ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, June 22, 2017

MAJALIWA AMPA WAKATI MGUMU DED WA MISUNGWI.


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Bw. Eliud Mwaiteleke aitishe kikao na wananchi wa Kigongo na kutafuta ufumbuzi wa tatizo la eneo la kujenga soko.

Ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Juni 21, 2017) wakati akizungumza na mamia ya wakazi na wajasiriamali wanaotumia kivuko cha feri cha Kigongo waliokuwa wakimsubiri avuke kwenda Busisi, wilayani Sengerema.

"Mkurugenzi haya mambo ya mipango, mipango na kupanga hayaleti tija kwa wananchi. Hivi hamjui kuwa wananchi wanahitaji kuwa na soko katika eneo hili ili waweze kuuza mazao yao au samaki?"

"Ninakuagiza Mkurugenzi, Alhamisi, saa 4 njoo na Afisa Biashara wako, Mwenyekiti wa kijiji na watu wako pamoja na Diwani wa hapa, itisheni kikao na muonyeshwe eneo la soko ili mliingize kwenye mipango yenu," alisema.

Waziri Mkuu alisema Serikali ya awamu ya tano haitaki kusikia lugha za michakato wakati wananchi wanaendelea kuteseka.

Awali, Waziri Mkuu alimwita Mkurugenzi huyo ili aeleze amejipanga vipi kwenye Halmashauri yake kutatua tatizo la soko kwa wananchi wa Kigongo.

Akitoa majibu mbele ya Waziri Mkuu, Bw. Mwaiteleke alisema hawajawahi kupata mpango kutoka kwenye kata hiyo na kwa hiyo akawasihi wananchi waibue mpango huo na kuuwasilisha kwenye Halmashauri ili wao waweze kutenga fedha za kujenga soko.

Mapema, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigongo, Bw. Sebastian Kisumo alimweleza Waziri Mkuu kwamba eneo hilo linakabiliwa na tatizo la soko pamoja na uhaba wa maji.

Kuhusu maji, Waziri Mkuu alisema Serikali imetenga sh. bilioni 2.5 kwa ajili ya mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria eneo la Itelele ambao utasambaza maji kwenda Misungi, Usagara hadi Kigongo Feri.



Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.