ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, June 8, 2017

KINACHOSUBIRIWA KWA HAMU NA WATANZANIA WOTE HII LEO JUNI 8.

Kuongeza au kupunguza makali ya maisha ndicho kitu kinachosubiriwa na wananchi leo wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango atakapowasilisha bajeti ya pili ya Serikali ya Awamu ya Tano bungeni mjini hapa.

Bajeti ya kwanza ya Sh29.5 trilioni ilionekana kubana sehemu tofauti na kusababisha wananchi wa kila nyanja kulalamika, wengi wakisema mzunguko wa fedha umedhoofika huku biashara zikifungwa.

Bajeti hiyo ndiyo iliyowafanya wachambuzi wa masuala ya uchumi, makundi ya biashara na wabunge kumtaka waziri huyo atangaze hatua mahususi za kuiokoa sekta binafsi na zitakazoharakisha ukuaji uchumi.

Wadau wanatarajia kuwa Dk Mpango, ambaye aliwahi kuwa mchumi mwandamizi katika Benki ya Dunia na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ataangalia kwa kina hali ya sasa ya uchumi na kutangaza hatua za kikodi zitakazozuia kupanda kwa gharama za maisha na wakati huo huo kuipa mkono sekta binafsi ili Serikali ifikie lengo lake kuifanya Tanzania  kuwa nchi ya viwanda.

Mfumuko wa bei, ambao unahusishwa na kupanda kwa bei za vyakula, tayari umefika asilimia 6.4 kwa mwezi Aprili kutoka asilimia 5.1 mwezi kama huo mwaka jana.

“Kwa wengine, hili linaweza kuonekana kama ongezeko dogo lakini kiuchumi ni kubwa mno na tunatarajia serikali inakuja na namna nzuri ya kukabiliana nao katika bajeti hii,” alisema  David Silinde, waziri kivuli wa Fedha na Mipango na mbunge wa Momba (Chadema).

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.