ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, June 25, 2017

BADO UNYANYASAJI WAFANYAKAZI WA NDANI NI TATIZO SUGU.Na James Timber, Mwanza
Shirika la wasaidizi kisheria Jamii Bugogwa (WAJABU)  Kata ya Bugogwa katika Wilaya ya Ilemela  jijini Mwanza, wamewasilisha changamoto  wanazokutana nazo wafanyakazi  wa majumbani na sheria zinazopaswa kufuatwa kwa waajiri na waajiriwa kwenye kikao cha Madiwani, Watendaji wa Kata na Afisa Maendeleo Kata kilichofanyika katika ukumbi wa malezi na makuzi Bugogwa.
 
Mwenyekiti wa Kikao hicho Swila Dede  ambaye ni Diwani wa Kata ya Shibula wilayani Ilemela alisema kuwa sheria ya kumlinda mfanyakazi wa nyumbani  ilitengenezwa mwaka 2011 na kusainiwa mwaka 2012 na  imeleta matokeo chanya kwa baadhi ya maeneo kutokana uhamasishaji wa hali ya juu, baada ya jamii kutoa ushirikiano mkubwa.

Dede alisema kuwa changamoto zinatokana na Afisa watendaji wa mitaa kubadilishwa yale maeneo na wenyeviti wa mitaa kuwa wapya na kutokupata elimu iliyotolewa shirika hilo waliposaini sheria hiyo hapo awali.

“Baada ya Kusainiwa kwa sheria ya wafanyakazi majumbani katika Jamii ya Bugogwa shirika lilihakikisha linatoa elimu huku wenyeviti wa Mtaa na watendaji kata waliokuepo  wakitoa ushirikiano  wa kutosha ambao kwa sasa uongozi umebadilika baadhi ya maeneo na wengi wao kutokujua elimu hiyo”, alisema Dede. 

Afisa Mtendaji wa Kata ya Sangabuye Juma Ngoroma  alisema baadhi wafanyakazi wa nyumbani wanafanyiwa ukatili na waajiri wao na kutosema  kwa kuhofia kuachishwa kazi na kuwataka wafanyakazi hao watumie kaulimbiu ya shirika hilo isemayo “vunja ukimya upate haki yako”.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo Kata ya Shibula Benjamin Prosper alilalamikia wanajamii ambao hawatoi ushirikiano  kwa uongozi ili kuwabaini waajiri ambao wanawanyanyasa watumishi wa majumbani.

“Kuna baadhi ya wananchi wamekuwa hawatoi ushirikiano kwa uongozi ili kuwabaini waajiri wanaowanyanyasa wasaidizi wa nyumbani”, alisema Prosper.

Hata hivyo Afisa Mtendaji wa Kata ya Bugogwa Rashid Sukwa alitoa pendekezo la kuanzisha daftari la  kuwaorodhesha  waajiri wanaofanya vitendo vya ukatili dhidi ya waajiriwa ili jamii iwe wazi na kuwatambua wanaofanya vitendo hivyo.

Mratibu wa Shirika la wasaidizi kisheria Jamii Bugogwa (WAJABU)  Kata ya Bugogwa katika Wilaya ya Ilemela  jijini Mwanza  Emmanuel Mhoja, akiwasillisha changamoto za watumishi wa kazi majumbani alisema baadhi ya watumishi wanalazimishwa kufanya ngono na waajiri na pengine watoto wa waajiri.

Mhoja alisema kuwa watumishi wa majumbani wengi wao hawana  mishahara, kutokana na kutofunga mikataba pale wanapopata ajira hizo na kuchangia kuwepo kwa ajira ya muda mfupi na mimba katika umri mdogo.

“Wafanyakazi majumbani  wengi wao wanapata ajira bila ya mkataba jambo linalochangia kuwepo kwa ajira kwa muda mfupi na bila ya malipo yoyote na kuchangia kuongezeka kwa vijana wasio kuwa na ajira ya mazingira rafiki na salama”, alisema Mhoja.

Akitaja  baadhi sheria  ndogo ndogo ambazo  zilitungwa kwa ajili ya kuwalinda watumishi wa majumbani na jamii ya Bugogwa kusaidiwa na WAJABU ni mwajamii haruhusiwi kuajiri mfanyakazi chini ya miaka 18, mkataba kati ya mwajiri na mwajiriwa ushuudiwe na Mwenyekiti wa Mtaa, Mwajiri amtambulishe  mwajiriwa  baada ya siku 3 kupewa ajira kwa uongozi wa Mtaa na kata.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.