YANGA
imevuliwa taji la pili msimu huu, baada ya kutupwa nje ya michuano ya
Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inayojulikana kama Azam
Sports Federation Cup (ASFC) kufuatia kipigo cha 1-0 kutoka kwa Mbao FC
katika mchezo wa Nusu Fainali jioni ya leo Uwanja wa CCM Kirumba,
Mwanza.
Mapema
mwanzoni mwa msimu, Yanga ilivuliwa taji la Ngao ya Jamii baada ya
kufungwa na Azam FC kwa penalti 4-1 kufuatia sare ya 1-1 katika mchezo
wa kuashiria ufunguzi wa msimu mpya, Agosti 17, mwaka jana.
Na
sasa Yanga ina jukumu la kutetea taji lake moja lililobaki na kubwa
zaidi, la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ambako wanakabana koo na
wapinzani wao wa jadi, Simba SC.
Katika
mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Erick Onoka wa Arusha, aliyesaidiwa
na Julius Kasitu na Mdogo Makame wa Shinyanga hadi mapumziko, tayari
Mbao walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0.
Ni
Yanga wenyewe waliojifunga bao hilo dakika ya 27, baada ya beki wake,
Andrew Vincent ‘Dante’ kuunganishia nyavuni kwake krosi ya Pius Buswita
katika harakati za kuokoa.
Mbao walibadilisha mfumo wa uchezaji baada ya bao hilo na kuanza kucheza kwa kujihami, jambo ambalo liliwasumbua Yanga.
Kipindi
cha pili, Mbao walifanikiwa kuendekea kuwabana Yanga na kujilinda vyema
hatimaye kuandika historia ya kuwa timu ya kwanza ya Mwanza na ya nje
ya Dar es Salaam kwa ujumla kufika fainali ya Kombe la TFF.
Na
sasa Mbao FC watakutana na Simba SC katika fainali ya michuano hiyo
baadaye mwezi huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Simba iliwatoa
washindi wa pili wa msimu uliopita, Azam FC kwa 1-0 jana, bao pekee la
Mohammed Ibrahim.
Kikosi
cha Mbao FC kilikuwa; Benedict Haule, David Mkwasa, Alex Ntiri,
Boniface Maganga, Salmin Hoza, Yussuf Ndikumana, Jamal Mwambeleko,
George Sangija, Everigustus Bernard/ Robert Ndaki dk73, Pius Buswita na
Ibrahim Njohole.
Yanga
SC; Deogratius Munishi ‘Dida’, Hassan Kessy/Juma Abdul dk67, Mwinyi
Mngwali, Andrew Vicent ‘Dante’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Said Juma
‘Makapu’/Geoffrey Mwashiuya dk46, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Obrey
Chirwa/Emmanuel Martin dk83, Amissi Tambwe na Haruna Niyonzima.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.