, ambayo inataka kila shule inapofunguliwa lazima iwe na viwanja visivyo pungua vitano hivyo nilazima hili lizingatiwe, “nichukue nafasi hii kumuagiza kamishna wa Elimu kuanzia sasa asisajili shule yeyote ile ambayo itakuwa haina Viwanja vya michezo, kwani bila kufanya hivyo azma yetu yakuinua michezo nchini haiwezi kutimia” alisema.

Mbali na kutoa maagizo hayo waziri Simbachawene, ameziagiza pia halmashauri na wilaya kote nchini kutenga sehemu ya mapato yao ya  ndani kwaajili ya kitengo cha michezo, huku akizihimiza kuweka katika bajeti ijayo ya serikali fedha kwenye vifungu vinavyo husiana na michezo na kuonya kuwa endapo Halmashauri itashindwa kufanya hivyo basi yeye kama waziri mwenye dhamana hatakubali ipite.

Amesema Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 sehemu ya (61) inatambua suala la Michezo lakini pia Sera ya Elimu ya Mwaka 1995, hivyo kama Serikali lazima waweke kipaumbele katika suala zima la michezo.

Ameongeza kuwa, Msingi wa Michezo nchini ni michezo ya UMITASHUMTA NA UMISETA ndio Dira ya timu zetu za Taifa, “Tukiwaandaa vijana wetu vizuri na kutokana kaulimbiu hii ya masula ya viwanda, hatuna wasiwasi kuwa hawa ndio viwanda vyenyewe, mchezaji mmoja aliyefikia viwango vya kimataifa huweza kugharamia hata bajeti ya nchi” alisema Simbachawene.

Katika hatua nyingine Simbachawene, amewaagiza makatibu Tawala kote nchini, kusimamia suala la taaluma na michezo, amesema hakuna taaluma bila Michezo na Hakuna michezo bila Taaluma kwa mantiki hiyo lazima nidhamu ya hali ya juu iongezwe miongoni mwa vijana na wanamichezo kwa ujumla.  

Naye  Mkurugenzi wa Michezo nchini kutoka Wizara ya Habari, Michezo Sanaa na Wasanii Dkt. Yusuph Singo amesema Tayari Wadau Mbali mbali wa Michezo wakiongozwa na Chama cha Mpira wa Miguu na Riadha wapo Mkoani Mwanza kwaajili ya Kuangalia Vipaji kwa ajili ya Timu mbali mbali za Taifa lakini pia vilabu vyao.

Aidha amesema kuwa wizara ipo katika Mazungumzo na Timu Manchester City kupitia wakala wao wa TECHNO kwaajili yakuchukuwa Vijana wapatao kumi kutoka Tanzania kwaajili yakuwaendeleza kimichezo.

Awali akimkaribisha Mgeni rasmi, Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella, aliishukuru serikali kwakuichagua Mwanza kuwa mwenyeji wa mashindano hayo huku akiomba kwa mwaka ujao mashindano hayo kufanyika tena mkoani humo, kutokana na madhari mazuri lakini pia ubora wa viwanja na hali ya ulinzi na usalama inayotamalaki katika mkoa huo, “Mh. Waziri mimi niombe tu, haya mashindando katika mwaka ujao myalete tena Mwanza sisi tupo tayari, huo ndio mtazamo wangu lakini pia wenzangu wataniunga mkono” alisema Mongella.

Mashindano ya shule za msingi (UMITASHUMTA) ya 2017 ni mashindano ya 22 ambapo yanashirikisha wanamichezo wapatao 2522 kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.