ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, June 13, 2017

MBUNGE LIJUALIKALI ATAKA KINGA YA RAIS IONDOLEWE.


Mbunge Kilombero kwa tiketi ya (CHADEMA) Peter Lijualikali, leo bungeni ameshauri bunge liweze kufanya mabadiliko ya sheria ili bunge liweze kuondoa kinga ya Rais ili ma-Rais wote waliofanya makosa waweze kushtakiwa kisheria kama watu wengine.
Lijualikali amesema hayo leo bungeni wakati akitoa maoni yake baada ya jana Rais Magufuli kupokea ripoti ya pili ya uchunguzi wa madini na kusema wao kama wabunge wameshajua ACACIA ni wezi kwa mujibu wa ripoti hiyo. Hivyo amependekeza kinga ya rais iweze kuondolewa ili waweze kushtakiwa kama watu wengine pindi wanapofanya makosa, akidai kuwa haiwezekani Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Wizara husika akafanya maamuzi juu ya madini pasipo Rais kufahamu lolote.

"Kama Taifa tumeona kwamba ACACIA ni wezi kwa mujibu wa Rais na ameshasema kuwa watu waliohusika wafanyiwe kazi, lazima bunge liondoe kinga ya Rais, tufanye 'Amendment' hapa Bungeni marais wa nchi hii wasiwe na kinga ya kutoshtakiwa, kwa sababu hainiingi akilini leo unamwambia Nazir Mustafa Karamagi, huwezi kuniambia mzee wangu huyu Chenge kwamba ahojiwe lakini marais waliopita wanaachwa haiwezekani Chenge afanye makosa rais asijue, haiwezekani baraza lilikuwa halijui. Tufanye 'Amendment' ya sheria marais wote waweze kushtakiwa" alisisitiza Lijualikali

Mbali na hilo Lijualikali alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa vita hii ya madini inapaswa kuwa vita ya taifa zima na si kuwa vita ya mtu mmoja mmoja na kudai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapaswa kuomba radhi kwa wananchi kutokana na hasara ambayo nchi imepata kwa viongozi wake kusaini mikataba mibovu inayolitia taifa hasara kubwa.

Mjadala huu umeibuka leo bungeni baada ya Rais Magufuli jana kukubaliana na mapendekezo kuwa watu wote waliotajwa kwenye ripoti hiyo wanapaswa kuhojiwa ili kujua ukweli ndipo baadhi ya wabunge wamependekeza kuwa Bunge liweze kufanya mabadiliko ya sheria ili waweze kuondoa kinga ya Rais.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.