ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, March 16, 2017

KITUO CHA EATV NA TAASISI YA HAWA YAWASHUKURU WATANZANIA KWA KUFANIKISHA KUCHANGIA KAMPENI YA 'NAMTHAMINI'

Afisa Masoko wa East Afrika Radio Basilisa Biseko akizungumza mbele ya waandishi wa Habari (hawapo pichani),mapema leo jijini Dar,kuhusua mafanikio yaliyopatikana kupitia kampeni ya 'NAMTHAMINI',Basilisa amebainisha kuwa kupitia EATV na East Africa Radio pamoja na Taasisi ya Haki za Wanawake (Hawa Foundation) imefanikiwa kukusanya michango ya fedha taslim na pakiti za pedi zitakazowawezesha takribani wanafunzi wa kike wapatao 673 kutokukosa masomo yao kwa muda wa mwaka mzima.Pichani kulia ni Mratibu wa Vipindi Eastafrika Radio,Irene Tillya na kushoto ni Mratibu wa Vipindi EATV,Sophie Proches.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki za Wanawake (HAWA) , Joyce Kiria akifafanua jambo kuhusiana na mafanikio makubwa waliyoyapata kupitia kampeni hiyo ya 'NAMTHAMINI',Kiria emesema kuwa Katika kampeni hiyo ambayo wananchi walijitokeza kuichangia katika kuonesha kumjali mtoto wa kike aliyepo shuleni zilichangwa jumla ya shilingi 20,176,110, ambazo fedha taslim shilingi 11,774,610 na pedi za thamani ya shilingi 8,401,500.
 Afisa Masoko wa East Afrika Radio Basilisa Biseko akifafanua zaidi mbele ya Waandishi wa habari (hawapo pichani),kuhusiana na mafanikio ya kampeni hiyo 'Namthamini',iliyolenga katika kuchangia pedi (Taulo za Kike) kwa wanafunzi wa Sekondari,ambapo takwimu zinaeleza kuwa karibia asilimia 45 ya wanafunzi wa kike hukosa masomo wakiwa katika hedhi kutokana na kukosa pedi za kujistiri.
 Baadhi ya Waandishi wa habari wakifuatilia mkutano huo uliofanyika mapema leo jijini Dar.

-------   ------   ------  ----------


Kituo namba moja kwa vijana East Africa Television (EATV) Limited kikishirikiana na Taasisi ya Haki za Wanawake (HAWA foundation) kinapenda kutoa shukrani za dhati, kwa umma wa watanzania  kwa  kufanikisha kuchangia kwenye kampeni ya Namthamini.

Namthamini  ni kampeni iliyolenga katika kuchangia pedi (Taulo za Kike) kwa wanafunzi  wa Sekondari, kutokana na takwimu kuonesha karibia asilimia 45 ya wanafunzi wa kike hukosa masomo wakiwa katika hedhi kutokana na kukosa pedi za kujistiri.

Kwa wastani wanafunzi wa kike wengi hupoteza siku tano hadi saba kila mwezi kutokana na ukosefu wa pedi za kujisitiri, na kwa mwaka inakadiriwa kukosa masomo kwa takribani siku 60 hadi 70.

EATV na East Africa Radio katika kufikisha mchango wake kwa jamii, na kwa kuangalia Siku ya Wanawake Duniani, Machi mosi tuliamua kuanzisha kampeni hii kwa kuishirikisha jamii ili kumuwezesha mwanafunzi wa kike asikose masomo yake na kumfanya kutofikia lengo lake kimasomo kwa kukosa pedi pale awapo kwenye hedhi.

EATV na East Africa Radio pamoja na Taasisi ya Haki za Wanawake (Hawa Foundation) imefanikiwa kukusanya michango ya fedha taslim na pakiti za pedi zitakazowawezesha takribani wanafunzi wa kike wapatao 673 kutokukosa masomo yao kwa muda wa mwaka mzima.

Katika kampeni hii ambayo wananchi walijitokeza kuichangia katika kuonyesha kumjali mtoto wa kike aliyepo shuleni zilichangwa jumla ya shilingi 20,176,110, ambazo fedha taslim shilingi 11,774,610 na pedi za thamani ya shilingi 8,401,500.

Michango yote ya fedha iliyopatikana itatumika katika kununua pedi na zitaelekezwa moja kwa moja katika shule za Sekondari 20 zenye uhitaji zilizoteuliwa kupata msaada huu, katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Lindi, Pwani na Tanga.

Uongozi wa EATV Limited na Taasisi ya Haki za Wanawake (Hawa Foundation) inapenda kutumia nafasi hii kwa dhati kuwashukuru wananchi wote walioguswa na tatizo la pedi kwa wanafunzi wa kike na kuichangia kampeni ya Namthamini na kuonyesha kuwa kwa pamoja tunaweza. Sisi EATV husema Together Tunawakilisha.

Mwisho kabisa tunapenda kusisitiza kuwa tatizo la wanafunzi wa kike kukosa kuhudhuria shuleni kutokana na kukosa pedi za kujisitiri ni la kwetu sote hivyo East Africa Television Limited pamoja na Taasisi ya Haki za wanawake inatoa wito kwa jamii kuendelea kuungana kwa pamoja katika kusaidia watoto wa kike kupata mahitaji muhimu wawapo shuleni, ili wapate kusoma kwa amani pasipo kukosa kuhudhuria darasani.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.