ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, March 22, 2017

CCM YATAKA VYETI VYA WAGOMBEA EALA.

Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Daniel Fred Kidega

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wagombea wa ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kupitia chama hicho, kwenda na vyeti vya taaluma katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu Lumumba jijini Dar es Salaam ili kuvihakiki.

Wagombea wote waliochukua fomu kutoka vituo vya Dodoma, Zanzibar na Dar es Salaam wanatakiwa kuripoti Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba Dar es Salaam keshokutwa saa 3.00 asubuhi wakiwa na vyeti vyao vya taaluma pamoja na hati ya kusafiria au kadi ya kupigia kura.

Wakizungumza na gazeti hili, wagombea waliofika kuchukua fomu kutafuta tiketi ya kugombea nafasi tisa za kuingia kwenye Bunge la Afrika Mashariki, walisema wanatakiwa kufika katika ofisi hiyo wakiwa na vyeti vyao vya taaluma.

Wagombea hao wanatakiwa kuwapo ofisini hapo siku moja baada ya kujaza fomu na na kuzirudisha na kwamba siku ya mwisho ya kurudisha ni kesho saa 10.00 jioni.

Akizungumza mjini hapa baada ya kuchukua fomu, mgombea Watson Mwakwalila (31) ambaye ni mtaalamu wa masuala ya upimaji wa ardhi, alisema anaingia katika kinyang’anyiro cha kutafuta nafasi moja kati ya tisa za ubunge wa Afrika Mashariki ili akatetee na kupigania masuala ya ardhi.

“Nataka kuacha historia kwamba mgombea aliyewahi kugombea uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, amepigania masuala ya ardhi katika Bunge la Afrika Mashariki,” alisema Mwakwalila.

Mgombea mwingine, Pius Lufutu (28) aliywakuwa wa 55 kuchukua fomu katika kituo cha Dodoma, na akiwa ni mtaalamu wa masuala ya Uhusiano wa Umma na Masoko, amesema anataka kuwa mbunge wa EALA ili kupigania ushindani wa bidhaa katika soko la Afrika Mashariki.

“Nataka kuingia nafasi hiyo kwanza kutoa woga ambao vijana wengi wa Tanzania wanao, kwa kupigania soko la mazao kwa vijana na akinamama ambao ni wajasiriamali wengi,” alisema Lufutu na kuongeza kuwa, vijana wengi wamejitokeza ili kuingia bungeni kutetea maslahi ya vijana na pia lugha ya Kiswahili ambayo ni lugha ya Afrika Mashariki.

Kitendo cha CCM kuwataka makada wake waende na vyeti, kinalenga kuchagua wenye sifa za kweli kuwania ubunge huo.

Watahakikiwa vyeti kuanzia keshokutwa saa 3 asubuhi na baada ya kuhakikiwa, wenye vyeti bandia wataondolewa na wengine wataingia kuhojiwa kwenye KamatiKuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na wachache watafikishwa mbele ya Bunge la Jamhuri ili kupigiwa kura na kubaki tisa tu kuwa wabunge wa wakilishi kutoka Tanzania kwenye Bunge hilo.

Bunge la Afrika Mashariki ni chombo cha Jumuiya ya Afrika Masharki kilichoanzishwa chini ya Ibara ya 9 ya Mkataba wa Uanzishaji Jumuiya hiyo na kwa sasa lina nchi tano wanachama ambazo ni Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini kila nchi inatakiwa kutoa wabunge tisa kwa ajili ya kuunda bunge hilo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.