BARAZA la Habari (MCT), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC)
na Umoja wa Vilabu vya Habari Tanzania (UTPC) vinakusudia kufungua kesi
kwenye mahakama kupinga uamuzi wa serikali wa kulifunga gazeti la Mawio.
Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
ilitangaza kulifunga gazeti hilo kwa miezi 24 kuanzia Alhamisi
iliyopita, kwa kuchapisha taarifa zinazowahusisha marais wastaafu
Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete kwenye sakata la mikataba mibovu ya
madini.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, wadau hao
walisema hawajaridhika na hatua zilizochukuliwa na serikali katika
kulifunga gazeti hilo kwa sababu ni kinyume cha mabadiliko ya Sheria ya
Huduma ya Habari ya mwaka 2016.
Kaimu Katibu Mtendaji wa MCT, Pili Mtambalike, alisema kimsingi sheria
hiyo haimpi waziri mamlaka ya kutoa adhabu kama aliyoitoa dhidi ya
gazeti hilo.
Alisema hatua iliyochukuliwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, inalenga kuvinyima uhuru vyombo vya
habari nchini.
Mtambalike alisema ni vema serikali kupitia Waziri Mwakyembe ikakaa
chini na kutafakari upya na pia kufanya mazungumzo na uongozi wa gazeti
hilo ili kutengua adhabu aliyoitoa.
"Serikali itengue uamuzi wake wa kulifungia gazeti la Mawio kwani
unaenda kinyume cha Katiba pamoja na Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka
2016 kwa kuwa haimpi waziri mamlaka ya kutoa adhabu kama hiyo,"
alisema.Alisema zaidi: "Kwa sababu hakuna sehemu ya kupeleka rufani
dhidi ya uamuzi wa waziri katika Sheria ya Huduma za Habari, endapo
hakutakuwa na mazungumzo kati ya gazeti husika na waziri, sisi
tutakwenda mahakamani kwa kushirikiano na Mawio kuonyesha haki
zilizokiukwa juu ya hatua hiyo.
"Ikumbukwe kwamba vyombo vya habari, yakiwamo magazeti, hufanya shughuli
zao kwa mujibu wa sheria na Katiba inasema wazi chini ya ibara ya 18
kwamba Watanzania wote wana haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari na
maoni kwa njia yoyote, hivyo kwa mujibu wa sheria na vipengele hivyo
vya Katiba, serikali inapaswa kuondoa marufuku yake dhidi ya gazeti la
Mawio."
Naye Mkurugenzi wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisema sehemu ya sheria
ambayo waziri alitumia kulifunga gazeti hilo haina uhusiano na sehemu
ambayo imewekwa kosa.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.