ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, April 2, 2017

MVUA WILAYANI IRAMBA, YAWAKOSESHA ZAIDI YA WANAFUNZI 150 VYUMBA VYA KUSOMEA.

 baadhi ya vyumba vya madarasa ya shule ya sekondari New Kiomboi,wilayani Iramba,Mkoani Singida vilivyoezuliwa paa kufuatia mvua kubwa iliyoambatana na upepo iliyonyesha kwa takribani nusu saa na hivyo kuwakosesha zaidi ya wanafunzi 150 vyumba vya kusomea.

 Ni baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tatu na nne katika shule hiyo waliokuwa wakijisomea nje ya vyumba vya madarasa wakisubiri kuingia kwa zamu darasani kufanya mitihani yao

NI baadhi ya bati za majengo ya shule ya sekondari New Kiomboi,iliyopo wilayani Iramba,Mkoani Singida yaliyoezuliwa katika vyumba vya madarasa,ofisi ya mkuu wa shule pamoja na ofisi za walimu wa shule hiyo.

MVUA kubwa iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha kwa takribani nusu saa imeezua mapaa ya majengo ya shule ya sekondari New Kiomboi,iliyopo wilayani Iramba,Mkoani Singida imesababisha zaidi ya wanafunzi 150 kukosa vyumba vya kusomea na hivyo kulazimika kutumia majengo mawili ya vyumba vya maabara viliyopo katika shule hiyo.

Mkuu wa shule hiyo,Lameck Ayeiko alisema kuwa tukio hilo lilitokea Machi,24,mwaka huu saa kumi jioni ambapo mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali ilinyesha kwa muda wa takribani nusu saa na hivyo kusababisha pia ofisi ya Mkuu wa shule na ofisi za walimu kuezuliwa paa na kujaa maji kwenye vyumba hivyo na kwamba zaidi ya shilingi milioni 20 zinahitajika kurudisha majengo hayo katika hali ya kawaida.

“Ili kurudisha yale majengo katika hali yake ilivyokuwa zilikuwa zinahitajika jumla ya shilingi milioni 13,648,lakini kuboresha yale madarasa ili yakae vizuri sasa, kulikuwa kunatakiwa kuwe na ongezeko la kama shilingi milioni 6,511,000/= karibu milioni ishirini”alisisitiza mwalimu huyo.

Kufuatia tukio hilo Mkuu wa shule huyo alisema walilazimika kufanya mkutano wa hadhara kwa kuwashirikisha wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo na kufikia makaubaliano kwa kila mzazi kuchangia shilingi 10,000/=ambapo papo kwa papo zilipatikana zaidi ya shilingi laki tano kwa ajili ya ukarabati wa majengo hayo.

Alipotakiwa kuzungumzia maafa hayo,Mkuu wa wilaya ya Iramba,ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa kamati ya maafa wa wilaya hiyo,Emmanuel Luhahula alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kwamba baada ya kufanyika kwa tathimini ya uharibifu huo walibaini zaidi ya shilingi milioni 20 zinahitajika kurejesha majengo hayo katika hali yake ya kawaida.

Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba,Mariether Kasongo aliweka wazi kuwa kati ya shilingi milioni 30 hadi 35 zinahitajika kukarabati majengo yaliyoathirika kutokana na mvua hiyo iliyonyesha kwa muda wa nusu saa.

Shule ya sekondari New Kiomboi iliyoezuliwa mapaa ya baadhi ya majengo yake kwa zaidi ya wiki moja sasa,lakini hakuna kiasi chochote cha fedha kilichotengwa na Halmashauri hiyo kwa ajili ya kurejesha hali ya majengo ya shsule hiyo.

Shule ya sekondari New Kiomboi,iliyopo Tarafa ya Kisiriri,wilayani Iramba,Mkoani Singida ipo katika Programu ya SEDP na fedha kwa ajili ya kuhakikisha shughuli za kuboresha majengo ya shule hiyo yanatekelezwa kupitia mpango huo zinapatikana.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.