ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, March 28, 2017

AHMED KATHRADA, MSHIRIKA WA MANDELA KATIKA KUPAMBANA NA 'APARTHEID' AMEAGA DUNIA.


Ahmed Kathrada, mwanaharakati wa mapambano dhidi ya mfumo wa ubaguzi wa rangi wa 'Apartheid' nchini Afrika Kusini na mmoja wa washirika wakuu wa shujaa wa nchi hiyo Mzee Nelson Mandela amefariki dunia. 
Kathrada, ambaye alikuwa amelazwa hospitali mapema mwezi huu kutokana na kuganda damu ubongoni, amefariki leo asubuhi mjini Johannesburg akiwa na umri wa miaka 87.

Marehemu Ahmed Kathrada alizaliwa mwaka 1929 katika mji mmoja wa kaskazini magharibi mwa Afrika Kusini kutokana wazazi wahajiri kutoka India.

Kutoka kushoto: Ahmed Kathrada, Winnie Mandela, Nelson Mandela na Walter Sisulu mara baada ya Mandela kuachiwa huru 1990
Katika enzi za ubaguzi wa rangi wakati wa utawala wa makaburu wachache, Kathrada alitumikia kifungo cha miaka 26 jela, muda mwingi akiwa pamoja na Mzee Mandela, kwa makosa ya kufanya hujuma mbalimbali dhidi ya utawala huo wa kibaguzi.

Mwaka 1964, mwanaharakati huyo wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, alihukumiwa kifungo cha maisha jela ambapo alitumikia kifungo hicho kwa muda wa miaka 26 na miezi mitatu.
Ahmed Kathrada na Nelson Mandela enzi za uhai wao
Baada ya kutokomezwa mfumo wa ubaguzi wa rangi, kuanzia mwaka 1994 hadi 1999, marehemu Kathrada aliteuliwa na Rais Nelson Mandela kuwa mshauri wake wa masuala ya bunge katika serikali ya kwanza ya chama cha ANC.

Ripoti zinaeleza kuwa, leo ilikuwa siku ya huzuni nchini Afrika Kusini kufuatia kifo cha veterani huyo aliyejulikana zaidi kama "Mjomba Kathy".

Wakati wa mazishi ya Mzee Nelson Mandela, Ahmed Kathrada alitoa hotuba ya kusisimua ambapo alisema ameondokewa na kaka.

Marehemu Kathrada akihutubia hafla ya kumuenzi hayati Mandela.

Kathrada aliendelea na harakati za kisiasa hadi siku za mwisho wa uhai wake ambapo mwaka uliopita aliungana na maveterani wengine waliokosoa serikali ya sasa ya chama tawala cha ANC hususan Rais Jacob Zuma anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi na ubadhirifu na kumwandikia barua ya wazi kiongozi huyo akimtaka ang'atuke madarakani

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.