Na Dkt. Hamisi Kigwangalla.
Kila
siku nashuhudia wananchi wenzangu wakikalamika. Natamani kujibu.
Naacha. Natamani kuwakumbusha wananchi wenzangu. Naacha. Nasema mbona
sisi ni wepesi kusahau? Natamani kuwakumbusha wabunge wenzangu. Naacha.
Nasema na mimi sasa nipo kwenye Serikali. Ni mtunga sera, ni mfanya
maamuzi, nikisema watasema huyu ni 'Naibu Waziri'. Lakini kiukweli nina
hamu na shauku ya kuzungumza na wananchi wenzangu. Nami nitoe yangu ya
moyoni. Kama mwananchi mwingine yeyote yule tu. Nina haki hiyo. Na mimi
haki yangu inalindwa na katiba na sheria za nchi yetu.
Leo
nimeona acha nipumue kidogo. Niseme. Niuvue userikali wangu. Niseme
kama mwananchi mwingine yeyote yule. Nianze kwa kuweka wazi kabisa hapa,
kwamba; haya ni yangu. Si ya Serikali.
Serikali
ni ya Rais Magufuli, tumempa dhamana, ndiyo. Hili halibishaniwi.
Tumempa kazi, ndiyo. Hili pia halibishaniwi. Lakini kazi hii
anaifanyaje? Tunazijua changamoto anazokumbana nazo? Je, ana nia ya
kuzitatua? Ni maswali ambayo yanastahili majibu. Kwenye makala hii
nitajaribu kuyafafanua kidogo kwa mtazamo wangu kadri nitakavyojaaliwa.
Pamoja
na kumpa dhamana Rais wetu, ni lazima tufahamu kuwa na sisi tuna wajibu
wa kutimiza kwa Taifa letu. Tuna kazi ya kufanya kumsaidia Rais wetu
kubeba mzigo wa kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kijamii kwenye Taifa
letu. Tusimuachie huu mzigo peke yake. Tuubebe sote.
Nchi
ina changamoto nyingi sana, siyo kwamba Rais ama Serikali yake
haizifahamu ama haina nia ya kuzitatua, ama Rais Magufuli amesinzia, ama
anastarehe; kila siku anahangaika kukuna kichwa, usiku na mchana
kuzitafutia ufumbuzi. Nadhani hili halina ubishani sana kwa mpenda
kweli. Binafsi, sina shaka kabisa juu ya uwepo wa nia thabiti ya kuleta
mapinduzi. Sina.
Kwenye
biashara ya kujenga nchi changamoto haziishi siku moja. Ukimaliza moja,
nyingine inaibuka, na nyingine zinazaliwa kutokana na majawabu ya
changamoto uliyoitatua.
Juzi
juzi hapa nilisema kuhusu mfumo wa afya wa nchi kubwa kama ya Marekani
kuwa na changamoto ya kuwabagua watu maskini na wale wa tabaka la kati
na kwamba unajenga matabaka makubwa sana yanayowanyima fursa sawa baadhi
ya watu kwenye Jamii. Na kwamba ObamaCare inajaribu kutoa majibu
yanayolenga kuleta usawa kwa kuwabana wenye kipato cha juu ili
kuwahudumia wenye kipato cha chini. Tayari imeonekana kuwa kuna
changamoto za kuwakamua zaidi watu wa daraja la kati, badala ya wale wa
tabaka la juu kama 'design' na muundo wa awali ulivyolenga, kwa
kuwatwisha mzigo wa watu maskini, na kwamba mpango huu kwa baadaye
hautohimilika. Bado wanaendelea kubishana! Juzi tumeshuhudia Rais Trump
amekwama kwenye jaribio la kuurekebisha. Kazi ya kutatua changamoto ipo
na inaendelea kwenye Taifa kubwa la Marekani lenye miaka zaidi ya 200 ya
demokrasia.
Mfano,
tazama changamoto mpya iliyokuja na sera ya CCM kutoa elimu bure mpaka
kidato cha nne. Tamko hili la kisera limeleta changamoto nyingi za
kiutekelezaji. Kwanza, limeleta urahisi kwa familia nyingi kuona hakuna
sababu ya watoto wao, hata mmoja, kukosa elimu hii ya msingi. Wakati
tunapitisha sera hii hatukujua kuwa kuna watoto wengi kiasi hiki
tunachoshuhudia sasa walikuwa wakikosa fursa (missed opportunity) ya
elimu kwa sababu ya vigharama vidogo vidogo.
Tumeondoa
gharama hizi tumekutana na ongezeko kubwa la watoto kuandikishwa shule.
Mlipuko wa wanafunzi kuingia darasa la kwanza kwenye shule za msingi
kwa wingi umezaa changamoto mpya za upungufu wa madawati, vyumba vya
madarasa, idadi ya matundu ya vyoo, idadi ya walimu nk. Wakati
tukumbukeni vizuri kuwa juzi tu hapa Serikali ilikuwa inaajiri walimu
kwa kipaumbele cha juu kabisa kwa miaka mitano mfululizo, ambapo walimu
wote waliohitimu waliajiriwa!
Uchumi
wetu unakua kwa kasi nzuri, kama ni ndege ndiyo inaongeza spidi ili
ipate nguvu ya kupaa; bado uchumi hauna uwezo wa kuhimili mahitaji yetu
'yote' ya matumizi ya kila siku kama tunavyotamani, achilia mbali ya
kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kadri tunavyodiriki kuota
ndoto zetu. Mfano: Kwenye ajira bajeti ya watumishi (wage bill)
inaongezeka kila siku. Hili tu ni hitajio kubwa na nyeti sana la uchumi
wetu.
Zamani
nilipokuwa Mbunge - bila userikali, kilichokuwa kinanikera ni kwamba,
pamoja na changamoto tulizonazo watu wengine walikuwa wanaishi kama wako
peponi na wengine wanaishi kama wako motoni, hawa wa peponi walifika
huko kwa wizi, rushwa, ufisadi, ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi
za umma, siyo kwa uchapakazi wala ubunifu. Tena bila huruma kwa
waliokuwa wakiishi kama vile wapo motoni. Huku wakiwa na dhamana ya
kuwaondoa motoni wananchi wenzetu waliobaki huko!
Leo
Rais JPM anakosolewa kwa kubana mianya ya rushwa, wizi, ubadhirifu wa
mali ya umma, matumizi mabaya ya madaraka na uchumi wa ujanja ujanja,
mambo ambayo nakumbuka mimi na wenzangu kwenye bunge la 10 tuliyapigia
kelele kwa nguvu sana, tena kwa uzalendo wa hali ya juu na bila hata
kuogopa kuwa tunapowashughulikia hawa ndugu wa peponi tunashusha imani
ya wananchi kwa chama chetu pia.
Sisi
tuliamini kwamba hawa ni lazima tushughulike nao. Tuwaondoe ili
kukisafisha Chama. Tulikuwa wachache sana. Tulipigana kuwaondoa watu wa
aina hiyo na tuliwatoa. Na kwa kiasi kikubwa tulimkataa mwanaCCM
mwenzetu, Ndg. Edward Lowassa, kwa sababu tuliamini yeye na kundi lake
(lilikokuwa kubwa ndani ya CCM) wangeigawana na kuimaliza nchi yetu.
Ilihitaji uwe mwendawazimu kumkataa ndugu huyu. Lakini tulikita mguu
waziwazi na kumkataa.
Tulionekana wasaliti
wenye kustahili kufukuzwa Chamani. Na wengine tukifikia kufukuzwa Chama
na baadhi ya viongozi wapuuzi, wakiamini viongozi wa aina yetu
hatukutakiwa, mpaka vikao vya juu vilipopuuzia ndipo tulipona. Tulifika
huku sababu kulikuwa na kundi la wachache waliokuwa wanafaidika na mfumo
uliokuwepo, hivyo waliona sisi tunachafua maji yao ya kuogelea. Mpaka
alipokuja Kanali Kinana na kutupongeza wabunge wa aina yetu akisema,
jitengeni na ushenzi wa baadhi ya watu wanaochafua taswira ya Serikali
ya Chama chetu ndipo tulipumua.
Kuna
njia mbili tu unaweza kutatua changamoto zinazotukabili nchini kwa
'uhakika'. Nasema kwa uhakika maana ni aibu kubwa kuinjika chungu cha
ugali nyumbani kwako na kuwapa wanao uhakika wa ugali kumbe unategemea
unga wa kuomba ama kuazima toka kwa jirani! Vipi akikunyima?
Ukichaguliwa
kuwa Rais, una ahadi na dhamana kubwa mabegani mwako, una hamu na
shauku kubwa ya kuanza kuzitekeleza, una ndoto nyingi za kutaka kuleta
mapinduzi kwenye nchi yako kwa heshima kubwa uliyopewa, unataka kuacha
alama isiyofutika!
Unachungulia hazina
unakutana na madeni, mahitaji, utaratibu na masharti; unatazama
makusanyo uliyonayo. Unachoka kabisa! Nguvu zinakuisha kabisa. Hamasa
yako inavurugwa na uhalisia.
Unakumbuka
ushauri wa wabunge kila siku bungeni - 'tubane matumizi...tukate
matumizi yasiyo ya lazima...tuweke kodi hii...ile...Serikali ni dhaifu
kwenye kukusanya kodi....tutanue wigo wa kodi....kwa nini Tanzania na
utajiri wote huu bado tunategemea misaada kutoka nje kwenye bajeti yetu -
mwishowe tutapewa pesa zenye masharti magumu (mambo ya ushoga
nk)...tuanzishe mahakama maalum ya mafisadi, nk!'
Unaanza
kutekeleza yote haya kama yalivyo - unalaumiwa! Tusiwe wepesi wa
kusahau. Tusiwe wanafiki. Ni nani hakuwahi kukerwa na watumishi hewa? Ni
nani hakukerwa na safari za nje? Ni nani alilalamika kuhusu uwepo wa
uwiano wa bajeti ya matumizi ya kawaida mkubwa kuliko bajeti ya
maendeleo? Rais Magufuli toka aingie madarakani, haya ndiyo maswali
anayojaribu kuyapatia majawabu.
Njia
za kupata fedha za kutatua changamoto kwa uhakika ni hizi mbili: moja -
ubane matumizi, ili unacho-save ukipeleke kwingine kikasaidie kupunguza
changamoto zako. Ndicho anachokifanya Rais Magufuli kila siku toka
amechaguliwa. Sisi wenye macho ya kizalendo na kiuhalisia tunaona
jitihada zake.
Mbili, ukusanye zaidi na ubane
mianya ya kuvuja kwa mapato. Ndicho kinachofanyika. Kwa mwaka unaoisha
makusanyo ya mapato ya Serikali yamepita malengo.
Kuna
njia nyingine za kupata fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji yetu.
Japokuwa haina washabiki wengi na inapigwa vita sana na watunga sheria
na wanaharakati mara nyingi. Hii ni ile ya misaada kutoka kwa wafadhili
na mikopo (ya ndani na nje). Hizi njia mbili zote zinapigiwa kelele sana
sababu; Moja, kwamba itasababisha tupewe pesa zenye masharti magumu
tusiyoyaweza, na nyingine, kwamba deni letu linakua sana - mwisho
halitohimilika! Njia ya mikopo ya ndani wanasema inaumiza uchumi wetu
nk.
Kwa
sasa tunachotakiwa kufanya ni kuongeza uzalishaji ili wigo wa serikali
kukusanya kipato chake utanuke zaidi. Na hili si la Rais peke yake, ni
letu sote. Kila mtu awe mzalishaji. Shime twende shambani, twende
viwandani, twende sokoni!
Kwangu
mimi, kama hali inakuwa ngumu kwetu sote na iwe tu, ili mradi wasiwepo
kati yetu wanaofaidika na serikali ya watu huku wengine hawana chakula,
hawana dawa, hawana madawati nk. Napenda usawa, haki na uwajibikaji.
Namuunga mkono Rais wangu kwa sababu analeta usawa kwa watu wetu.
Nasimama na Rais wangu.
Kwangu hili la usawa,
haki na uwajibikaji kwa wote ni kubwa sana. Linagusa historia ya
machozi, jasho na damu ya makuzi yenye maumivu makali na furaha nyakati
nyingine kipindi cha makuzi yangu na watoto wengine wa maskini kwenye
Tanzania ya miaka ya 70 na 80. Maana mimi ni zao la mfumo uliotoa haki
na usawa kwa wote. Bila Tanzania hiyo mtoto wa maskini kama mimi, hata
ningekuwa na bidii na kipaji cha namna gani, nisingefikia kusoma mpaka
kuwa Daktari, na hata kufikia kutamani kugombea nafasi ya ubunge. Sitaki
kufikiri labda ningekuwa wapi mimi leo!
Tufanye
kazi kwa bidii na maarifa, zama zimebadilika. Hakuna mtu atakayethubutu
kutuibia kwenye zama hizi. Walau hili ni la uhakika.
Na
zile kesi za rushwa, wizi wa mali ya umma, matumizi mabaya ya ofisi na
ubadhirifu wa mali ya umma sasa zifike kwenye mahakama yake na kesi
zikimbie ili tuone haki ikitendeka.
Huwezi
kupanda mchicha ukasubiria ukuwe kwa matarajio ya kuvuna bangi. Tulimpa
kura zetu Ndg. Magufuli, mwenye rekodi ya uchapakazi, uaminifu na
uadilifu, basi tutarajie uchapakazi, uaminifu na uadilifu; mwenye rekodi
ya kuacha alama ya kazi yake, basi ni lazima tutarajie kuona kazi
itakayoacha alama. Si vinginevyo.
Tungempa
mla rushwa, tungeshuhudia rushwa. Tumevuna tulichopanda. Tumevuna kazi
tu. Tutulie tuone kazi. Tuamke tufanye kazi. Tushiriki kujenga Tanzania
Tuitakayo.
_____________
Imeandikwa na Dkt. Kigwangalla. Mwandishi ni Mwanafalsafa aliyegeuka kuwa Daktari, Mjasiriamali, Mwanasiasa na Mtunga Sera.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.