ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, March 7, 2017

YANGA 6-1 KILUVYA 1 KOMBE LA TFF.


YANGA SC imefanikiwa kwenda Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ushindi wa kishindo wa mabao 6-1 dhidi ya Kiluvya United ya Pwani katika mchezo wa kukamilisha hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo inayojulikana pia kama Azam Sports Federation Cup (ASFC).

Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, mshambuliaji Mzambia Obrey Chirwa alifunga mabao manne peke yake, huku mengine yakifungwa na viungo Geoffrey Mwashiuya na Juma Mahadhi.Yanga sasa itamenyana na Prisons katika Robo Fainali Machi 18, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Robo fainali nyingine zitakuwa kati ya Simba SC na Madini FC Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Azam FC na Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na Kagera Sugar na Mbao FC ya Mwanza Uwanja wa Kaitaba.

Katika mchezo wa leo uliochezeshwa refa hodari anayechipukia nchini, Kheri Sasii, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-1.

Winga Geoffrey Mwashiuya alianza kuwafungia Yanga bao la kwanza dakika ya 11 kwa shuti kali baada ya kuwatoka vizuri wachezaji wa Kiluvya United kuanzia katikati pembezoni mwa Uwanja kushoto kufuatia pasi ya beki wa kushoto, Oscar Joshua.

⁠⁠⁠mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa akaifungia Yanga bao la pili dakika ya 24 kwa shuti kali pia baada ya pasi nzuri ya kutanguliziwa na mshambuliaji pacha wake leo, Juma Mahadhi.

Chipukizi Edgar Charles Mfumakule akamtoka vizuri beki Mtogo, Vincent Bossou baada ya pasi ya Shala Juma na kumtungua kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ kuipatia Kiluvya United bao la kufutia machozi.

Chirwa akaifungia Yanga mabao mawili mfulilizo dakika za 45 akimalizia pasi ya Juma Mahadhi na dakika ya 70 akimalizia krosi ya Hassan Kessy kukamilisha hat trick yake ya kwanza tangu ajiunge na timu hiyo Julai mwaka jana kutoka FC Platinums ya Zimbabwe.

Juma Mahadhi akaifungia Yanga bao la tano dakika ya 74 kwa shuti la umbali wa mita 21 hadi misuli ikambana. Yanga ilicheza pungufu tangu dakika ya 74 baada ya Mahadhi kuumia misuli na kutoka nje, wakati wamekwishatimiza idadi ya wachezaji watatu wa kubadili.

Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deogratias Munishi ‘Dida’, Hassan Kessy, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Said Juma ‘Makapu’/Justin Zulu dk48, Yussuf Mhilu/Emmanuel Martin dk35, Deus Kaseke, Juma Mahadhi, Obrey Chirwa na Geoffrey Mwashiuya/Simon Msuva dk44.

Kiluvya United: Philimoni Ramadhani, Nassor Abubakar/Hashik Fakhi dk62, Ramadhani Ally, Jagani Mvugalo, Aloyce Nkya, Mwita Emmanuel, Yohana Richard, Hassan Ayoub, Edgar Charles/Juma Mohammed dk79, Shala Juma na Mwinyi Rehani/Ramadhani Said dk79.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.