ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, March 25, 2017

CHADEMA KUTUMIA BUNGE KUFAFANUA HALI YA SIASA NCHINI.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitautumia Mkutano wa Saba wa Bunge la Bajeti utakaoanza Aprili 4 kufafanua hali ya kisiasa ilivyo nchini.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema jana kuwa chama chake ndicho kinachoongoza kambi rasmi ya upinzani bungeni na kitautumia mhimili huo kuikosoa Serikali.

“Haki inapovunjwa mahali popote pale, hata inapovunjwa juu ya mwanaCCM na juu ya raia yoyote wa Tanzania hatusiti kutoa kauli ya kukemea na kutaka hatua kuchukuliwa, ”alisema Mnyika.

Alisema katika Bunge lijalo, wabunge wa upinzani na wa CCM watakuwa kitu kimoja katika kuchukua hatua hivyo Watanzania watarajie Bunge litakalokuwa limechangamka.

Alisema kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kilichofanyika  Machi 22 na 23 kilijadili hali ya kisiasa na vyombo vya habari nchini.

“Matukio yaliyojitokeza hivi karibuni yanagusa uhuru wa vyombo vya habari, jambo kubwa linaloonekana bayana ni matumizi mabaya ya wazi ya madaraka yanayofanywa na baadhi ya viongozi,” alisema

Alisema katika siku za karibuni kumekuwa na matumizi mabaya ya silaha. “Tunalaani kwa kiwango kikubwa sana matumizi mabaya ya madaraka na matumizi mabaya ya vyombo vya dola hasa yanapofanyika hadharani.”

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Kibamba, alimpa pole mbunge wa Mtama Nape Nauye kwa tukio la juzi la mtu anayedaiwa kuwa ni askari kanzu kumtolea bastola hadharani. Alisema upinzani umekuwa ukikilalamika kuhusu matumizi mabaya ya silaha na kuonekana unapiga kelele, lakini sasa kila mmoja anaona hali ilivyo na inamgusa.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.