ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, June 10, 2017

WATU 14 WAUAWA SOMALIA BAADA YA WANAJESHI KUPIGANA WAKIGOMBANIA CHAKULA.

Kwa uchache watu 14 wameuawa kusini magharibi mwa Somalia wengi wao wakiwa ni raia baada ya kuzuka mapigano baina ya wanajeshi wakigombea chakula cha misaada.

Taarifa zinaeleza kuwa, mapigano hayo ya kugombania chakula ambayo mbali na kusababisha mauaji ya watu 14 yamepelekea pia makumi ya watu kujeruhiwa yalitokea katika mji wa Baidoa ambao una makumi ya maelfu ya raia wanaohitajia misaada ya chakula kutokana na kukabiliwa na ukame na uhaba mkubwa wa chakula.

Mapigano hayo yalizuka baada ya baadhi ya wanajeshi kujaribu kuiba chakula cha misaada ambapo kundi jingine la wanajeshi lilikuja na kuwazuia wenzao hao.

Mohammed Ahmed mmoja wa maafisa katika hospitali kuu ya Baidoa amewaambia waandishi wa habari kwamba, baadhi ya majeruhi wa tukio hilo hali zao ni mbaya, inagawa wanaendelea kupata matibabu.

Wanawake wa Somalia wakiwa katika foleni ya kusubiria chakula cha msaada
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa nchi ya Somalia inakabiliwa na ukame na hivyo kuiongezea matatizo nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inayokabiliwa pia na tatizo la njaa na ukosefu wa amani na usalama.
 
Mbali na majanga hayo ya kimaumbile, Somalia inakabiliwa pia  na harakati za kundi la kigaidi la al-Shabaab ambalo limekuwa likifanya mashambulizi ya kigaidi nchini humo.

Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, nusu ya raia wa Somalia ambao ni karibu watu milioni sita na laki mbili wanahitajia msaada wa haraka huku watoto laki tatu na elfu 63 wakikabiliwa na hali mbaya sana ya utapiamlo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.